ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, October 25, 2015

Kasoro kibao upigaji kura

By Waandishi Wetu, Mwananchi

Sumbawanga/Vunjo/Bukoba. Watu wasiojulikana wameteketeza kwa moto vifaa vya kupigia kura wilayani Sumbawanga, huku wasimamizi wasaidizi watatu wa uchaguzi katika Jimbo la Vunjo wakipigwa na kujeruhiwa kwa madai ya kusambaza kura zisizo halali.

Kutokana na tukio hilo la Sumbawanga, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeahirisha uchaguzi wa ubunge na udiwani isipokuwa wa rais. Katika tukio hilo, watu hao wanadaiwa kulizuia gari lililokuwa likisafirisha vifaa vya kupigia kura kwenda Tarafa ya Milepa, Bonde la Ziwa Rukwa usiku wa kuamkia jana. Kati ya vifaa vilivyokuwamo kwenye gari hilo ni makasha 45 ya kuhifadhia kura.

Inadaiwa kuwa watu hao waliteketeza vifaa hivyo kwa madai kwamba vilikuwa na kura ambazo tayari zilikuwa zimeshapigwa.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu jana, msimamizi wa uchaguzi wa wilaya ya Sumbawanga, Adam Missana alikiri kutokea kwa tukio hilo katika kijiji cha Zimba kati ya saa 3:00 na 4:00 usiku wa kuamkia jana.

Missana, ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa Wilaya ya Sumbawanga, alisema vifaa vyote, ambavyo ni karatasi za kupigia kura za wagombea wa urais, ubunge, na udiwani, taa, kalamu na makabrasha 45, vimechomwa moto.

Mkurugenzi huyo alifafanua kuwa baada ya kusambaza vifaa vya kupigia kura katika kata ya Zimba, walikuwa wakielekea kituo cha mwisho majira ya saa 12:00 jioni, lakini askari waliokuwa wakisindikiza vifaa hivyo waligoma kuendelea na safari kwa madai kuwa wangefika Kata ya Milepa usiku mwingi.

“Msimamizi msaidizi wa jimbo, Charles Mwita aliwasihi waendeleee na safari lakini walikataa, hivyo gari hilo liliendelea na safari kwenda Milepa bila ya kuwa na ulinzi wa polisi hadi walipovamiwa na watu hao ambao waliweka mawe barabarani kijijini Zimba,” alisisitiza.

“Walishusha vifaa vyote vya kupigia kura kutoka ndani ya gari wakanyonya mafuta kutoka kwenye gari hilo kisha wakayatumia kuchomea vifaaa hivyo,” alieleza.

“Maofisa wasaidizi wawili wa uchaguzi na dereva wa gari hilo lililotekwa walijeruhiwa na kuporwa simu zao na vitu vingine vya thamani,” alisema Missana na kuongeza kwamba baada ya gari kutekwa maofisa hao, waliokuwa wametoka kwenye mafunzo, walifanikiwa kukimbia na kujificha.

Mkurugenzi huyo alisema baada ya kuwasiliana na NEC uchaguzi wa wabunge na madiwani umeahirishwa isipokuwa wa urais.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Kamanda Mwaruanda alidai kuwa watu wapatao 200 waliokuwa na mapanga, marungu, mawe na mikuki, waliweka mawe makubwa barabarani na kulizuia gari lililokuwa likisafirisha vifaa hivyo.

Alieleza kuwa gari hilo lililokuwa na maofisa wawili wasaidizi wa uchaguzi na dereva, lilizuiliwa na watu hao ambao walichoma vifaa vyote vya kupigia kura. Kamanda Mwaruanda alisema watu wanane wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuhusika kwenye tukio hilo.

Kwa mujibu wa Mwaruanda hakuna mtu aliyejeruhiwa katika tukio hilo.

Wasimamizi wapigwa Vunjo

Katika Jimbo la Vunjo, wasimamizi wasaidizi watatu wamejeruhiwa baada ya kupigwa na wananchi waliohisi kulikuwa na masanduku yenye kura zilizokwishapigwa yaliyokuwa yakisafirishwa usiku wa kuamkia jana.

Tukio hilo liliwalazimu polisi kupiga mfululizo mabomu ya machozi kwa nyakati tofauti kati ya saa 5:00 na saa 8:00 usiku wa kuamkia jana ili kuwatawanya wananchi waliofurika kituo cha polisi cha Himo.

Tafrani hiyo iliibuka baada ya wasimamizi hao kukamatwa na wananchi kati ya eneo la Marangu Kilema na mji mdogo wa Himo wakiwa na gari lililodaiwa kuwa la kada wa CCM.

Baada ya kukamatwa na masanduku hayo ya kura yakiwa na karatasi ambazo hazijapigwa bado, wananchi hao waliwapiga wasimamizi hao hadi kuwajeruhi.

Akithibitisha tukio hilo, kamanda wa polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Fulgence Ngonyani alisema polisi walilazimika kutumia nguvu za ziada kutawanya watu hao.

“Baada ya wasimamizi kukamatwa na kupelekwa kituo cha polisi cha Himo, taarifa zilizagaa na kuvuta wananchi wengi waliofurika kwenye hicho kituo,” alisema Ngonyani.


Alisema polisi waliwataka watawanyike, lakini wakagoma na kuanzisha vurugu hali iliyowalazimu polisi kutumia nguvu ya ziada kuwatawanya. Habari zaidi zinasema wananchi walifunga barabara zote zinazoingia mjini Himo huku wakikagua kila gari lililokuwa linapita na wale waliokaidi kusimama ili wakaguliwe, magari yao yalivunjwa vioo kwa mawe, hali iliyowalazimu polisi kutumia mabomu kuwatawanya.

Kamanda Ngonyani alisema matairi manne ya gari hilo yaliharibiwa na watu hao.

Kituoni hapo alikuwapo Augustino Mrema, mgombea ubunge wa Jimbo la Vunjo kwa tiketi ya TLP na James Mbatia anayegombea kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi. Msimamizi wa uchaguzi, Fulgence Mponji pia alifika kituoni na kuwatambua kuwa ni watumishi hao wa NEC.

Mrema alikataa kuzungumzia suala hilo akisema alimkabidhi jukumu hilo kijana wake ambaye alikuwa hajampata.

“Tukiwa pale polisi tuliambiwa kila mmoja ateue mtu atakayeshiriki kuzihakiki pamoja na msimamizi. Kuna kijana wangu nilimpa hiyo kazi mpaka sasa bado sijakutana naye anipe mrejesho,” alisema.

Kwa upande wake, Mbatia aliilaumu NEC kwa kutaka kuvuruga uchaguzi huo kwa kuwapa wasimamizi vifaa nyeti vya uchaguzi kusafirisha bila ulinzi wa askari.

Meneja ajeruhiwa Kilimanjaro

Mjini Moshi, gari la mmoja wa meneja wa kampeni wa mgombea ubunge wa Jimbo la Moshi Vijijini kwa tiketi ya CCM, Dk Cyrill Chami, limeshambuliwa na kuharibiwa vibaya na wananchi wakilishuku kuwa na kura bandia.

Katika tukio hilo lililotokea saa 10:00 alasiri katika kijiji cha Uru Kitandu, Kizitto George, ambaye ni mmoja wa mameneja wa Dk Chami, aliokolewa na Polisi lakini akiwa ameshaumizwa kwa kipigo.

Gari hilo aina ya Toyota Verosa lilivunjwavunjwa vioo, kung’olewa magurudumu yake, kutolewa redio na vifaa vingine.

Katibu wa zamani wa Dk Martin Mallya alisema gari hilo halikuwa limebeba kura yoyote ila kinachoonekana walikuwa wakimuwinda kwa muda mrefu.

“Hivi ninavyoongea na wewe niko hapa Polisi Majengo ili kufuatilia nijue amepelekwa hospitali gani, lakini nimeambiwa gari limeharibiwa vibaya,” alisema Mallya ambaye aliwahi kuwa diwani wa kata ya Okaoni Kibosho kwa tiketi ya CCM.

Karatasi zagundulika shuleni Bukoba

Wilayani Bukoba, karatasi za kupigia kura ambazo ziliwekewa alama ya vema kwenye sehemu za wagombea wa udiwani, ubunge na urais, ziligundulika nyuma ya bweni la Shule ya Sekondari ya Kahororo.

Karatasi hizo zilikuwa zimesambaa nyuma ya bweni la wanafunzi wa kidato cha sita, hali iliyowafanya wanafunzi wahisi kuwapo kwa karatasi zaidi ndani ya mabweni. Mmoja wa wanafunzi alisema karatasi hizo zilisambaa nyuma ya bweni hilo baada ya mwanafunzi mmoja kuzirusha kupitia dirishani kutokana na kutuhumiwa kutumiwa na mmoja wa wagombea kwenye jimbo hilo lenye ushindani mkali kati ya Chadema na CCM.

Mmoja wa walimu, Charles Rushinge alisema aligundua karatasi hizo wakati akikagua mazingira ya shule na baadaye kutoa taarifa kwa vyombo husika kwa ajili ya kuchukua hatua.

Hata hivyo, pamoja na kamanda wa polisi wa Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi kufika shuleni hapo kushuhudia tukio akiwa na baadhi ya maofisa usalama, bado hakuwa tayari kutoa ufafanuzi wa idadi ya karatasi za kura na chanzo cha tukio hilo. Tukio hilo limeibuka huku yakiwepo malalamiko mengi katika vituo vya Kata ya Kashai kuwa kuna karatasi zimenyofolewa kutoka kwenye baadhi ya vitabu vya kupigia kura, ikiwa ni pamoja na kituo cha Zahanati ya Kashai na Shule ya Msingi na Mafumbo.

Mkurugenzi wa uchaguzi wa Jimbo la Bukoba Mjini, Aron Kagurumjuri aliwataka wananchi wapige kura na kudai alipokea vitabu kutoka NEC vikiwa vimefungwa kwenye maboksi, hivyo tatizo la karatasi hizo za kura si lake.

Imeandikwa na Mussa Mwangoka, Daniel Mjema na Phinias Bashaya.

2 comments:

Unknown said...

Hadaa za baadhi ya watu kuweka picha feki za matukio ya kusambazwa na kukamatwa kura feki. Na kauli za baadhi kama si wote za viongozi wa upizani kuwaaminisha wafuasi wao kuwa kura zitaibiwa bila ya ushahidi wowote kwa kiasi kikubwa ndio waliosababisha kasoro hizo zilizotokea. Ikumbukwe upizani huohuo ndio uliokataa watumishi wa serikali kama walimu kuwa wasimamizi wa vituo vya kupigia kura kwa madai ya kutokuwaamini sasa utaona hao watu waliowapendekeza wao baadhi yao wamejishirikisha na hujuma katika zoezi hilo la upigaji wa kura usifanyike kwa ufanisi na amani na utaona wao ukawa na chadema haraka haraka linapotokezea jambo wanakimbilia kuilaumu serikali ya CCM. Kwa kweli ni vigumu kufahamu nini hasa malengo ya ukawa katika uchaguzi huu, kuwa walitaka usifanyike au kuwapotosha wananchi na jumuiya za kimaifa kwamba hata CCM ikishinda kwa haki itakuwa imeiba kura? Kwani katika kila tukio baya lililojitokeza katika uvunjifu wa amani basi wafuasi wa ukawa wao ndio chanzo cha matukio hayo . Hata hizo wanazoziita kura feki wanazodai kuzikamata katika eneo la shule huko bukoba utakuwa ni mchezo mchafu wa chadema/ukawa katika ile mikakati yao kuwatia hofu wananchi wasishiriki kugiga kura kwa amani ilimradi tusubiri na tuone kwani tunaamini ukawa watafanya mabaya zaidi hasa ikitokezea kushindwa uchaguzi.

Anonymous said...

Wache waweke picha zao wanazozitaka na pia uongo wao lakini haitasaidia kwani jahazi tayari limeshakitoa na sasa liko masafa marefu. #Hapa kazi tu.