ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, November 5, 2015

Wagombea wataka Maalim Seif akamatwe Zanzibar.

Wagombea wanne urais wa Zanzibar wametaka kufutwa kwa uteuzi wa Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad na kufunguliwa mashtaka kutokana na kitendo chake cha kujitangaza ameshinda urais kabla ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) kutangaza matokeo.

Wagombea hao walitoa tamko hilo jana wakati wakizungumza na waandishi wa habari, Vuga, mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Akisoma tamko hilo kwa niaba ya wenzake, mgombea wa urais kupitia chama cha AFP, Soud Said Soud, alisema kitendo cha Maalim Seif kujitangaza kuwa mshindi katika uchaguzi huo kabla ya Zec ni kinyume cha sheria ya uchaguzi Namba 11 ya mwaka 1984.

“Tunamshauri Rais wa Zanzibar kufuta uteuzi wa Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad katika kipindi hiki cha mpito kutokana na kiongozi huyo kupoteza sifa za kuendelea kushika wadhifa huo na nafasi hiyo apewe mtu mwingine,” alisema Soud.

Alisema inashangaza kuona vyombo vya sheria na Zec wanakuwa wazito kuchukua hatua za kisheria wakati ni kosa kwa mgombea kujitangaza mshindi kabla ya matokeo rasmi ya tume hiyo.

“Hatua hiyo imeanza kujenga dhana miongoni mwa wananchi kwamba sheria za nchi hii zimewekwa kwa watu maalum na wengine wapo juu ya sheria hizo,” alisema mgombea huyo.

Aidha, alisema kauli na matamshi ya Maalim Seif ambayo amekuwa akiyatao hadharani dhidi ya Rais wa Zanzibar yanamuondolea sifa ya kuendelea kushika wadhifa huo akiwa mshauri mkuu wa Rais katika kutekeleza kazi zake kwa mujibu wa kifungu cha 39 (5) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Wagombea hao wameunga mkono uamuzi wa Mwenyekiti wa Zec kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu wa Zanziba uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Wagombea waliotoa tamko hilo ni, Ali Khatibu Ali (CCK), Hafidhi Hassan Suleiman (TLP) na Issa Mohamed Zonga ambao wamesema wanasubiri taarifa ya siku ya kufanyika uchaguzi mwingine.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Hivi swala zenu zinamfikiaje Mola wenu kama nyuso na utu wenu mmeuuza hapa duniani? Hizi ni sentensi za vibaraka mnaotumiwa kwa kushibisha matumbo yenu. Ni kura ngapi mmepata jumla? Nawaomba muwe na aibu na muogopeni Mungu kwani siku zetu hapa duniani si nyingi. Siku zote make mkijua hilo.