Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza juzi jioni, Wasira alisema matokeo ya ubunge yalichakachuliwa kutokana na uhesabuji kura kutofuata utaratibu.
Wasira alisema kutokana na hilo, msimamo wake ni kutoyatambua matokeo hayo yaliyomshangaza na kumwangusha katika mbio hizo za kulitetea jimbo hilo.
Alisema kura katika uchaguzi huo ziliibwa na kilichotangazwa hakitokani na uamuzi wa wapigakura wa jimbo hilo.
Wasira alitolea mfano wa kituo kimoja cha kupigia kura, akisema kura 1,000 ziliongezwa kwa lengo la kumsaidia mpinzani wake.
Alifafanua kuwa kituo hicho cha kupigia kura kilionyesha kilikuwa na wapigakura waliojiandikisha 367, waliopiga kura 276, kura halali zilikuwa 271.
Lakini alisema matokeo katika kituo hicho yalionyesha kuwa chama cha ACT- Wazalendo kilipata kura moja, CCM kura 120 na Chadema kura 749, na Msimamizi wa Uchaguzi akatangaza waliojiandikisha walikuwa 1,367.
Alisema hatasaini matokeo hayo kwa sababu ni batili na hawezi kuafikiana nayo wala kuyatambua huku akisisitiza uchaguzi huo haukufanyika kwa haki. Hata hivyo, Wasira alisema Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo, Msoffe hakutilia maanani barua ya malalamiko aliyoandika kupitia kwa Mwanasheria wake ili kusitishwa utangazaji wa matokeo hayo. Hata hivyo, alikanusha tuhuma za kukimbilia jijini Mwanza kwa kile kilichodaiwa ni kukwepa aibu ya kushindwa, bali alikwenda huko kwa lengo la kupata ushauri wa nini cha kufanya katika kipindi hiki.
CHANZO: NIPASHE
1 comment:
Move on man, u have been there for a long time, change was required, people of Bunda have spoken, u should respect their decision.
Post a Comment