Mkurugenzi wa Uchaguzi, Kailima Kombwey alisema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya masuala mbalimbali yaliyojiri katika uchaguzi mkuu uliofanyika jana. Kailima alisema uchaguzi umekwenda vizuri.
Alieleza kuwa matokeo ya awali, yataanza kutolewa leo asubuhi na yatakuwa yanatolewa kwa awamu tatu au nne kwa siku kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 12 jioni. “Tunatarajia Mungu akijalia, siku ya tarehe 29, saa tatu asubuhi, tutatangaza nani mshindi wa kiti cha rais, na tarehe thelathini tutamkabidhi cheti chake aendelee na shughuli zake,” alisema Kailima.
Alisisitiza, “tume hatuna mbeleko…hatuna mbeleko ya kubeba mtu… Tutatangaza matokeo kama yatakavyokuwa. Koleo tutaita koleo, kisu tutaita kisu.” Alisema watatangaza ushindi wa kiti cha udiwani, ubunge na urais kulingana na idadi ya kura zilizoko kwenye masanduku ya kura.
Alisema wapo baadhi ya watu waliokuwa wakizungumza kupitia kwenye vyombo vya habari, kujenga mashaka na kuhoji uhalali wa NEC wakati tume hiyo ni huru na isiyoingiliwa na mtu.
“Si lazima utamke neno huru,” alisema na kusema sheria inatamka kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi itakuwa ni idara huru inayojitegemea, haitaingiliwa na mtu na taasisi yoyote ile.
Mkurugenzi huyo wa uchaguzi alipongeza kile alichoita ukomavu mkubwa wa Watanzania, walioonesha kwenye uchaguzi huu ukafanyika kwa amani. Alisema pamoja na kwamba tume ilijiandaa vyema, pia Watanzania wameonesha ukomavu, kiasi cha uchaguzi kutofautiana na wa mwaka 2005 na 2010 ambao zilishuhudiwa vurugu.
“Tunaendelea kukomaa na hii ni sifa bora, wale waliokuwa wanadhani sasa tunaingia kwenye mtafaruku Tanzania, sasa dhana yao haipo na itaendelea kuwa hivyo. Na nadhani mmewasikia wale wagombea walipotoa kauli zao wakisema watakubali matokeo kwa sababu ni sanduku la kura linaamua na si utashi wa mtu,” alisisitiza.
Akipongeza pia Polisi, Kailima alisema “uchaguzi wa mwaka 2005 na 2010 yalishuhudiwa mabomu yakipigwa. Naipongeza sana Polisi, inatoa elimu kwanza kabla ya kumwadhibu mtu…sijasikia mahali ambako polisi wanakimbizana na watu.”
HABARI LEO
2 comments:
Lubuva asante ila inakuweaje unakubali kukaa kwenye kipaza sauti kusoma matokeo unayofahamu wazi kuna utata ndani yake ??
Wacha ushambenga wako matokeo gani yenye utata???
Post a Comment