ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, November 22, 2015

Bila mipango makini, ‘uendawazimu’ utadumu

NYOTA wa zamani wa Timu ya Taifa ya Uholanzi, Hendrick Johannes Cruijiff, maarufu kama Johan Cruyff, ana nukuu mbili kuhusu soka ambazo bila shaka zinaweza kuwa somo mwanana kwetu na timu yetu ya taifa, Taifa Stars.

 Cruyff anasema katika moja ya nukuu zake kwamba “Soccer is simple, buti it is difficult to play simple,” akimaanisha Soka ni mchezo rahisi lakini ni vigumu sana kuucheza kirahisi. Katika nukuu nyingine mwanasoko huyo mahiri wa miaka ya 1970, na ambaye anasifika kuiongoza timu yake kucheza ile staili maarufu ya kiholanzi ya ‘Total football’ anasema, “Football is a game of mistakes. Whoever makes the fewest mistakes wins.” Kwamba Soka ni mchezo wa makosa, anayefanya makosa machache zaidi ndiyo anashinda. Nitajaribu kuzitafakari kauli hizi kwa kuangazia timu yetu ya taifa. 

Hatuwezi kubishana juu ya ukweli kwamba timu hiyo inahitaji kuungwa mkono kwa nguvu zote kwa sababu ukiondoa ukweli kwamba ushindi wake unatupa burudani kama Watanzania, lakini muhimu zaidi timu hiyo ni utambulisho wa taifa letu, haijalishi tunaipenda au inatukera namna gani, maadamu sisi ni Watanzania, timu ya taifa inatuhusu kwa kiwango hicho. 

Hata Mzee Ali Hassan Mwinyi alipoiita timu yetu hiyo ni sawa na kichwa cha mwendawazimu, hakumaanisha kuipuuza, kama Rais wa nchi wakati huo ilikuwa ni namna ya kuelezea kukerwa kwake na jinsi timu hiyo isivyofanya vizuri. 

Tangu Mzee huyo akerwe na kuumizwa na timu hiyo mpaka kuifananisha na kichwa cha chizi, ambaye kila anayetaka kujifunza kunyoa anakitumia, ni zaidi ya miaka ishirini sasa imepita bado kama taifa wala chama cha soka hatuna mpango mkakati (Strategic Plan) ya kuondokana na wendawazimu huo. 

Tumejifungia kujifaraji na mafanikio tunayopata kama homa ya vipindi, nakumbuka wakati wa Marcio Maximo, tulipocheza na Senegal katika dimba la CCM Kirumba jijini Mwanza na kutoa sare mechi hiyo, tulijipa matumaini, kwamba timu imecheze vyema na ile mechi ilikuwa ‘yetu’, yaani tulipaswa kushinda. 

Majuzi wakati wa mechi ya kwanza na Algeria katika Uwanja wa Taifa, mpaka dakika ya 70, tulikuwa mbele kwa magoli mawili dhidi ya wapinzani wetu, lakini dakika nne, kuanzia dakika ya 71 mpaka ya 75 zilitosha kutunyong’onyesha na kauli ile ile ya ilikuwa mechi yetu, ikajirudia, tukawa tunatamani zile dakika nne zisingekuwepo kwenye mchezo huo. 

Wakati tunabatizwa kuwa kichwa cha mwendawazimu, tungeweza kabisa kuweka mipango ya maana na kuandaa vijana, ambao hata kama wangekuwa wanazaliwa wakati huo, wangekulia katika shule za soka na mipango mahsusi ya kuwaendeleza, leo wangekuwa wanabeba matumaini yetu ya kwenda Urusi mwaka 2018. 

Badala yake tumeendelea na mipango ya zima moto na kutegemea mikakati ya kuunga unga kana kwamba mashindano tunayoshiriki yameshuka ghafla. 

Ni kweli kama anavyosema Cruyff, soka ni mchezo wa makosa, tunaweza kukaa chini wadau wote wa soka na kutafari idadi na aina ya makosa tunayofanya, tukishapata jibu tunaweza kuanzia hapo namna ya kujirekebisha. 

Tunayo makosa mengi tunayofanya, moja wapo ni kutokuwa na mipango ya muda mrefu, ambayo ingetusaidia sisi kutambua uwezo wetu, udhaifu wetu, nini cha kufanya kuondokana nao, kifanyike namna gani, na kwa muda gani na ili kupata matokeo yepi. 

Wenzetu makini wanaoshiriki mbio za kuelekea Urusi 2018, walianza maandalizi zaidi ya miaka kumi iliyopita, mimi sina hakika kama mwaka 2005 hata kama tulikuwa tuna ndoto kuwa kuna fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018,

 kwa muktadha wa maandalizi. Sisi tumechangau kwenda kinyume na kanuni za mafanikio, unaposhindana na mtu ambaye amewekeza katika rasilimali watu kwa maana ya wachezaji na wataalam, anafanya yote yapasayo ushindi katika vifaa na zana zingine za kufundishia soka, hata kama utashinda mechi hiyo, utashinda kwa kubahatisha tu lakini huwezi ukawa ushindi wa kukupeleka kokote, utakuwa ni ushindi wa nasibu tu, ambao hauna tofauti na nguo ya kuazima, kwa kuwa hauwezi kusitili aibu ya kuwa mtupu. Sisi tunaufanya kuwa mchezo rahisi unaoweza kuchezwa kirahisi, mafanikio ya kweli ya soka letu lazima yatokane na mipango na mikakati makini. Hii bahatisha bahatisha haitatufikisha popote.

 Kwa mfano tungekuwa na mpango mkakati wa maana, leo tungekuwa na uhakika baada ya miaka kumi ijayo tutakuwa na akina Samatta, kama kumi hivi na kina Ulimwengu kama ishirini.

 Lakini kwa kuwa ni kichwa cha mwenawazimu tunabaki kuomba dua tu kwamba watokee kina Samatta wengine, bila hata kujiuliza wanatokeaje na kwa mipango ipi. 

Kitu kimoja ambacho tunaweza kujivunia ni kwamba ikiwepo dhamira ya kweli tunaweza. Samatta leo ni mfungaji bora Afrika, hiki ni kielelezo cha wazi kwamba vipaji na vijana wenye uwezo tunao. Lakini hatuna mipango ya kuwaendeleza, bahati haiwezi kuendelea kuwa yetu kila siku, lazima tuwekeze kwa vijana, ili miaka 10 au 20 ijayo tuwe na uhakika wa kuwa na kikosi bora. 

Tunapojivunia mafanikio ya Samatta na Ulimwengu, tujiulize kama TFF na hata taifa kwa maana ya vyombo vinavyohusika na michezo nchini wanaweza kujitokeza na kusema vijana hao ni matunda ya mipango yao? Tusipikuwa makini tutarudi kule kule kwenye riadha, ambako baada ya Filbert Bayi na Suleiman Nyambui, hatuna tena wanariadha mahiri, hawa wamekuwa kama walitokea Tanzania kwa bahati mbaya, kwingine kote duniani vipaji vinaendelezwa, jirani zetu Kenya ni mfano mzuri jinsi wanavyoendeleza kizazi na vipaji vya wanariadha wao. 

Mafanikio katika soka, hayaji isipokuwa kwa mipango makini nay a muda mrefu, inayoambatana na dhamira ya kweli katika kujenga uwezo wa vijana wetu na kuendeleza vipaji vyao. Ukiwatazama, Algeria leo, wamepita katika vipindi vigumu lakini walikuwa wakijipanga na kuinuka upya. 

Wamekuwa na kizazi cha dhahabu kati ya 1980 na 1990 ambacho kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka 1982, kiliishangaza dunia kwa kuwachapa Mabingwa watetezi Ujerumani Magharibi bao 2-1, na isingekuwa mizengwe tu walikuwa waningia raundi ya pili. 

Kuanzia mwaka 1990 mpaka 2007, walikuwa katika kipindi cha giza, wenyewe wanakiita ‘The dark years’. Kikosi chao tunachokiona leo ni matokeo ya mapinduzi waliyofanya baada ya kugundua wako gizani, kuanzia mwaka 2008 mpaka sasa ni kikosi makini. Tumekaa kwenye miaka ya giza kwa muda wa kutosha, hatupaswi kuendelea kutegemea bahati, soka ni uwekezaji na mipango makini, tuelekeze nguvu zetu huko. - See more at: http://www.raiamwema.co.tz/bila-mipango-makini-%E2%80%98uendawazimu%E2%80%99-utadumu#sthash.FeUIIw0s.dpuf

Raia Mwema

No comments: