Uamuzi wa Rais Dk. John Magufuli, kubana matumizi ya serikali kwa nia ya kuelekeza nguvu katika kushughulikia kero mbalimbali zinazowakabili wananchi, umeokoa wastani wa zaidi ya Sh. bilioni 90 katika siku 20 tangu aingie madarakani.
Dk. Magufuli ambaye aliapishwa Novemba 5, 2015 kufuatia ushindi wake wa asilimia 58.46 katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, ametangaza maamuzi kadhaa ya kubana matumizi ya serikali ili kuimarisha huduma za jamii.
Miongoni mwa maamuzi aliyofanya Rais Magufuli katika siku zake hizo 20 hadi kufikia jana ni pamoja na kusitisha safari holela za nje, kupiga marufuku michango ya aina yoyote kwa wanafunzi kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne na pia kuamuru kutengenezwa mara moja kwa mashine za vipimo vya CT-Scan na MRI katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Kadhalika, wiki iliyopita, Rais Magufuli alitangaza pia kufuta sherehe za Uhuru zilizotarajiwa kufanyika Desemba 9 na kutaka siku hiyo iadhimishwe kwa kufanya usafi nchi nzima ili kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu.
Uchunguzi uliofanywa na Nipashe kupitia vyanzo mbalimbali umebaini kuwa katika kipindi hicho kifupi cha siku 20, maamuzi ya Rais Magufuli yameokoa kiasi hicho kikubwa cha fedha ambacho sasa chaweza kutumika kusaidia shughuli mbalimbali za kijamii ikiwa ni pamoja na kuchimba visima, kujenga zahanati, kununua magari ya kubebea wagonjwa, kununua madawati na pia kuweza kujenga viwanja vya soka walau viwili vyenye hadhi kama Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
1. MICHANGO SHULE YA MSINGI
Wakati akihutubia Bunge kuelezea mapitio ya kazi za wizara yake kwa mwaka wa fedha 2013/2014, aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia, alisema wanafunzi wa darasa la kwanza walioandikishwa mwaka 2014 walikuwa 1,166,497.
Aidha, uchunguzi wa Nipashe hivi karibuni ulibaini kuwa gharama walizokuwa wakilipa wazazi kama michango pindi wakipeleka watoto wao kuandikishwa darasa la kwanza zilikuwa zikitofautiana kati ya shule moja na nyingine, mfano ni katika Shule ya Msingi Mabatini iliyopo Temeke jijini Dar es Salaam iliyokuwa ikitoza michango ya jumla ya Sh.25,000, Shule ya Msingi Kwembe wilaya ya Kinondoni Sh. 67,000 huku shule nyingi za msingi kadhaa za Wilaya ya Mtwara Vijijini zikiwaandikisha darasa la kwanza kwa michango yenye thamani ya jumla ya Sh. 9,000. Hivyo, wastani wa michango hiyo kwa shule walau tatu ni takriban Sh. 35,000.
Ingawa siyo shule zote za msingi zilizoanza uandikishaji darasa la kwanza kipindi hiki, bado hesabu zinaonyesha kuwa amri ya Magufuli ya kupiga marufuku michango ya aina yoyote kwa wanafunzi kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne imesaidia kuwapunguzia wazazi mzigo wa gharama zitokanazo na michango ya uandikishaji darasa la kwanza.
Kwa ujumla, kama kila mzazi nchini angeandikisha mwanawe darasa la kwanza kwa Sh. 35,000, na kama idadi ya wanafunzi hao ni sawa nay a mwaka 2014 ambayo ni 1,166,497, maana yake kiasi cha fedha za michango kwa wanafunzi wote milioni kingekuwa ni takriban Sh. bilioni 40.83. Amri ya Magufuli imeokoa fedha hizi kwani sasa wazazi hawatalazimika kuzitoa ili kaundikisha watoto wao.
2. SHEREHE ZA UHURU
Katika moja ya makala zilizopo kwenye tovuti yake, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika (Chadema), anasema gharama za sherehe za wiki ya maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru, Desemba 2011, zilikuwa ni zaidi ya Sh. bilioni 50.
Gharama hizi zilikuwa kubwa zaidi kutokana na ukweli kuwa sherehe hizi zilikuwa na upekee wa aina yake kwani ilikuwa ni nusu karne baada ya uhuru wa Tanganyika. Hata hivyo, chanzo kimoja kiliiambia Nipashe kuwa gharama za kawaida za sherehe za siku ya uhuru huwa siyo chini ya bilioni 29. Hizi huwa ni pamoja na maandalizi kabambe yanayohusisha gwaride la vikosi vyote vya ulinzi na usalama, ngoma, muziki, halaiki na pia kukaribisha viongozi wa mataifa mbalimbali wa ndani na nje ya nchi. Kadhalika, jioni ya siku ya Uhuru huwa na dhifa maalum ya chakula inayoandaliwa na mkuu wa nchi.
Gharama nyingine za siku hii ya sherehe za Uhuru huwa ni fedha za kulipa posho askari wanaoshiriki kwenye gwaride, watumishi wa umma na watoto wanaoshiriki maonyesho ya halaiki, vinywaji, mafuta ya magari, ndege, vifaru, vipeperushi, mapambo na gharama nyinginezo.
Kwa sababu hiyo, uamuzi wa Rais Magufuli kufuta sherehe za mwaka huu za Uhuru siku ya Desemba 9, 2015 na kutaka siku hiyo isherehekewe kwa kila mmoja kufanya usafi wa mazingira ili kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu umeokoa fedha hizo ambazo sasa zinaweza kuelekezwa katika maeneo mengine ya maendeleo.
3. SAFARI NYINGINE ZA NJE
Katika hotuba yake wakati akilizindua Bunge Novemba 20, 2015, Dk. Magufuli alisema anafuta safari zote holela za nje kwa sababu zimekuwa zikiligharimu taifa mabilioni ya fedha ambayo yangeweza kusaidia shughuli nyingine za maendeleo kama kujenga barabara za lami za urefu wa kilomita 400, kuchimba visima vya maji safi na salama na pia kujenga zahanati au kununua dawa ili kuondoa kero wanayopata wananchi waendapo kwenye hospitali za umma.
Katika kutoa mfano, Rais Magufuli alisema kuwa katika mwaka wa fedha wa 2013/2014 na sehemu ya 2014/2015, taifa lilitumia takriban Sh. bilioni 356. Kwa sababu mwaka mmoja huwa na siku 365, maana yake wastani wa matumizi ya serikali kwa safari za nje kila uchao ni takriban Sh. milioni 975.34. Hata hivyo, hesabu hizi ni kwa makadirio kuwa fedha alizotaja Rais Magufuli zilitumika kwa kipindi cha mwaka mmoja wa kalenda.
Kwa sababu hiyo, katika siku 20 za kuwa madarakani kwa Magufuli, yaani kuanzia Novemba 5, 2015 hadi jana Novemba 25, maana yake kama siyo amri ya Magufuli, kiasi cha fedha kilichopaswa kutumiwa na taifa kwa ajili ya safari za nje za vigogo ni takriban Sh. bilioni 19. 51 (yaani siku 20 x Sh. milioni 975.34). Ukiondoa kiasi kilichohesabiwa katika safari ya Jumuiya ya Madola, yaani takriban Sh. milioni 700, maana yake fedha zinazobaki kwa ajili ya safari nyingine za nje zisizokuwa za Jumuiya ya Madola ni Sh. bilioni 18.81. Wastani wa fedha zote hizo zimeokolewa na kutokana na amri ya Magufuli hadi kufikia jana na sasa zinaweza kufanya kazi nyingine za maendeleo.
4. VIPIMO CT-SCAN MUHIMBILI
Kabla ya kuapishwa kwa Magufuli, vipimo vya CT-Scan katika Hospitali ya Taifa Muhimbili vilikuwa vimesimama kufanya kazi kwa zaidi ya miezi miwili kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni ubovu, na pia kuwapo kwa mgogoro wa malipo baina ya hospitali hiyo na kampuni iliyokuwa zabuni ya kufanya matengenezo.
Baadhi ya taarifa zilieleza kuwa kifaa hicho kiliharibika tangu Agosti 30, 2015, hivyo kwa ujumla hadi kufikia jana (Novemba 25, 2015), tayari zilishatimia siku 85 ziliopita bure bila kifaa hicho kufanya kazi.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma na Huduma za Jamii wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Aminiel Aligaeshi, CT-Scan inapofanya kazi huhudumia watu 25 hadi 40 kwa siku. Gharama wanazolipia wagonjwa huwa ni kati ya Sh. 100,000, Sh. 170,000 au Sh. 250,000, kutegemeana na kundi la malipo la mgonjwa kuwa ni wa ‘private’, ‘general’ au mwenye kadi ya Bima ya Afya.
Kwa sababu hiyo, ikiwa itachukuliwa kwamba kila mgonjwa huwa wa kujilipia binafsi (private) na hivyo kulipa Sh.250,000 ili kupata huduma ya CT-Scan, maana yake gharama zinazokosekana kwa siku kutokana na vifaa hivyo kutofanya kazi yake huwa ni Sh. 10,000,000; yaani 250,000 x 40. Jumla ya gharama hizi hadi kufikia jana ambayo ni siku ya 85 tangu kuharibika kwake ni Sh. milioni 850.
Hata hivyo, gharama hizo sasa zinaelekea kukomeshwa kwani Rais Magufuli ameingilia kati kwa kutimua Bodi ya Hospitali hiyo, kumuengua aliyekuwa akikaimu nafasi ya ukurugenzi na pia kuamuru kutengenzwa vipimo hivyo mara moja. Mafundi wameshaingia kazini na vilitarajiwa kukamilika jana.
5. HAFLA KUPONGEZA WABUNGE
Hii ni tafrija maalum iliyokuwa imeandaliwa na Bungeni mkoani Dodoma kwa nia ya kupongezana kufuatia ushindi walioupata katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, kuapishwa na mwishowe Rais Magufuli kulizindua Bunge lao la 11, Ijumaa ya Novemba 20, 2015.
Kwa kawaida, hafla za namna hii ambazo huwakutanisha wabunge wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kisha Rais kukaribishwa, huwa na mbwembwe za kila namna. Waheshimiwa wabunge hula na kunywa watakavyo huku wakiburudika kwa muziki wa ‘live’ kutoka kwa bendi maarufu za muziki wa dansi nchini.
Ili kufanikisha sherehe hizo, yaelezwa kuwa fedha kiasi cha takriban Sh. milioni 225 kilichangishwa. Hata hivyo, bahati mbaya sana kwa waheshimiwa wapya wa Bunge la 11, Rais Dk. Magufuli hakukubaliana hata kidogo na matumzi ya mamilioni yaliyochangwa. Mwishowe, badala ya kuzimwaga fedha zote hizo kwenye sherehe, akaamuru zitumike kati ya Sh. milioni 10 na Sh. milioni 15 tu, kisha kiasi chote kilichobaki cha Sh. milioni 210, kielekezwe katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ili kitumike kununua vitanda na kuwaondolea wagonjwa adha ya kulala sakafuni.
Kufika Jumatatu, ikiwa ni siku mbili tu baada ya Magufuli kutoa agizo hilo, vitanda 300 vilinunuliwa kwa kutumia fedha hizo, pmoja na ziada ya mashuka 600. Viotu hivyo vyote vimeshafikishwa Muhimbili na wagonjwa wangali wakinufaika na uamuzi huo wa Rais Magufuli.
6. VIPIMO MRI MUHIMBILI
Kama ilivyokuwa kwa CT-Scan, mashine ya kipimo cha MRI pia iliharibika kwa takriban siku 85 hadi kufikia jana. Kwa mujibu wa Eligaeishi, wastani wa watu wanaopata huduma ya kipimo hiki kwa siku huwa ni 10 hadi 15 na gharama huanzia Sh. 160,000 kwa wagonjwa wa kundi la jumla (general), Sh. 350,000 kwa walio na kadi za Bima ya Afya na Sh. 450,000 wanaojilipia binafsi (private).
Ikiwa wahitaji wote wa huduma ya MRI ni wa kundi la private, yaani wanaojilipia Sh. 450,000, na ikiwa vipimo hivyo huhudumia idadi ya juu ya wahitaji ambayo ni watu 15, maana yake serikali ilikuwa ikipoteza takriban Sh. milioni 6.75 kila uchao au Sh.milioni 573. 75 kwa siku zote 85 hadi kufikia jana.
Hata hivyo, mzigo wa gharama zote hizo zinazotokana na ubovu wa kipimo hicho zinaelekea kukomshwa kwani kutokana na amri ya Magufuli, tayari mafundi walishaingia kazini tangu wiki iliyopita na kipimo hicho kinatarajiwa kuanza kazi leo.
7. SAFARI JUMUIYA YA MADOLA
Siku moja tu baada ya kuapishwa Novemba 5, 2015, Rais Dk. Magufuli alitoa maagizo kadhaa yakiwamo ya kuzuia safari holela za nje nchi. Alisema panapokuwa na ulazima, safari yoyote ni lazima iidhinishwe na yeye (Rais Magufuli) au Katibu Mkuu Kiongozi Ikulu, lengo likiwa ni kupunguza matumizi ya serikali ili fedha zinazookolewa zitumike kuboresha huduma za jamii.
Kutokana na agizo lake hilo, Rais Magufuli ameripotiwa kufyeka msafara mzito uliopaswa kuongozwa na yeye mwenyewe na vigogo wengine serikalini takriban 50 kwenda kwenye mkutano wa wakuu wa Jumuiya ya Madola unaofanyika barani Ulaya, katika kisiwa cha Malta.
Ikiwa ni sehemu mojawapo ya kubana matumizi, yaelezwa kuwa ni watu wanne tu ndiyo walioruhusiwa kwenda kwenye mkutano huo kumuwakilisha Rais Magufuli na timu yake yote iliyopaswa kuwa kisiwani humo kwa wiki nzima, ambao ni Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, balozi mwingine mdogo na maafisa wengine wawili wa ofisi za ubalozi huo zilizopo jijini London, Uingereza. Uamuzi huu umeokoa matumizi ya serikali yatokanayo na gharama za tiketi za ndege na posho za vigogo waliopaswa kusafiri kutoka takriban Sh. milioni 700 hadi Sh. milioni 49.9 tu.
BILIONI 90.97/- ZAWEZA KUFANYA NINI?
Kwa ujumla, wastani wa fedha zilizookolewa kutokana na maamuzi mbalimbali ya Rais Magufuli ndani ya siku 20 za kuwapo kwake madarakani, yaani Sh. bilioni 90.97, zaweza kufanya mambo mengi ya maendeleo kwa taifa.
Kwa mfano, akizungumza na Nipashe juzi, Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Elibariki Kingu, alisema wastani wa gharama za kukamilisha ujenzi wa zahanati hadi kukamilika katika jimbo lake ni Sh. milioni 50.
Kwa sababu hiyo, kama fedha hizi zikielekezwa katika kujenga zahanati za kiwango sawa na kile cha Singida Magharibi, maana yake zaweza kukamilishwa zahanati 1,819.
Wakati Uwanja wa Taifa ukikamilishwa mwaka 2009, gharama zake zilitajwa kuwa ni takriban Sh. bilioni 56. Kwa sababu hiyo, ikiwa fedha zilizookolewa na Magufuli katika siku 20 za kuwa madarakani, yaani Sh. bilioni 90.97 zingeelekezwa kujenga viwanja vya namna ya ule wa Taifa na kutumia hesabu za wakati huo, maana yake kungekuwa na uwanja mmoja uliokamilika na mwingine wa pili ungefikia katika hatua muhimu ya kuukamilisha.
Akizungumza na Nipashe, Kingu (Mbunge wa Singida Magharibi) alisema wastani wa bei ya bati moja la migongo myembamba mkoani Singida ni Sh. 15,000. Kadhalika, bei ya mfuko mmoja wa saruji ya ujazo wa Kilogram 50 huuzwa pia kwa Sh. 15,000. Kwa sababu hiyo, kama fedha hizi zilizookolewa na Rais Magufuli katika siku 20 za kuwa kwake madarakani zingeelekezwa kununua vitu hivyo kwa bei kama ya Singida, maana yake ingepatikana mifuko 6,064,667 ya saruji au mabati ya idadi kama hiyo.
Aidha, kwa mujibu wa Kingu, gharama ya kuchimba kisima cha maji safi kwenye jimbo lake huwa ni wastani wa Sh. milioni 15. Hivyo, kama fedha zilizookolewa kutokana na maamuzi ya Rais Magufuli katika siku 20 za kuwa kwake madarakani zitaelekezwa kuchimba visima vya kiwango sawa na vile vya Jimbo la Singioda Magharibi, maana yake vyaweza kupatikana visima 6,065.
CHANZO: NIPASHE
2 comments:
Siku 20 za kazi za magufuli hata kabla ya kupata usaidizi kutoka kwa mawaziri tayari ameshafanya mambo makubwa. Kwa kweli watanzania na hasa wenye kuitakia mema nchi yetu tuna kila hali ya kujivunia utumishi wake. Vile vile anahitaji kuungwa mkono hasa kutoka kwetu sisi wanadiaspora nna imani tukiacha itikadi zetu za kisiasa tunauwezo mkubwa wa kuchangia kitu fulani kwa mueshimiwa raisi katika harakati zake za kuliletea taifa maendeleo. Bila ya kuweka mbele itikadi zetu kwa manufaa ya Taifa tuna kila sababu ya kumuunga mkono magufuli kwa kile anachoendelea kukifanya nyumbani kwa kweli mueshimiwa raisi Maghufuli amemua kujitoa muhanga kuhakikisha Tanzania na watanzania wanapiga hatua stahiki ya maendeleo kulingana na utajiri wa rasili mali zilizonazo. Mueshimiwa raisi ameanza vizuri na tumuombe mwenyezi mungu amjalie afya na uzima ili atuongoze katika vita alioiyanzisha ya kulitoa taifa kutoka katika dimbwi la umasikini na ufisadi wa kila aina.
Atupatie Dual Citizenship. Tutaweza kuchangia kwa 100000% kwa hali na mali.
Post a Comment