Awassa Ethiopia. Waswahili husema, bahati haizuiliwi. Ethiopia imeambulia sare kwa bao la kujifunga la beki wa Kilimanjaro Stars, Salim Mbonde, dakika ya 90, ambalo lilitosha kuivushja timu hiyo kama mshindwa bora namba mbili.
Matokeo hayo yameibeba Ethiopia na kuiondoa Burundi ambayo ilipoteza mchezo dhidi ya Uganda kwa bao 1-0 jana.
Kwa matokeo hayo, wenyeji Ethiopia watakutana na kinara wa Kundi A, Kilimanjaro Stars katika mchezo wa robo fainali, kesho, Jumatatu kwenye Uwanja wa Taifa, Awassa.
Kili Stars iliongoza kundi hilo kwa pointi saba na kufuatiwa na Rwanda yenye pointi sita na Ethiopia, yenye pointi nne, kama Burundi, ambazo zote zitacheza robo fainali ya mashindano ya Chalenji.
Kili Stars haikupoteza mchezo wowote tangu kuanza kwa mashindano hayo mwaka huu baada ya kuanza kwa kuifunga Somalia mabao 4-0, kisha ikaichapa Rwanda mabao 2-1 na jana ilitoka sare na Ethiopia ya bao 1-1 na hivyo kuwa vinara wa kundi A kwa pointi saba.
Sare hiyo ya jana imeibeba kwa kiasi kikubwa Ethiopia na hivyo kutinga robo fainali na kuwafariji maelfu ya mashabiki waliofurika uwanjani kuiunga mkono timu yao.
Ethiopia au Walya Antelopes, imeungana na Sudan kucheza robo fainali kwa faida ya mabao na hivyo moja kwa moja kuifungashia virago Burundi ambayo jana ilikuwa ikiombea Kili Stars iifunge Ethiopia ili wao wafuzu.
Kutokana na matokeo hayo, Kili Stars itaikabili Ethiopia katika mchezo wa robo fainali utakaofanyika kesho, Jumatatu jioni ukitanguliwa na robo fainali ya kwanza kati ya Uganda dhidi ya Malawi ambayo ni timu mwalikwa kwenye mashindano hayo.
Robo fainali nyingine zitachezwa Jumanne kati ya Sudan Kusini dhidi ya ndugu zao, Sudan wakati Rwanda wataikabili Kenya katika mchezo ambao unatazamiwa kuwa mkali na wenye ushindani mkubwa.
Bao hilo la kujifunga la beki Mbonde ambaye amecheza mashindano hayo ya mwaka huu lilipatikana dakika za mwisho za mchezo huo wakati akiokoa krosi iliyopigwa na Mohammed Nasser.
Bao hilo lilitosha kuibeba Ethiopia na kuipeleka robo fainali na kuamsha shangwe kutoka kwa mashabiki wengi wlaiofurika kwenye Uwanja wa Awassa.
Katika mchezo wa jana, Kili Stars ilionyesha soka la taratibu na licha ya kufanya mashambulizi kadhaa langoni mwa Ethiopia, lakini ilishindwa kupata mabao mengi kutokana na kukosa umakini.
Washambuliaji wake, John Bocco,Elius Maguli na Simon Msuva walishindwa kuipatia Kili Stars ushindi licha ya mara kwa mara kuipenya ngome ya Ethiopia, lakini kukosa umakini kulisababisha wakashindwa kufunga mabao mengi.
Kili Stars ndiyo ilikuwa ya kwanza kupata bao lililofungwa na Simon Msuva, dakika ya 51 kabla ya Ethiopia kusawazisha dakika za mwisho kwa bahati ya mtende kwa beki wa Kili Stars, Salum Mbonde aliyejifunga wakati akijaribu kuokoa mpira wa krosi iliyopigwa na Mohammed Nasser.
Katika mchezo huo, kocha Abdallah ‘King’ Kibadeni alifanya mabadiliko kidogo ya kikosi chake kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa mashindano hayo baada ya kuwaanzisha Jonas Mkude na Hassan Kessy wakichukua nafasi za Shomari Kapombe na Deus Kaseke walioanzia benchi.
Katika mchezo wa awali uliokuwa wa kuvutia kutokana na soka la kiwango kikubwa lililoonyeshwa na timu zote mbili, Uganda waliichapa Burundi bao 1-0 lililofungwa na Frank Kalanda, dakika ya 70 na hivyo moja kwa kuongoza kundi B kwa kufikisha pointi sita.
Uganda iliyokuwa ikishika nafasi ya tatu kabla ya mchezo huo wa jana, wengi waliitabiria kuwa itatinga robo fainali kama mshindwa bora, lakini mambo yakawa tofauti baada ya kuinyuka Burundi iliyokuwa na wachezaji mahiri kama Amissi Tambwe wa Yanga, Didier Kavumbagu wa Azam na beki wa Gor Mahia ya Kenya, Karim Nizigiyimama na hivyo kuwafanya Warundi hao kufunga virago na kurudi kwao mapema.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment