ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, November 26, 2015

PICHA: PAPA FRANCIS AWASILI NCHINI KENYA AHIMIZA AMANI NA UWAZI

 
 Papa Francis ameanza ziara yake Afrika kwa kuhimiza umoja, uwazi, kuwathamini vijana na kuyatunza mazingira. Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki aliwasili Nairobi mwendo wa saa kumi unusu jioni na kukaribishwa kwa shangwe na viongozi wa kisiasa na kidini uwanja wa ndege.
 Baada ya kuwasili, alielekea Ikulu ambako alipanda mti kisha kukutana na Rais Uhuru Kenyatta kabla ya kutoa hotuba yake ya kwanza.Akimkaribisha kutoa hotuba, Rais Kenyatta, alieleza umuhimu wa ziara ya kiongozi huyo wa kidini, akimkumbusha kwamba kesho ni siku ya mapumziko na siku ya kitaifa ya maombi Kenya.
 Aliposimama kuhutubu, Papa Francis alishukuru sana kwa alivyopokelewa kabla ya kuanza mara moja kusisitiza kuhusu umuhimu wa umoja na utangamano Afrika. Pia, alikariri umuhimu wa kuwa na uwazi na usawa akisema ndiyo njia bora ya kumaliza mizozo.
 Kadhalika, alisisitiza nafasi muhimu ya vijana kwa taifa. "Taifa lenu pia lina vijana wengi. Siki hizi nitakazokuwa hapa, nasubiri sana kukutana na wengi wao, kuzungumza nao na kuwapa matumaini katika ndoto zao za siku za usoni.” Alisema.
 "Vijana ndio rasilimali yenye thamani zaidi kwa taifa. Kuwalinda, kuwekeza katika vijana, na kuwasaidia, ndiyo njia bora zaidi ya kuhakikisha siku njema za usoni zenye kufuata busara na maadili ya kiroho ya wazee wetu, maadili ambayo ndiyo nguzo ya jamii.”
 Moja ya masuala ambayo amekuwa akitilia mkazo ni kutunza mazingira. "Kenya imebarikiwa sio tu na umaridadi, katika milima, mito na maziwa, misitu, nyika na maeneo kame, bali pia katika utajiri wa maliasili,” alisema.
 "Tuna wajibu wa kupitisha maumbile haya yakiwa hayajaharibiwa kwa vizazi vijavyo. Maadili haya yamekuwepo kwenye jamii za Kiafrika.”
 Kadhalika, alisitiza umuhimu wa usawa katika jamii na kuwajali wanyonge. Papa alitumia Kiswahili kuhitimisha hotuba yake, akisema: "Mungu abariki Kenya!”
 Alikuwa ameandika maneno yayo hayo kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Twitter alipokuwa safarini, saa moja hivi kabla ya kuwasili Kenya.
 Leo, Papa Francis amepangiwa kuongoza ibada ya misa katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Nairobi.
 Ataondoka Kenya Ijumaa kuelekea Uganda. Atakamilisha ziara yake Jamhuri ya Afrika ya Kati.

 

Taarifa na BBC Swahili na Picha na Ukurasa wa Rais Wa Kenya

No comments: