Kadhalika, inaelezwa kuwa Dk. Magufuli aliyeahidi kuleta mabadiliko ya kweli wakati akiomba kura kwa Watanzania kabla ya kuibuka na ushindi wa asilimia 58.46 dhidi ya wapinzani wake katika uchaguzi mkuu Oktoba 25, sasa yuko mbioni kutangaza baraza lake la mawaziri litakalokuwa na wizara 15, idadi inayofanana kwa kiasi kikubwa na ile ya Baraza la Mawaziri la miaka ya 1980 lililoundwa na Rais wa Awamu ya Kwanza, Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere. Serikali ya awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete, ilimaliza muda wake Novemba 5, 2015 ikiwa na Wizara 30. Kadhalika, alipoingia kwa mara ya kwanza mwaka 2005, Rais Kikwete alikuwa na serikali kubwa yenye mawaziri na naibu wao zaidi ya 60.
Kufikia leo, Rais Magufuli aliyeapishwa Novemba 5, mwaka 2015, tayari ameshamteua Mbunge wa Ruangwa, Kassim Majaliwa, kuwa Waziri Mkuu wa serikali yake ya awamu ya tano na Ijumaa iliyopita alizindua rasmi Bunge la 11.
Chanzo kimoja cha uhakika kimeiambia Nipashe jana kuwa hivi sasa, tayari Rais Magufuli kwa kushirikiana na wasaidizi wake, ameshakamilisha sehemu kubwa ya mchakato wa kuunda baraza lake la mawaziri na kwamba, kinachosubiriwa sasa ni kulitangaza wakati wowote kuanzia sasa.
Chanzo hicho kiliambia Nipashe kuwa Dk. Magufuli ambaye amejichimbia mjini Dodoma tangu mwishoni mwa wiki iliyopita, anatarajiwa kutangaza baraza lake dogo la mawaziri wakati wowote kuanzia leo.
“Halitakuwa sawa na hili alilomaliza nalo Rais Kikwete… na wala halitakuwa na watu wengi kama lile aliloingia nalo kwa mara ya kwanza Rais Kikwete mwaka 2005. Ni baraza dogo tu na wizara kadhaa hazitakuwapo,” chanzo kiliiambia Nipashe.
Kwa mujibu wa ibara ya 55 (1) ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mawaziri wanakuwa wajumbe wa Baraza la Mawaziri na pia kwa mujibu wa ibara ya 54, mawaziri huteuliwa na rais baada ya kushauriana na Waziri Mkuu.
“Kuna mambo madogo bado hayajakamilika… baada ya hapo Mheshimiwa Rais atalitangaza Baraza la Mawaziri siku yoyote kuanzia leo. Kimsingi mkakati wake ni kuwa na baraza dogo lenye wizara 15,” kilieleza chanzo hicho.
Aidha, ilielezwa zaidi kuwa sura kadhaa katika baraza hilo dogo zitakuwa mpya na kwamba, mawaziri waliokuwamo katika serikali ya awamu ya nne wana nafasi ndogo ya kuteuliwa katika baraza hilo.
“Kwa kiasi fulani Baraza hili jipya linafanana na lile la Serikali ya Mwalimu Nyerere miaka ya 1980… lina wizara chache sana, zenye lengo la kubana matumizi ya serikali lakini likiwa na uhakika wa kuchapa kazi usiku na mchana ili kutimiza lengo la Rais Magufuli katika kuwaletea maisha bora Watanzania,” chanzo kiliongeza.
BARAZA LA MAWAZIRI LA NYERERE
Uchunguzi wa Nipashe kupitia vyanzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na maandiko mbalimbali, umebaini kuwa iwapo Magufuli ataunda Baraza lake kwa kuangalia muundo wa Mwalimu Nyerere miaka ya 1980, maana yake baadhi ya wizara maarufu hazitakuwapo tena kwani zitakuwa miongoni mwa zile 15 zitakazofutwa na majukumu yake kuhamishiwa katika wizara nyingine za idadi kama hiyo zitakazosalimika.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa miaka ya 1980, Mwalimu Nyerere alikuwa na serikali yenye wizara 15; ambazo ni Wizara ya Elimu; Wizara ya Mipango; Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa; Wizara ya Mambo ya Ndani; Wizara ya Ujenzi; Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi na Wizara ya Kazi na Ustawi wa Jamii.
WQizara nyingine wakati huo ni Wizara ya Habari na Utamaduni; Wizara ya Afya; Wizara ya Nishati, Madini na Maji; Wizara ya Sheria; Wizara ya Viwanda na Biashara; Wizara ya Kilimo na Wizara ya Fedha.
KASI YA MAGUFULI
Wakati Watanzania wakiendelea kusubiri kwa hamu kusikia baraza la mawaziri la Rais Magufuli, inaelezwa kuwa baadhi ya wabunge kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) wako njiapanda kuhusiana na majina ya wateule watakaokuwamo katika kuunda serikali.
Inaelezwa kuwa, kama ilivyokuwa katika uteuzi wa jina la Waziri Mkuu, hivi sasa kuna usiri mkubwa pia kuhusiana na majina ya wateule wa Rais Magufuli kwa nafasi hizo za uwaziri.
“Tofauti na ilivyokuwa katika mika michache ya hivi karibuni, uteuzi huu wa mawaziri umebaki kuwa wa siri sana na hadi sasa hakuna majina ya uhakika ya watu wanaotazamiwa kuwamo kwenye Baraza la Rais Magufuli, “ mmoja wa wabunge aliiambia Nipashe jana.
Ilielezwa zaidi kuwa mbali na kuwapo kwa usiri mkubwa, pia staili ya utendaji kazi aliyoanza nayo Rais Magufuli imekuwa ikiwatisha baadhi ya wabunge wa CCM waliokuwa na matumaini ya kuteuliwa kuwa mawaziri.
“Misimamo ya Rais Magufuli haitoi matumaini ya ulaji kwa wateule wa nafasi hizo… wengine wameshaanza kuingiwa hofu kwamba hata wakiteuliwa, hakuna maslahi makubwa binafsi watakayoyapata zaidi ya kutakiwa wajiandae kutumikia wananchi kwa moyo mmoja na tena kwa kujituma kwelikweli, chini ya Magufuli uwaziri siyo kazi rahisi ya kuikimbilia,” mbunge mwingine aliongeza.
Katika hotuba yake Ijumaa wakati akizindua Bunge, Rais Magufuli alianisha mambo kadhaa aliyosema yamekuwa kero kubwa kwa wananchi na hivyo serikali yake itafanya kazi kubwa ya kuyashughulikia, baadhi ya maeneo hayo yakiwa ni ya kuboresha elimu ambayo itatolewa bure hadi kidato cha nne, kuinua mapato na pia kupambana na kukomesha vitendo vya rushwa na ufisadi.
Kadhalika, hivi karibuni Rais Magufuli ametangaza hatua kadhaa za serikali yake kubana matumizi na badala yake kuelekeza fedha katika shughuli za maendeleo; baadhi ya hatua hizo zikiwa ni kupiga marufuku safari holela za viongozi kwenda nje ya nchi, kufuta sherehe siku ya uhuru na badala yake kuamuru siku hiyo iwe ya kufanya usafi ili kukabiliana na kipindupindu na pia aliamuru zaidi ya Sh. milioni 200 zilizochangwa kwa ajili ya wabunge kupongezana baada ya kuapishwa wiki iliyopita zielekezwe katika Hospitali ya Muhimbili ambako zilisaidia kununuliwa kwa vitanda vya wagonjwa 300.
“Tusubiri tu kusikia baraza lake la mawaziri limewajumuisha kina nani. Lakini ukweli unabaki palepale kwamba uwaziri siyo kazi lelemama kwa serikali hii. Maana Rais (Magufuli) kaweka wazi kuwa mtu (Waziri) yeyote akiboronga, anamfuta kazi mara moja… kinachotakiwa ni kazi tu, hakuna kwenda Ulaya ovyo, wala hakuna tafrija na makongamano yenye nia ya kuhalalisha ulaji kwa vigogo,” chanzo kiliongeza.
SOURCE: NIPASHE
2 comments:
Safi sana baba magufuli,hapa kazi tu,
Mageuzi from CCM!
Post a Comment