ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, November 12, 2015

Lowassa kutoa tamko zito uchaguzi mkuu Jumamosi.

Aliyekuwa mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, ambaye pia alikuwa akiungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), anatarajiwa kunguruma jijini hapa Jumamosi ambapo atatoa tamko kuhusu uchaguzi mkuu uliopita.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni za ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema, anayetetea tena nafasi hiyo, alisema Lowassa atazungumza na Watanzania Jumamosi kupitia wakazi wa Arusha.

Alisema pamoja na kuja kumnadi yeye katika kinyang’anyiro cha ubunge, Lowassa pia anatarajiwa kutoa tamko kuhusu uchaguzi mkuu uliopita na namna alivyoibiwa kura za urais.

“Angetoa tamko siku ile ya kwanza ya matokeo ya uchaguzi, tungeharibu nchi,” alisema na kuongeza: “Lowassa alishinda kwa asilimia nyingi kuliko kura alizopata Rais Dk. John Magufuli, aliyekuwa mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Alisema nchi imenusurika kutokana na busara za viongozi wa Ukawa kutotoa tamko lolote wakati huo.

“Atakuja Jumamosi, hivyo tusubiri tamko kuhusu hatua gani zinachukuliwa…tuwe na subira,” alisema.

Akizungumzia uchaguzi wa ubunge unaotarajiwa kufanyika Desemba 13, mwaka huu jijini hapa, Lema aliwataka wakazi wa jiji hili kutokata tamaa na matokeo ya uchaguzi mkuu uliopita.

“Hatuna namna yoyote ile kushindwa kuleta maendeleo jimboni hapa iwapo tumepata madiwani 24 kati ya kata 25 zilizopo. “Kama tutashindwa kuleta maendeleo hadi mwaka 2020 huku meya, naibu wake na wenyeviti wa kamati, wote ni wa Chadema, basi mtupige chini na kuwachagua wengine.

Mapema Mbunge Mteule wa Jimbo la Mbeya, Joseph Mbilinyi (Chadema), alisema ingawa wakazi wa Arusha wana hasira kufuatia matokeo ya uchaguzi mkuu uliopita, lakini hasira zao haziwezi kuzidi zile za wakazi wa Mbeya.

Alisema viongozi wao mara zote wametaka kutoa tamko kwa kuzungumza na wananchi, lakini CCM imekuwa ikikaba hadi penati.

Alisema katika jimbo lake, wananchi wamewachagua madiwani 26 wa Chadema na kuwaachia CCM kata tisa, hivyo watapata nafasi nzuri ya kujadili maendeleo katika Baraza la Madiwani na siyo siasa kama ilivyokuwa awali.

Mbunge wa Viti Maalum kutoka Kilimanjaro, Lucy Owenya, alisema Lema alifanya kazi katika mazingira magumu ya halmashauri ambayo ilikuwa ikiongozwa na madiwani wa CCM.

Alisema kwa vile wakazi wa Arusha wamewachagua madiwani wa Chadema 24 kati ya 25, Lema sasa atafanya kazi nzuri ya kuwaletea maendeleo wananchi wake.

Mbunge Mteule wa Simanjiro, James Ole Millya (Chadema), alisema amefanya kitu kimoja kikubwa cha kuondolewa bungeni mpiga kelele bungeni.

Alisema wakifika bungeni, kitu cha kwanza ni kudai Tume Huru ya Uchaguzi, jambo ambalo alisema bila kuwa na tume hiyo CCM itaendelea kuwaibia kura.
CHANZO: NIPASHE

3 comments:

Anonymous said...

Hawa jamaa wa CDM ni watu wa ajabu sana. Richmond na skendo yote uliahidi kutoa mazito ukashindwa. Leo mjanja mwenzio kaenda zake village kula raha wewe unataka kutugiribu akili zetu "ET I UNAMAZITO " subutu yake........nakushauri usichezee tinga tinga. Pumzika na uache siasa. E.L.

Anonymous said...

Hilo tamko limesha pitwa na wakati tayari. Acheni kudanganya wananchi kuwa haki yenu itapatikana kupitia mahakama za kimataifa. Mahakama za kimataiafa siyo katiba ya Tanzania. Lowassa umeshindwa kubali. Acha mwenzako achape kazi. Mnajua wazi kabisa kuwa hakuna chochote mtakacho kufanya kutengua haya matokeo. Kama hamuitambui serikali ya Magufuli bungeni mneanda kufanya nini? kuchukua posho na kurudi nyumbani? CCM kama walikuwa na uwezo wa kuiba wangeiba sana kusudi washinde kwa mbali sana.Siasa ni sayansi na hesabu. Mlikuwa mna hesabu mafuriko badala ya kura. Mlikuwa na washabiki na siyo wapiga kura.Ningependa CCM itoke siku moja, lakini kwa siasa zenu hizi za ulaghai ni kama mnaua upinzani.Tafuteni watu makini wa kukisuka chama upya, mkiwategemea Lowassa, Sumaye na kingunge kuleta maendeleo kwa kasi ya ajabu, imekula kwenu. Achane utapeli wa kisiasa.

Anonymous said...

Mzee Lowassa, tafadhali GROW-UP..or AGE-UP. Kweli unataka kujifedhehesha tena? Sasa geni lipi utalizungumza kwa Watanzania who have written you off? Whatever comes from your mouth at this juncture onwards, doesn't matter and is of no consequences. Tumekuzika kifikra, ukitaka usipotaka..Watanzania tunasonga mbele, wewe endelea na hiyo 'presidential obsession' yako, lakini usisahau kucheki Ng'ombe zako pale Monduli, labda wanahitaji veterinary services.