ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, November 29, 2015

Moto wa Magufuli wachoma zaidi TRA

Moto wa serikali ya awamu ya tano katika kukomesha upotevu wa kodi kwenye Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) umeendelea kushika kasi baada ya vigogo wengine watatu kusimamishwa kazi jana kuhusiana na kashfa ya upotevu wa makontena 349 yaliyoligharimu taifa zaidi ya Sh. bilioni 80.

Kwa mujibu wa habari zilizoifikia Nipashe kutoka kituo kikuu cha Polisi cha Mkoa wa Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TRA, Bade alikamatwa ili kuzuia uwezekano wa kuvuruga upelelezi wa sakata la upotevu wa kontena 349 zilizoinyima serikali kodi ya Shilingi bilioni 80.

Bade pamoja na Kamishna wa Forodha wa TRA Tiagi Masamaki, waliamriwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuhojiwa kufuatia upotevu wa shehena hiyo, unaodaiwa kufanywa kwa muda mrefu na kuikosesha serikali mapato.

Chanzo kilieleza kuwa maofisa hao wako rumande kwa maagizo yaliyotolewa na Waziri Mkuu , juzi wakati alipofanya ziara ya kushtukiza bandarini Dar es Salaam. Kilisema maofisa wengine kadhaa walikamatwa wakiwamo wa TRA na TPA.

Waziri Mkuu aliagiza wakuu wa vitengo vya Huduma kwa Wateja cha TPA Habib Mponezya, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Haruni Mpande, Bandari Kavu, Eliaichi Mrema na Hamis Omari, wakamatwe.

Wahusika hao wanaendelea kushikiliwa na polisi huku uchunguzi wa akaunti zao pamoja na mali wanazomiliki ukifanywa. ôTunachunguza ili kulinganisha vipato vyao. Kadhalika pasi zao za kusafiria zimezuiliwa ... kilidokeza.

Jitihada za kupata taarifa kutoka kwa Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Sulemain Kova, ili kuzitolea ufafanuzi zilikwama baada ya kamanda huyo kugoma kuzungumzia taarifa hizo.

Taarifa iliyotolewa jana na serikali, ilieleza kuwa viongozi wengine wa juu wa TRA waliosimamishwa kazi jana ni Anangisye Mtafya, Nsajigwa Mwandengele na Robert Nyoni.

Vigogo hao wamesimamishwa kazi kwa amri ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ambaye awali, juzi aliamuru wahamishiwe kwenye mikoa mingine nchini kupisha uchunguzi kuhusiana na upotevu wa makontena hayo, huku pia akiwasimamisha vigogo wengine kadhaa.

Uamuzi huo wa jana wa Majaliwa umetolewa ikiwa ni siku moja tu baada ya Rais Dk. John Magufuli kumsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade na kuteuliwa kwa Dk. Philip Mpango kukaimu nafasi hiyo (Kamishna Mkuu).

Akitangaza uamuzi wa kuwasimamisha kazi vigogo hao wa TRA kupitia taarifa yake kwa umma jana, Waziri Mkuu Majaliwa alisema lengo ni kupisha uchunguzi zaidi wa tuhuma zinazowakabili.

Aidha, kama ilivyo kwa wenzao sita waliosimamishwa kazi juzi, (akiwamo Bade), Mtafya, Mwandengele na Nyoni, pia hawaruhusiwi kusafiri kwenda nje ya nchi hadi uchunguzi dhidi yao utakapokamilika.

Mbali na Bade aliyesimamishwa na Rais Magufuli, wengine waliosimamishwa kazi juzi na Waziri Mkuu Majaliwa walikuwa ni Kamishna wa Forodha, Tiagi Masamaki; Mkuu wa Kituo cha Huduma kwa Wateja, Habibu Mponezya; Mkuu wa Kitengo cha Tehama, Haruni Mpande; Mkuu wa Kitengo cha Bandari Kavu, Eliachi Mrema na pia Hamis Ali Omari ambaye hakutajwa ni wa idara gani.

“Kazi ya kuwachunguza ilianza jana ile ile (juzi) na sasa, tumeona hawa watu wanapaswa kuwa nje ya utumishi ili uchunguzi ufanyike kwa uhuru zaidi,” alisema Waziri Mkuu.

Pia Waziri Mkuu amemuagiza Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA, Dk. Mpango, kutekeleza maagizo hayo kwa kuwaandikia barua wahusika.
Juzi mchana, Majaliwa alifanya ziara ya kushtukiza kwenye Bandari ya Dar es Salaam akiwa na nia ya kukagua namna shughuli zinavyoendelea kwenye bandari hiyo, hasa kwenye maeneo ya kupokelea mizigo kutoka nje ya nchi.

Katika kikao kilichofanyika bandarini hapo na kuhudhuriwa na baadhi ya viongozi wa Serikali, Waziri Mkuu alitangaza kuwasimamisha kazi maofisa watano wa TRA kutokana na taarifa za upotevu wa makontena 349.

Waziri Mkuu alisema upotevu huo unasababishwa na mchezo unaofanyika kwa ushirikiano baina ya wafanyabiashara na watumishi wa TRA ambao wanaruhusu makontena kupita bila kulipiwa ushuru na hivyo kuikosesha Serikali mapato yenye thamani ya mabilioni ya fedha.

Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25 na kumpatia ushindi wa asilimia 58.46 dhidi ya wapinzani wake akiwamo Edward Lowassa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chademea), Dk. Magufuli aliahidi kukomesha ufisadi na pia kuinua mapato yatokanayo na makusanyo ya kodi kwa taifa walau mara mbili ya wastani wa kiwango kinachokusanywa sasa cha takriban Sh. bilioni 800 kwa mwezi.

Hadi sasa, tayari Dk. Magufuli ameshatangaza maamuzi kadhaa ya kubana matumizi na kuelekeza nguvu katika kuboresha huduma za jamii, baadhi ya maamuzi makubwa yakiwa ni kupiga marufuku safari holela za nje ya nchi, kuzuia maadhimisho ya Siku ya Ukimwi ambayo huambatana na matumizi ya mamilioni ya fedha, kuamuru kusitishwa kwa maadhimisho ya sherehe za uhuru na pia kuzuia matumizi ya fedha za serikali kwa uchapishaji wa kadi na utoaji wa zawadi za Krismasi na Mwaka Mpya.

WATANGULIZI WA BADE TRA
Kabla Bade hajateuliwa kuiongoza TRA, watangulizi wake katika nafasi hiyo walikuwa ni Harry Kitillya na Melkizedeck Sanare.

Wote waliomtangulia Bade hawakuwahi kukumbana na mkasa wa kusimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi wowote dhidi yao.
Kitilya aliiongoza TRA kuanzia mwaka 2003 hadi mwaka 2014 alipostaafu na nafasi yake kutwaliwa na Bade.

Kielimu, Kitilya alipata Shahada ya Uzamili ya Fedha, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na kisha alikwenda kusomea Shahada ya Uzamivu ya Utawala na Uongozi katika vyuo vya Green State na Harvad nchini Marekani.

Kitilya alifanya kazi kama mhadhiri Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na baadaye kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Fedha na maendeleo ya kodi wa TRA.

Baada ya kutumikia nafasi hiyo kwa muda mfupi aliteuliwa kuwa Naibu Kamishna, kisha Rais wa wakati huo wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, alimteua kushika ukamishna mkuu wa TRA hadi alipostaafu Desemba 14, 2013.

Wakati hupohuo, taarifa zilizopatikana baadaye zinasema polisi imemkamata Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA) Rished Bade jana asubuhi na kuunganishwa na maofisa wengine kadhaa wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), wanaoshikiliwa kwa tuhuma za upotevu wa kontena zaidi ya 300 bandarini Dar es Salaam.

*Imeandikwa na Gwamaka Alipipi, Moshi Lusonzo na Beatrice Shayo
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: