Advertisements

Friday, November 20, 2015

Mali: Miili ya watu 18 imedaiwa kupatikana hotelini


Image copyrightAFPImage captionPolisi wa Mali wameingia katika hoteli hiyo

Maafisa wa serikali ya Mali wamesema sasa hakuna mateka wowote waliosalia katika hoteli ya Radisson Blu mjini Bamako iliyokuwa imeshambulia asubuhi na watu wenye silaha huku miili ya watu 18 ikidaiwa kupatikana ndani ya hoteli hiyo.

Waziri wa usalama wa Mali Salif Traore ameambia kikao cha wanahabari kwamba watu wenye silaha walioshambulia hoteli ya Radisson kwa sasa hawazuilii mateka wowote.
Afisi ya rais wa Mali imeandika kwenye Twitter ikishukuru maafisa wa usalama na mataifa yaliyosaidia kukabiliana na shambulio hoteli hiyo ya kifahari.

Watu watatu wamethibitishwa kufariki na wanajeshi wawili kujeruhiwa.

Ubelgiji imesema afisa mmoja wa serikali yake ni miongoni mwa waliouawa kwenye shambulio hilo.

Geoffrey Dieudonne alikuwa Mali kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa serikali.

Uvamizi huo wa wanamgambo hao ulitekelezwa mapema asubuhi kwenye hoteli hiyo ya kifahari ambayo hupendwa sana na raia wa mataifa ya nje.Image copyrightRadisson Blu HotelImage captionTovuti ya hoteli hiyo inaieleza kama "hoteli ya kifahari"

Baadhi ya ripoti zilisema watu walioshambulia hoteli hiyo huenda wakafika 10.
Moja kwa Moja: Shambulio hotelini Bamako

Ufaransa ambayo imekuwa na wanajeshi Mali tangu 2013 ilituma wanajeshi wake kusaidiana na wanajeshi wa Mali. Aidha, polisi maalum wapatao 50 walitumwa kutoka Paris.

Kundi la wapiganaji wa kijihadi la al-Murabitoun limedai kuhusika kwenye shambulio hilo kupitia ujumbe kwenye akaunti ya Twitter ya kundi hilo, kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, ingawa habari hizo hazijathibitishwa. Kundi la Al-Murabitoun linajumuisha makundi mawili ambayo yalijitenga kutoka kwa tawi moja la al-Qaeda eneo la Afrika Kaskazini.

Agosti, wapiganaji wa Kiislamu waliua watu 13, wakiwemo wafanyakazi watano wa UN, baada ya kushikilia mateka watu katika mji wa Sevare, katikati mwa Mali.

Ubalozi wa Marekani mjini Bamako umeandika kwenye Twitter kwamba unafahamu kuhusu shambulio hilo na kuwashauri wafanyakazi wake pahala salama nao raia wawasiliane na familia.

No comments: