.png)
Dk. Magufuli aliapishwa rasmi jana katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam. Baadhi ya wasomi na wananchi katika maeneo mbalimbali, wameanza kujadili sura ya baraza hilo jipya litakavyoundwa na utendaji wake wa kazi utakavyokuwa.
Hata hivyo, Rais Dk. Magufuli baada ya kuingia Ikulu jana, mara moja alimteua Mwanasheria Mkuu, George Masaju na kueleza kuwa Novemba 17, mwaka huu ataitisha Bunge na Novemba 19, mwaka huu, atapendekeza jina la Waziri Mkuu na kuliwasilisha bungeni, kwa mujibu wa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.
Rais Magufuli alieleza kuwa hatafanya kazi kwa usahihi bila ya kuwa na Mwanasheria, hivyo ameamua kumteua Mwanasheria kwanza ili aanze kazi kwa kasi. Akizungumza muda mfupi baada ya kuapishwa jana, Rais Dk. Magufuli aliendelea kusisitiza kufanya utendaji wa kazi mzuri kwa serikali yake na kurudia kauli mbiu yake ya `Hapa kazi tu.’
Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma wa Chuo Cha Kumbukumbu ya Mtakatifu Stefano Moshi (SMMUCo), Dk. Gasper Mpehongwa, alisema Rais Dk. Magufuli siyo mbabaishaji katika utendaji wa kazi, lakini kuna uwezekano mkubwa kwa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi kumchagulia mawaziri.
Hata hivyo, Dk. Mpehongwa alisema kutokana na kauli zake anazoendelea kuzitoa, ni dhahiri atachagua mawaziri watakaoendana na uwezo wake wa kiutendaji wa kazi.
“Rais Dk. Magufuli atachagua mawaziri watakaoendana na yeye, hakika watakuwa mawaziri wachapakazi na siyo legelege,” alisema Dk. Mpehongwa. Kuhusu muundo wa baraza la mawaziri, Dk. Mpehongwa alishauri idadi yake ya wizara zisizidi 20 ili kuepuka matumizi makubwa ya fedha za umma.
Alisema baraza la mawaziri liwe na idadi ndogo ya wizara ili kupunguza matumizi yasiyokuwa ya lazima kwa serikali.
Aliongeza kuwa hata nchi za Kenya, Uganda na nyinginezo za Ulaya, mabaraza yao ya mawaziri, ni madogo. Alisema kama Rais Dk. Magufuli atahitaji kufanikiwa katika serikali yake, anapaswa kuteua mawaziri wenye uzoefu na wizara atakazoziongoza na siyo kumteua waziri asiye na ujuzi wa wizara husika.
“Rais Dk. Magufuli ateue mawaziri wenye utaalamu au elimu ya mambo atakayoongoza katika wizara husika na siyo waziri aliyesomea sheria akaongoze Wizara ya Maliasili na Utalii,” alisema Dk. Mpehongwa. Mhadhiri Mwandamizi wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Haji Semboja, alisema Rais Dk. Magufuli siyo mtu wa siasa, bali ni wa utekelezaji, hivyo mawaziri atakaowateua watakuwa wachapakazi. Alisema mawaziri wake watakuwa wamejifunga na utendaji kazi wake anaoutaka wa kuleta maendeleo hususan kuondoa umaskini.
“Rais Dk. Magufuli atateua mawaziri walio tayari katika utendaji wa kazi na siyo mawaziri wa maneno kuliko utekelezaji, watakuwa ni mawaziri wenye kuleta maendeleo,” alisema Dk. Semboja.
Alisema mawaziri wake hawatakuwa wabinafsi, bali watakuwa wazalendo watakowajali wananchi katika kuleta maendeleo ya kweli.
Alisema Rais Magufuli achague viongozi wenye taaluma sahihi na wizara watakazoziongoza kuliko kuangalia urafiki, udini na ukabila.
Kuhusu uundaji wa wizara, Dk. Semboja alisema Rais Dk. Magufuli anapaswa kuzifuta wizara ambazo hazina manufaa kwa wananchi ili zibaki wizara zenye maendeleo kwa jamii. Alisema hakuna haja ya kumuita mtu waziri wakati hana umuhimu wowote katika kuleta maendeleo, wizara yake inakuwa haina mchango wowote katika jamii. Naye Philipo William, mkazi wa Kimara, alisema namna Rais Magufuli anavyojieleza kwa umma jinsi atakavyofanya kazi, inadhihirisha wazi kuwa baraza lake la mawaziri litakuwa ni la kiutendaji zaidi kuliko maneno.
Alisema Rais Magufuli anapaswa kuunda wizara zenye umuhimu wa kuleta maendeleo kuliko wizara zisizokuwa na tija kwa jamii.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment