Hatimaye
mahakama kuu kanda ya Mwanza imetoa hukumu ya kuondoa zuio la kamanda wa polisi
mkoa wa Mwanza la kuinyima familia ya aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha
demokrasia na maendeleo (Chadema ) kibali cha kuuaga mwili wa marehemu Alphonce
Mawazo katika jiji la Mwanza.
Hukumu
ya kesi hiyo iliyovuta umati mkubwa wa wakazi wa jiji la Mwanza na mikoa jirani
ya kanda ya ziwa, imetolewa leo mchana na jaji Lameck Mlacha, baada ya familia
ya marehemu kupitia kwa baba yake mdogo mchungaji Charles Lugiko kufungua kesi
ya madai dhidi ya kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza na mwanasheria mkuu wa
serikali ya kupinga marufuku ya jeshi la polisi mkoani humo kuaga mwili wa
Alphonce Mawazo kwa madai kwamba jijini Mwanza kuna mlipuko wa ugonjwa wa
kipindupindu na taarifa zao za kiitelejensia zilibaini kwamba kungetokea
uvunjifu wa amani.
Akisoma
hukumu hiyo iliyochukua muda wa saa moja na dakika 33, Mhe. Jaji Lameck Mlacha
amesema kuwa baada ya kupitia maombi ya mapitio ya Charles Lugiko dhidi ya
kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza chini ya hati ya dharura, ameona kuna utofauti
mkubwa katika zuio hilo na kusema kuwa marehemu ana haki zote za kuagwa na
ndugu, jamaa, marafiki na wafuasi wa chama chake na pia anayo haki ya kufanyiwa
taratibu za ibada, huku akiongeza kwamba mtu asiangaliwe kwa historia yake ya
nyuma bali aangaliwe sasa.
Amesema
kama kamanda wa polisi alikuwa na taarifa za kiitelenjesia hakuwa na sababu ya
kuweka katazo, bali alitakiwa kuwaita ndugu na viongozi wa Chadema na
kuzungumza nao kwa ajili ya kujitetea na wala si kuwanyima haki yao ya
kikatiba, kwani haki ya kisheria ilikuwa ni kuwaita wote.
Baada ya
kutoa hukumu hiyo, Mh. Jaji Lameck alitoa maelekezo ya kuzingatiwa na pande
zote mbili, ambapo amesema mtoa maombi ambaye ni baba mdogo wa marehemu
Alphonce Mawazo, mjibu maombi wa kwanza – kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza na
viongozi wa Chadmea wakutane haraka kwa ajili ya kuweka taratibu za ibada na
kuaga mwili.
Chanzo: Itv Tanzania
CHA
Chanzo: Itv Tanzania
CHA
1 comment:
Tungepata majaji kama watano Kama huyu labda Tanzania ingekuwa nchi yakutenda haki sawa. Kuliko kuwa na police na majaji wanao fanya kazi za ccm badara yakuwatumikia wananchi wao.
Post a Comment