Sunday, October 25, 2015

Zoezi la upigaji kura laenda kwa utulivu Dar

Hatimaye zoezi la upigaji kura nchi nzima limeanza leo huku kukiwa na hali ya utulivu katika vituo vingi.

Hata hivyo, baadhi ya vituo vilionekana kuwa na changamoto kadhaa ikiwamo waandikishaji na wasimamizi wa uchaguzi kukosa viti na meza za kuandikisha.

Tabata Kimanga

Mwananchi lilifika katika kituo cha Kimanga Darajani na kujionea makarani wakiandikia mapajani hali iliyochangia kuchelewa kwa mchakato wa uandikishaji.

Akizungumzia adha hiyo, karani wa eneo la Muungano, Kimanga Darajani, Mwinjuma Abdallah alisema mchakato wa uandikishaji unachukua muda mrefu kutokana na kukosekana kwa meza.

“Ningekuwa na meza ningetumia dakika mbili hadi tatu kuandika namba ya kitambulisho cha kura katika karatasi zote tatu, yaani ya Rais, Diwani na Mbunge, kuzikunja na kuzipiga mhuri, lakini natumia dakika nne hadi sita kwa kuwa naandikia mapajani,” alisema.

Katika kata hiyo kulikuwa na vituo nane ambavyo ni kimoja tu ndicho kilikuwa na meza ya kuandikisha wakati makarani katika vituo vingine hawakuwa na meza.

Kadhalika, mawakala na wasimamizi hawakuwa na viti hali iliyowalazimu kukaa kwa zamu ili kupumzika na kuifanya kazi hiyo kwa ufanisi.

Mjumbe wa shina namba 47, wa CCM, Herbet Shauri alisema uchaguzi wa mwaka huu unaonekana kuwa na utulivu licha ya vijana wengi kujitokeza kupiga kura tofauti na miaka iliyopita.

“Hali ni ya utulivu, watu wamejitokeza kwa wingi, zamani waliokuwa wanapiga kura ni wanawake na wazee lakini leo tumeona vijana wengi wanapiga kura,” alisema.

Kijichi A


Katika kituo cha Kijichi A kilichopo shule ya msingi kijichi, ilionekana misururu mirefu, huku baadhi ya watu waliofika tangu saa 11 asubuhi hasa wanawake na wazee wakionekana kukaa chini. wamekaa chini. Hali ni tulivu polisi wanazunguka kuangalia usalama.

Mikocheni A, TSJ

Hali ya mvurugano imeonekana kwenye kituo cha kupigia kura cha Mikocheni A TSJ baada ya kukosekana utaratibu mzuri wa kuwaongoza wapiga kura.
Mwananchi ilifika kituonI hapo saa moja kasoro na kukuta tayari watu wakiwa wamefika wakisubiri zoezi la kupiga kura kuanza.
Pamoja na kuwahi wananchi hao walionekana kuwa kwenye misongamano wengi wao wakitaka kuhakiki majina.
Mwandishi wa gazeti hilI alishuhudia watu wakiminyana kuelekea mlango uliokuwa na vyumba vya kupiga kura.Askari alionekana kuingilia kati kuthibiti msongamano huo lakini alishindwa na kutoka akisikika anasema kuwa anakwenda kuongeza nguvu.

Bagamoyo

Huko Bagamoyo, mkoa wa Pwani, mamia ya wakazi walionekana wamefurika kwenye vituo vya kupiga kura.

Licha ya vituo vilifunguliwa saa 1.00, wapiga kura walianza kupanga foleni tangu saa 12.00 asubuhi, wakisubiri zoezi hilo lianze.

Mwananchi imefanikiwa kutembelea zaidi ya vituo 10, kutoka kwenye kata za Kisutu, Nyagema na Dunda ambako, imeshuhudia zoezi la upigaji kura likiendelea kwa utulivu.

Baadhi ya wananchi walisema, tofauti na siku nyingine hali ya mji wa Bagamoyo imetulia na kuwa zaidi ya foleni kuwa ndefu hakuna changamoto walizokutana nazo.

Mabasi ya kwenda wilaya za kyela,rungwe, mbarali yasitisha. Kituo cha nanenane kikiwa kitupu. Daladala nazo zasimamisha shughuli.

MWANANCHI

No comments: