ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, October 17, 2015

SERIKALI KULIPA MADENI YA WATUMISHI WA SERIKALI ZA MITAA.

Kaimu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais-Utumishi Bw. HAB Mkwizu (wa pili kutoka kulia) akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu namna Serikali  inavyoshughulikia madai ya watumishi walio katika Serikali za Mitaa wasio walimu. 

Na Magreth   Kinabo-maelezo
SERIKALI  imetenga  kiasi cha fedha cha  Sh. bilioni tano ( 5.93) ikiwa ni madeni ya mishahara ya  Watumishi wa Mamlaka za Serikali za  Mitaa(TALGWU) na  Sh. bilioni nne(4) kwa ajili ya kulipa madeni  ya yasiyohusu mishahara, fedha ambazo zitalipwa Oktoba mwaka huu.

Kauli hiyo ya Serikali imetolewa leo na  Kaimu  Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, HAB  Mkwizu  wakati akizungumza  na waandishi wa habari kuhusu  madai na madeni  ya watumishi hao  kwenye  ukumbi  wa  Idara ya Habari (MAELEZO) jijini Dares Salaam.

Aidha Serikali imefafanua kwamba madai ya watumishi hao yanayohusu mishahara mpaka kufikia Oktoba Mosi,mwaka huu,ambao si walimu   malimbikizo yake yalikuwa takribani Sh. bilioni 6.147,  na idadi ya watumishi wanaodai ni 5,695  katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2015/2016.

Hivyo hadi kufikia Oktoba , mwaka huu Serikali ilikuwa  imewalipa watumishi 1,551 wakiwemo wa Serikali za Mitaa jumla ya Sh. bilioni 1.6 na malipo hayo  hayajumuishi yale yaliyofanyika kwa walimu.
“Aidha Watumishi  wa Serikali  za Mitaa wapatao  455 wenye madai  ya Sh. milioni 593.2 watalipwa mwezi  Oktoba, mwaka huu. Madai yaliyosalia yataendelea  kulipwa  kila mwezi kadri uhakiki unavyokamilika,” alisema Kaimu Katibu Mkuu huyo.  
Alisema  kwa upande wa madai  yasiyohusu mishahara , ambayo yamekuwa yakilipwa  kupitia fungu la Matumizi  Mengineyo, madai ya kiasi  Sh. bilioni 18 yalikwishahakikiwa na yanasubiri kulipwa.  

Mkwizu aliongeza kwamba  madeni hayo  ya watumishi hao ni yale  yaliyolimbikizwa hadi mwaka  2012/2013.
“ Serikali imepanga kulipa deni hilo lote katika kipindi cha kuanzia Oktoba 2013 hadi Januari,2016,kwa kuanzia Oktoba 2015 Serikali imetenga kiasi cha Sh. bilioni 4 na kiasi cha sh. bilioni 14 kitakachosalia kitalipwa kwa awamu ndani ya kipindi kilichopangwa,” alisisitiza.

Aidha Kaimu Katibu Mkuu huyo alisema wakati wa kutekeleza malipo hayo, waajiri wameaagizwa kuwaandikia barua watumishi ambao madai yao yamekataliwa au kupunguzwa ili kuwafahamisha sababu za kutakataliwa  kwake na hivyo kuwawezesha kuwa na taarifa sahihi kuhusu madai  yao na kuondoa uwezekano wa kudai mara nyingine.

 Akizungumzia kuhusu suala la uhakiki wa madeni alisema  kwa upande wa madai yasiyohusu mishahara yalikuwa ni sh.  bilioni 18,lakini baada ya kuhakikiwa yakafikia Sh. bilioni 14.

 Alizitaja sababu mbalimbali za kukataliwa  baadhi ya madeni hayo  kuwa ni  zipo tofauti na zinatokana na kutofuata  sheria, kanuni na taratibu.

No comments: