Advertisements

Tuesday, October 6, 2015

UVCCM: TULITARAJIA UAMUZI WA KINGUNGE

Aliyekuwa Kamanda Mkuu wa UVCCM, Kingunge Ngombale-Mwiru.

Jumuiya ya Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), imesema haijashtushwa na uamuzi wa aliyekuwa Kamanda Mkuu wa jumuiya hiyo, Kingunge Ngombale-Mwiru, kuachana na CCM kwa kuwa tangu awali haukuridhishwa na mwenendo wake kisiasa.


UJumuiya hiyo imesema na ndiyo maana Kingunge alivuliwa wadhifa huo tangu Agosti 15, mwaka huu.

Hata hivyo, UVCCM imesema itaendelea kuwatumia viongozi wakongwe wa kisiasa waliopo wenye busara, heshima na wanaokiheshimu Chama na kuiheshimu demokrasia.

Kauli hiyo ilitolewa na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.

Shaka alisema chama hicho kitaendelea kuhimili, kitabaki imara na kukabiliana na misukosuko pamoja na dhoruba za kisiasa na kuwa hakuna kiongozi hata mmoja ambaye ni muhimu kuliko mwingine.

Alisema kitendo cha Kingunge kusema kuwa kanuni, taratibu na katiba ya chama vilikiukwa katika kumpata na kumteua mgombea urais, hazina mashiko wala ukweli wowote.

“Tunaunga mkono na kukubaliana na maamuzi vya vikao vya Chama katika kumpata na kumteua mgombea urais CCM, siyo mtu wala umbo na uso, maamuzi yatokanayo na vikao vya kikatiba, akaona havina maana wala uzito kuliko fikra na utashi binafsi, huo ni mtazamo wake,” alisema Shaka.

Kadhalika, alisema Kingunge hakuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Nec wala Mkutano Mkuu wa chama hicho.

“Tunamuuliza kuwa anaposema taratibu zilikiukwa, je, ni sahihi demokrasia iliyotumika katika kumpata mgombea urais wa chama ambacho yeye anamuunga mkono? Tulifahamu tangu awali kuwa ataondoka CCM, baada ya vijana kukataa kuyafuata wanayoyataka wao,” alisema Shaka.

Alisema kauli ya Kingunge kwamba kuna vijana wanaotumika kuwatukana baadhi ya viongozi na wazee, siyo za kweli kwa kuwa vijana wa sasa wanajitambua.

Aidha, Shaka alisema wanalaani kitendo cha wanachama wa vyama vya upinzani kushambulia kwa mawe misafara ya wanachama wa CCM katika maeneo ya Kuyuni, Mtuhaliwa na Chokocho katika Mkoa wa Kusini Pemba, wakitokea katika mikutano ya kampeni.

“Septemba 15 na 18, mwaka huu, wanachama wa CCM walishambuliwa na baadhi ya watu walijeruhiwa na magari kuvunjwa vioo. Tunaamini kuwa siasa za vyama zingeendeshwa kistaarabu kipindi hiki na si kama tunavyoshuhudia,” alisema Shaka.

KAULI YA JAJI WARIOBA
Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, akizungumza na Nipashe jana kuhusiana na hatua ya Kingunge kuihama CCM, alisema kuondoka kwake hakuna madhara yoyote kwa kuwa bado wapo viongozi kama yeye ambao walikuwa mawaziri na walioshika nyadhifa mbalimbali za kisiasa nchini.

Alisema CCM hivi sasa inapitia kama yaliyotokea wakati Tanzania ilipoingia katika mfumo wa vyama vingi.
Jaji Warioba alifafanua kwamba kulikuwa na makundi ambayo Chama kilijitahidi kuyapinga na kuyavunja kwani CCM inahitaji misingi ya umoja.

“Ninashangaa kwa nini amehama kwa kuwa tumekuwa naye kwa muda mrefu kwa zaidi ya miaka 60 kama alivyosema, tangu tukipigania uhuru tulikuwa pamoja, nitajivunia kwa kuwa ni kiongozi mwenye ushawishi mkubwa na aliyeacha historia,” alisema Jaji Warioba.
SOURCE: NIPASHE

No comments: