ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, November 3, 2015

Ukawa ilivyoipa CCM majimbo

Baadhi ya viongozi wa vyama vinavyounda Ukawa,
By Kelvin Matandiko na Daniel Mjema, Mwananchi

Dar/Moshi. Licha ya makubaliano ya kusimamisha mgombea mmoja kila jimbo yaliyofikiwa na Ukawa, umoja huo wa Katiba ya Wananchi umepoteza majimbo mawili kwa sababu ya kushindwa kutekeleza makubaliano hayo.
Katika uchaguzi huo wa Oktoba 25, mwaka huu, umoja huo wa vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, umepata ushindi wa majimbo zaidi ya 60 kati ya 264 waliyokubaliana kusimamisha mgombea mmoja.
Katika uchaguzi huo wa Oktoba 25, mwaka huu, umoja huo wa vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, umepata ushindi wa majimbo zaidi ya 70 kati ya 264 waliyokubaliana kusimamisha mgombea mmoja.

Katika mgawanyo huo, Chadema ilisimamisha wagombea katika majimbo 138, CUF 99, NCCR Mageuzi 14 na NLD matatu lakini baadhi ya wagombea wa vyama hivyo hawakukubaliana na uamuzi huo na badala yake kugombea kivyake.

Kutokana na mazingira hayo, baadhi ya majimbo yaliyochukuliwa na CCM, yalikuwa na mvutano wa wagombea wa Chadema na CUF kwa pamoja, ambao walipata kura ambazo zingeweza kupeleka ushindi kwa Ukawa.

Jimbo la Segerea

Katika jimbo hilo ambalo upinzani ulikuwa na nafasi kubwa ya kulitwaa, aliyeshinda ni Bonna Kaluwa wa CCM aliyepata kura 94,640 na kuwashinda Julius Mtatiro (CUF) aliyesimamishwa na Ukawa akiwa na kura 75,744 na Anatropia Theonest wa Chadema kura 48,623.

Akizungumzia matokeo hayo, Mtatiro alisema, hiyo ina maana kuwa kura za Ukawa kama zingelipigwa kwa mgombea halisi wa umoja huo, wangeishinda CCM kwa zaidi ya kura 20,000 lakini kwa sababu zimepigwa kwenda vyama viwili wameshindwa.

Jimbo la Mwanga

Mgawanyiko huo wa Ukawa pia umempa nafasi Profesa Jumanne Maghembe ya kushinda tena ubunge katika Jimbo la Mwanga.

Katika jimbo hilo, NCCR-Mageuzi ilimsimamisha Youngsaviour Msuya na Chadema, Henry Kileo ambao kama wangeweka nguvu ya pamoja wangeshinda.

Katika uchaguzi huo, Profesa Maghembe alipata kura 21,982 wakati Kileo alipata 17,366 huku Msuya akiambulia 4,616.

“Ukichanganya kura za Msuya na zile za Kileo unaona kabisa wangepata kura 21,982 sawa na kura alizopata Profesa Maghembe,” alisema mkazi wa jimbo hilo, George Mberesero na kufafanua kuwa kukiuka makubaliano huenda kulichangia wagombea wa Ukawa kunyimwa kura. “Kama wangeungana, wapo waliompa kura Profesa Maghembe wangeamua kuwapa Ukawa lakini waliposhindwa kuafikiana inaonekana liliwavunja moyo baadhi ya wapigakura,” alisema.

Kileo alikiri kuwa kushindwa kukubaliana kwa njia moja ama nyingine kumechangia kumpa ushindi Profesa Maghembe .

Mtazamo wa wasomi

Mhadhiri kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), Richard Mbunda alitaja mambo matatu yaliyosababisha mivutano hiyo kuwa ni makubaliano ya vyama hivyo kufanyika kwa haraka na kuamuliwa na viongozi wa ngazi ya juu bila kuhusisha ngazi ya chini.

Katika hatua nyingine alisema wananachi wanapogundua migogoro ya ndani ya vyama wanakosa imani na mgombea.

“Anaona hamko makini na uchaguzi lakini kuna wengine wanapingana na uamuzi wa ngazi ya juu kupitisha mgombea wasiyekubaliana naye.”

Majimbo mengine

Hata hivyo, kuna baadhi ya majimbo ambako hesabu zinaonyesha hata kama wagombea hao wa Ukawa wangekubaliana, bado mgombea wa CCM angeshinda.

Majimbo hayo ni Mtama ambako Nape Nnauye wa CCM alishinda kwa kura 28,110, Seleman Mathew (Chadema) 13, 918 na Isihaka Nachinjita (CUF) 1,547.

Jimbo la Nkenge, Deodorus Kamala wa CCM alishinda kwa kura 36,769, Varelian Rugarabamu (Chadema), 27,848 na Salum Bagachwa (CUF) 281.

Jimbo la Nyamagama, Stanslaus Mabula wa CCM alishinda kwa kura 81,017 lakini Wenje Ezekiah (Chadema) 79,280 na Faida Potea (CUF) 1,005.

Bukoba Vijijini, Jason Rweikiza wa CCM alishinda kwa kura 70,183, Siliacus Rutashobya (Chadema) 22, 110 na Buberwa Kaiza (CUF) kura 4,467.

Kibaha Vijijini, Hamoud Jumaa wa CCM alishinda kwa kura 18,521, Editha Babeiya (Chadema) 4,777 na Hussein Chuma (CUF) 7,709.

Jimbo la Mkinga, Dustan Kitandula wa CCM alishinda kwa 21,623, Bakari Kassimu (CUF) 13,547 na Rachel Sadick wa Chadema 3,789.

Jimbo la Solwa, Ahmed Salum wa CCM alishinda kwa 57,962 na kuwaacha Jeremia Mshandete (Chadema) 30,648 na Kisenha Hangaya (CUF) 726.

Geita, Joseph Msukuma wa CCM alishinda kwa 44, 313 huku Mangilima Augutine (Chadema) akipata 18,909 na Malugu Magese wa CUF 1,786. Biharamulo Magharibi, Oscar Mukasa wa CCM alishinda kwa 41,879 dhidi ya Dk Anthony Mbassa (Chadema) 27,332 na Julius Mahano (CUF) 236.

Korogwe Mjini, Mary Chatanda wa CCM alishinda kwa 16,690 na kuwaacha Kimea Phares (Chadema) 7,025 , Masoud Mohamed (CUF) 113 na Rose Lugendo wa NCCR- Mageuzi 394.

Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani wa CCM alishinda kwa kura 53,906, Kimea Phares (Chadema) 17,003 na Peter Msangi wa CUF kura 784.

Itilima, Njalu Daud Silanga wa CCM alishinda kwa kura 55,850 huku Martine Makondo (CUF) akipata 28,000 na Martin Magile wa Chadema 8,000.

Handeni Vijijini, Mboni Mahita wa CCM alishinda kwa kura 50,268 dhidi ya Haji Mwikalo (Chadema) 8,993 na Kilango Richard (CUF) 5,580.

Kwimba, Sanif Mansoor wa CCM alishinda kwa kura 39,357 huku Shilogela Nganga(Chadema) akipata 7,338 na Julius Otto (CUF) 4,076.

Magu, Kiswaga Destery wa CCM alishinda kwa kura 61,508, Ngongoseke Julius Kalwinzi (Chadema) 32,217 na Lushanga Esau Sospeter wa CUF kura 894.

Kilosa Kati, Bawasili Mbaraka wa CCM alishinda kwa kura 55,703 lakini Msabaha Muhamed (Chadema) 19,632 na Mlapakolo Sadoq(CUF) kura 5,056.

Jimbo jingine ni Nzega Vijijini, Dk Khamis Kigwangalla wa CCM alishinda kwa kura 31,554 lakini Malongo Joseph Kulwa (Chadema) 10,401 na Katuga Khamis Idd (CUF) kura 663.

Jimbo la Ngara, Alex Gashaza wa CCM alishinda kwa kura 53,387 lakini Dk Peter Bujari (Chadema) 35,254 na Hellen Gozi (NCCR Mageuzi) 997.

Upande wa Jimbo la Geita Mjini, Kanyasu John wa CCM alishinda kwa kura 34,953, Rogers Ruhega(Chadema) 26,303 na Malebo Michael(CUF) kura 625.

Jimbo la Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka wa CCM alishinda kwa kura 63,120, Alistides Kashasila (Chadema) 53,405 na Ananias Rushojo (NCCR-Mageuzi) kura 418.

Hata hivyo, pamoja na kukiuka makubaliano hayo ya Ukawa, kuna baadhi ya majimbo ambayo mgombea mmojawapo wa Ukawa alishinda.

Maja ya majimbo hayo Ubungo ambapo Saed Kubeneya wa Chadema alishinda kwa kura 87,666, Ngole Khalifan (CUF) 2,283 huku Dk Didas Massaburi wa CCM akipata kura 59,514.

Majimbo mengine ni Singida Mashariki ambapo Tundu Lissu wa Chadema alishinda kwa kura 24, 874 dhidi ya Jonathan Andrew wa CCM kura 18,233 na Msafiri Patrick (CUF) aliyepata 84.

Katika jimbo la Ukonga, Waitara Mwita wa Chadema alipata kura 83,387 dhidi ya Jerry Silaa wa CCM aliyepata 76,975 na Khomcin Rwihula (CUF) 2,390.

No comments: