Advertisements

Monday, November 30, 2015

Serikali yazungumzia tishio la Marekani.

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.

Serikali imezungumzia tishio la Serikali ya Marekani la kusitisha misaada kwa Serikali ya Tanzania kutokana na mgogoro wa kisiasa Zanzibar na kukamatwa kwa maofisa wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu.

Ofisi ya Ikulu jana ilisema masharti yaliyotolewa na Serikali ya Marekani yanatekelezeka na yatamalizwa kabla ya kikao cha Bodi ya Shirika la Maendeleo ya Milenia (MCC) kukaa Desemba, mwaka huu.

Wiki iliyopita, Serikali ya Marekani iliitaka Serikali ya Tanzania kumaliza haraka mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar, vinginevyo upo uwezekano wa kusitishwa msaada wa zaidi ya Dola za Marekani milioni 472 (Sh. bilioni 999.4), za awamu ya pili ya fedha za MCC la nchi hiyo.

Fedha hizo za MCC awamu ya pili ni kwa ajili ya kuiwezesha Tanzania kusambaza umeme na kuwaunganisha wananchi wengi katika Gridi ya Taifa na uimarishaji wa taasisi zinazohusika na na sekta ya nishati.

Mambo ambayo Serikali ya Marekani iliitaka Tanzania kumaliza haraka ni suala mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar pamoja na kupata ufafanuzi wa watuhumiwa waliokamatwa kwa makosa ya mtandaoni, wakati wa Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, mwaka huu.

Akizungumza na Nipashe, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alisema suala hilo haliisumbui serikali na ni tatizo dogo ambalo linatatuliwa.

Alisema serikali ina uhakika wa kumaliza masuala hayo kabla ya kikao hicho cha Bodi ya MCC kukaa ambao masuala hayo yatakuwa yameshatatuliwa na kupatiwa ufumbuzi.

Alisema Bodi ya MCC ilikaa kikao chake cha kwanza Septemba, mwaka huu na inatarajia kukaa tena kikao chake Desemba, mwaka huu.

Alisema serikali ina uhakika Bodi ya MCC ikikaa kikao cha Desemba, mwaka huu itapitisha pasipo na shaka yoyote.

Aliongeza kuwa suala la sheria ya makosa mtandaoni, kuna watu walikamatwa na watafikishwa mahakamani ambapo mahakama yenyewe ndiyo itakayotoa hukumu na kama wana makosa watahukumiwa na kama hawatakutwa na makosa basi wataachiwa huru.

Balozi Sefue alisema suala hilo ni la kisheria, watu wametuhumiwa na wamepelekwa mahakamani ambako itaamua.

Kuhusu mgogoro wa Zanzibar, Balozi Sefue alisema kuna vikao vinavyoendelea vya kupata muafaka na mgogoro huo nao utamalizwa kwa haraka zaidi.

Marekeni ilieleza kuwa mambo hayo iliyotaka ipatiwe ufumbuzi, yataiwezesha MCC kuipima Tanzania katika sifa za kupata fedha hizo.
CHANZO: NIPASHE

2 comments:

Anonymous said...

mheshimiwa magufuli tunahitaji maendeleo ya nchi, dhamira na nia tumeiona, changamkia fedha hiyo kwa maendeleo ya nchi, siasa baadae, tuwa mzigo wa zanzibar huo tuchangamkie maendeleo ya nchi, ikifeli hapo linaweza kuwa janga kubwa likala kwetu mataifa yakaendelea kutuwekea vikwazo

Anonymous said...

First of all kwa nini kutegemea misaada kutoka nchi za nje wakati Tanzania inayo rasilimali za kutosha?? Ikumbukwe hiyo misaada imesainiwa wakati wa enzi za serikali ya awamu iliyopita kitu ambacho hawakujali kufanya kazi kwa maslahi ya wananchi. Kwa hali ya uchapa kazi ya Rais wa sasa JPM, misaada hii hazihitajiki. Pia misaada mingi za fedha nyingi kutoka nchi za nje zilikuwa zinafujwa na kuibiwa kitu ambacho JPM anaithibiti kwa sasa hivi.