Dar es Salaam. Wakati Kilimanjaro Stars ya Tanzania Bara ikianza harakati zake za kuwania ubingwa wa Chalenji leo kwa kuikabili Somalia, ndugu zao Zanzibar Heroes wamezama mbele ya Burundi kwa bao 1-0.
Timu hiyo na Zanzibar Heroes hawana budi kufanya vizuri katika mashindano hayo ili kuwafuta machozi Watanzania ambao wana uchungu baada ya Taifa Stars kutolewa kwa kipigo cha aibu cha mabao 7-0 na Algeria wiki iliyopitra katika mashindano ya kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Dunia.
Zanzibar Heroes ilipoteza mchezo wake wa kwanza kwa kufungwa bao 1-0 na Burundi.
Bao la dakika ya 38 la mshambuliaji wa Burundi anayeichezea Azam, Didier Kavumbagu lilitosha kuimaliza Zanzibar Heroes iliyokuwa imesheheni nyota kama vile, Nadir Haroub ‘Canavaro’, Haji Mwinyi, Mudathir Yahaya na Mwadini Ally.
Tanzania iliyochukua ubingwa wa Chalenji mara tatu, ipo Ethiopia ikiwa na matumaini ya kufanya vizuri katika mashindano hayo ambayo bingwa mtetezi ni Kenya.
Kilimanjaro Stars itaikabili timu dhaifu ya Somalia iliyo katika nafasi ya 203 kwenye viwango vya soka vya Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), ingawa inapaswa kuwa makini kwani timu ndogo kama hizo zimekuwa zikizitilia ngumu timu kubwa.
Ushindi kwenye mchezo wa leo utaisaidia Kilimanjaro Stars katika michezo yake ijayo dhidiya wenyeji Ethiopia na Rwanda, Amavubi zilizocheza jana jioni.
Kocha wa Kilimanjaro Stars, Abdallah Kibadeni alisema wamekwenda katika mashindnao hayo si kushiriki, bali kushindana na kuwataka wachezaji wake kupambana kufa na kupona kuhakikisha wanarudi na ubingwa na kuwapa raha watanzania.
“Kipigo tulichopata dhidi ya Algeria kimemsononesha kila mtu, hivyo hatuna budi kupambana katika mashindano ya Chalenji na kuhakikisha tunashinda kila mechi ili tutwae ubingwa na iwe kama zawadi ya kuwafuta machozi Watanzania.
“Najua mashindano ni magumu na tumepangwa na timu ngumu lakini tutakomaa kuhakikisha tunatimiza malengo yetu ya kutwaa ubingwa”alisema Kibadeni.
Mshambuliaji Simon Msuva alisema watajituma kuhakikisha wanatwaa ubingwa wa mashindnao hayo licha ya kwamba yatakuwa na ushindani mkubwa.
“Tuna kikosi kizuri, matokeo yaliyopita dhidi ya Algeria yasiwakatishe tamaa Watanzania, bado mapambano yanaendelea naamini tutafanya vizuri, “alisema Msuva
Mashindano hayo yanashirikisha timu 11, kundi A linazo Kilimanjaro Stars, Ethiopia,Rwanda na Somalia, kundi B linaundwa na Burundi, Kenya,Uganda na Zanzibar, kundi C linazo timu za Djibouti, Sudan, Malawi (mwalikwa) na Sudan Kusini.
Tangu mashindano hayo yaanze, Uganda imechukua ubingwa mara 13, ikifuatia na Kenya mara sita, Ethiopia mara nne, Tanzania Bara, Malawi, Sudan zimetwaa mara tatu kila mmoja , Zambia (ambayo haipo tena Cecafa), mara mbili, Zanzibar na Zimbabwe (pia haipo Cecafa), mara moja kila moja.
No comments:
Post a Comment