Advertisements

Sunday, October 11, 2015

SILAHA ZA MAANGAMIZI ZISIISHIE MIKONONI MWA MAKUNDI YA KIHALIFU –TANZANIA

Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzani katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, akichangia majadiliano kuhusu upokonyaji wa silaha na usalama wa kimataifa mwishoni mwa wiki, ambapo ametoa wito wa jumuiya ya kimataifa kushirikiana katika kuhakikisha kuwa silaha za maangamizi haziishii mikononi mwa makundi ya kihalifu.

Tanzania imetoa wito Kwa Jumuiya ya Kimataifa wa kuhakikisha inashirikiana kuhakikisha kwamba silaha za maangamizi zikiwamo za nyukilia haziiangukii mikono ya makundi ya kihalifu.

Wito huo umetelewa mwishoni mwa wiki na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi,wakati wa Mkutano kuhusu masuala ya uponyaji wa silaha na usalama wa kimataifa.

Katika mkutakno huo wazungumzaji wengi walieleza wasiwasi wa kuwapo kwa ushirikiano wa karibu kati ya nchi ambazo zina silaha za nyukilia na zile ambazo hazina, lakini huku zile ambazo zinamiliki silaha hizo zikiendelea kuziboresha na kujilimbikizia.

“Ni jambo la kusikitisha, badala ya kuzipungua silaha hizi na hatimaye kuzitokomeza kabisa, nchi zinazolimiki silaha za nyukilia zinaendelea na kasi ya kuziboresha , kuzifufua na kujilimbikiza”. Akasema Balozi Manongi.

Akabainisha kuwa mbaya Zaidi hata zile nchi ambazo hazina silaha hizo nazo sasa zinatafuta kila maarifa ya kuwa nazo. Jambao ambalo amesema ni tishio kwa usalama wa mwanadamu.

Amesisitiza kuwa ingawa ni miongo saba imekwisha kupita lakini madhara ya matukio ya Hiroshima na Nagasaki bado yanaendelea na yapo hai miongoni mwetu.

Balozi Manongi akaongeza kuwa ni muhimu basi utokomezaji wa silaha za nyukilia na teknolojia inayoambatana nazo likaendelea kupewa kipaumbele pamoja na kuwa na mikataba ya kisheria itakayosimamia jambo hilo.

Akasema kutoka na ongezeko la ulimbikizaji wa silaha za nyukilia, Jumuia ya kimataifa inawajibu wa kushirikiana kuhakikisha kwamba silaha hizo na nyingine za maangamizi haziangukii mikononi mwa makundi ya kigaidi na kihalifu.

Pamoja na ukweli kwamba silaha za nyukili na zingine za maangamizi bado ni tishio kubwa kwa uhai wa mwanadamu. Balozi Manongi akasema kwa nchi zinazoendelea tatizo la usaambaji na matumizi holela ya silaha ndogo na nyepesi zinaendelea kuwa janga kubwa kwa ustawi na maendeleo ya bara hili na kwingineko.

Akimnukuu Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan kwamba madhara yatokanayo na matumizi holela ya silaha ndogo na nyepesi yameendelea kuwa makubwa sana na madhara yake ni makubwa pengine kuzidi mabomu ya atomic yaliyoiangamizia Hiroshima na Nagasaki .

Akizungumzia zidi kuhusu matumizi holela ya silaha ndogo na nyepesi, Mwakilishi huyo wa Tanzania anasema mirindimo ya risasi na hata matumizi ya silaha kali zikiwamo za maangamizi, haiwezi au haitamhakikishia mwananchi maisha yenye hadhi, utu, ustawi na maendeleo.

Akasema kuna uhusiano mkubwa baina ya Amani, usalama na utekelezaji wa Malengo ya maendeleo endelevu y (Agenda 2030) malengo yanayojikita katika kumaliza umaskini pasipo kumwacha yoyote nyuma pamoja na kuilinda sayari dunia.

Akasema itakuwa vigumu kuyatekeleza malengo mapya ya maendeleo kama kiwango cha gharama za kujilimbikiza silaha kitaendelea ambapo inakadiriwa kuwa mataifa hasa yale makubwa yanatumia Zaidi ya dola za kimarekani trillion 1.7 kwa mwaka kwa matumizi ya silaha.

Akasema matumizi ya kiasi hicho cha fedha kujilimbikizia silaha katika maghara mbalimbali duniani huku mamilioni ya watu wakiendelea kuishi katika umaskini uliopindukia, na maelfu ya watoto wakiathirika kwa utapia mlo na wengine wakipoteza maisha kwa kukosa chakula na huduma nyingine za msingi ni jambo lisilo kubalika.


No comments: