ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, November 19, 2015

Mama amchoma mwanaye kwa maji moto

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mara, ACP Alex Philip
By Veronica Modest, Mwananchi
Musoma. Polisi mkoa wa Mara inamshikilia mwananke mmoja (jina tunalo) mkazi wa Bweri Manispaa ya Musoma kwa kosa la kumchoma mtoto wake mwenye miaka minne, kwa maji ya moto, mikono yote miwili baada ya kumtuhumu kuwa ameiba nyama jikoni.

Mama huyo alikamatwa Novemba 14 saa nne asubuhi katika eneo la Morembe kata ya Bweri mjini Musoma baada ya Polisi kufika nyumbani kwake kumkamata kwa kosa jingine la kumkatakata kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili Kabula Rubeni (32) akimtuhumu kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mume wake.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mara, ACP Alex Philip Kallangi alidai kuwa siku ya tukio hilo la kumchoma moto mtoto huyo, mama yake mzazi alikuwa amepika nyama jikoni na baadaye alikwenda kuchota maji.

Kamanda Kallangi alidai baada ya mama huyo kurudi alimkuta mwanaye anakula nyama ndipo alishikwa na hasira na kuanza kumchapa sehemu mbalimbali za mwili wake na kisha akachukua mikono yote miwili na kumchoma kwa maji ya moto.

Baada ya kufanya kitendo hicho cha kinyama, mama huyo alianza kumtibu mtoto huyo kwa siri hapo nyumbani kwa dawa za kienyeji bila majirani kufahamu kilichokuwa kikiendelea nyumbani kwa mama huyo.

Kamanda Kallangi alieleza kuwa kilichosababisha kufahamika kwa taarifa hizo, ni baada ya Kabula aliyekuwa ameshambuliwa kwa mapanga na mwanamke huyo kwenda polisi kutoa taarifa ya kushambuliwa.

Kallangi alieleza kwamba polisi walipofika nyumbani kwake ndipo walipewa taarifa za mtoto huyo kujeruhiwa kwa kuchomwa moto. Kutokana na tukio hilo polisi hao, kwa kushirikiana na maofisa ustawi wa jamii na kituo cha ushauri cha Jipe Moyo walimchukua mtoto huyo na kumpeleka katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara kwa matibabu na kisha kupelekwa Jipe Moyo anakoishi hadi sasa kwa uangalizi zaidi.

Kallangi alisema mtuhumiwa huyo yupo kituoni na anatarajiwa kufikishwa mahakamani hivi karibuni kujibu mashtaka yanayomkabili.

Ofisa Ustawi wa Jamii Musoma, Vedastus George aliwataka wazazi na walezi kuzuia hasira zao pale watoto wanapowakosea na hata wanapowaadhibu wawe makini ili waziwaumize kama alivyofanyiwa mtoto huyo.

3 comments:

Anonymous said...

Haya ndiyo maisha waTanzania wanayoishi!! Yaani mlo wa nyama katika familia nyingi ni mara moja kwa mwezi na inapopatikana ni wazi nusu kilo pekee ndiyo inayonunuliwa na familia ina watu zaidi ya 5-10, haya ndhiyoo maisha bora kwa kila mTanzania tuliyoneemeka nayo miaka yote hiyo !! Familia nyingi zinaishi maisha ya ili basi tu siku iende wengine wananeemeka kila kuchapo!! Kweli jinsi hii hata mwanafunzi atasoma aelewe kitu kama atakuwa analala nja au kuola chakula ili mradi tumekula haijalishi ni cha kutunza afya!, Bado wengine tunakunyw maji ya ajabu, hizi ndizo neema tulizoahidiwa miaka nenda na majuzi kwenye kampeni zimeendelea?!! Sasa watu wanachoma wanaambulia kuchomwa maji ya moto kisa kipande cha nyama jamani!!! haya ni maajabu. Nyama, Sukari, mchele ni vitu adimu kwa familia nyingi pamoja na kuwasomesha kwa ada ya juu ndicho kinachowafikisha wazazi wengine kutenda wasiyotarajia!! Hebu serikali ibuni mbinu mbadala walau bei za vile muhimu ziwezekanike, sukari inayoagizwa nje inachangia gharama kupaa juu!! Viwanda runavyo?? MAISHA GANI KWA MtANZANIA!! Hapa ndipo tulipofikishwa na utawala wa CCM!! Wale wanaokula milo mitatu watabisha na kutoa maoni yakejeli>!!

Anonymous said...

Kaka Luka story nyingine naomba uwe unazisoma Kabla hujaturushia humu, hii story inasena mama kamchoma mwanae na maji ya Moto na Jina la mama mwandishi kakata kulitaja Ila kasema " TUNALO" sasa mama kafanya kitendo cha kinyama namna hii Halafu mwandishi Ana " protect" Jina la huyo mama kwanini???? Au hii story ni ya kutunga sioni Sababu ya Jina la muhalifu kufichwa !!! Asante Sana...

Anonymous said...

Mdau wa 11:16 PM jaribu kuielewa stori ya hapo juu. Usilete mambo ya siasa hapa. Hili ni suala la ukatili i.e. Child abuse. Ni tatizo kubwa hapa ulimwenguni, nchi nyingi zinakabiliwa na masuala kama haya. Ni wajibu wetu wote kulipiga vita. Sielewi hii CCM inajitokeza wapi katika kitendo ambacho huyu mama amekifanya. Wabongo tusiwe obsessed na politics so much kiasi cha kuwa wenda wazimu. Jee? kama simba atamla mmasai wakati akichunga ng'ombe zake utailaumu serikali ya CCM kwa kutomlinda mmasai?