Advertisements

Tuesday, October 13, 2015

Serikali ya ACT-Wazalendo kuanzisha wakala wa maji vijijini

Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe 

Mbulu. Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema Rais wa awamu ya tano atakayetokana na chama hicho ataanzisha mfuko wa wakala wa maji vijijini ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya majisafi na salama.

Amesema fedha zitakazotumika kuendesha mfuko huo zitakuwa ni asilimia moja ya asilimia 18 ya fedha za kodi ya ongezeko la thamani (VAT) inayolipwa serikalini kwa sasa.

Zitto ambaye anagombea ubunge Jimbo la Kigoma Mjini ametoa kauli hiyo leo katika mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani Mbulu mkoani Manyara.

Amesema maji safi na salama imekuwa ni kero ya muda mrefu kwa Watanzania wa maeneo tofauti na kwamba majibu ya kero hizo yapo katika utekelezaji wa Ilani ya chama Chama cha ACT-Wazalendo.

“Mwaka 2012 nilitoa hoja bungeni kuhusu ushuru wa mafuta ya taa na tukafanikiwa kuongeza pato katika mfuko wa umeme vijijini kutoka Sh 45bilioni mpaka Sh250bilioni, leo maeneo mengi ya vijijini wananufaika na huduma ya umeme huo. ACT Wazalendo tutatumia njia hiyo hiyo kuhakikisha maji salama yanapatikana,”amesema Zitto

Amesema jambo hilo linawezekana kama Serikali itakuwa na nia thabiti ya kuhakikisha Watanzania wanapata maji safi na salama kwa kutenga asilimia moja ya VAT, kwa ajili ya shughuli hiyo.

“Chama hiki ndiyo kimetoa jawabu la kukabiliana na kero ya maji nchini hasa wakati huu ambao nusu ya Watanzania hawana majisafi na salama,” amesema.

Akizungumzia Maendeleo ya mji wa Mbulu, Zitto amesema serikali imeusahau mji huo licha ya kuwa miongoni mwa miji ya kwanza kuanzishwa katika eneo la Afrika Mashariki.
MWANANCHI

1 comment:

Anonymous said...

CCM B hawa