
Agizo hilo limetolewa na Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kata ya Nyihogo, Simon Mabumba katika kikao cha wazazi na kamati ya shule hiyo kilichofanyika juzi shuleni hapo ambapo wazazi walimlalamikia mwenyekiti huyo kufanya tuhuma za waziwazi na kushindwa kulitolea ufafanuzi suala hilo.
Baada ya tuhuma hizo za ubadhirifu, wazazi waliunda timu ya ufuatiliaji ambapo Mwenyekiti wa Muda, Bushiri Mashilabi alisema Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Nyihogo, Emmanuel Mrosso alikuwa akimkingia kifua mtuhumiwa huyo hali iliyozidi kuwapa wasiwasi wazazi.
Mmoja wa wazazi, Joyce Ruleka alidai mwenyekiti huyo alifikia hatua ya kuwadharau na kukiuka makubaliano yao katika vikao na kuchukua uamuzi wa kuzibadilisha matumizi fedha hizo na kuziingiza katika ukarabati wa madawati hali iliyowafanya kuyakataa majengo hayo na kumuamuru awarudishie fedha zao ili jukumu hilo walifanye wenyewe.
Hata hivyo, mwenyekiti huyo, Soka alikanusha madai hayo na kueleza kuwa pamoja na wazazi kudai warudishiwe fedha zao, yeye hahusiki na wizi wa fedha hizo, na kwamba suala la ukarabati wa madarasa alikubaliana na wazazi kuanza ukarabati wa majengo hayo kwa kutumia fedha za wafadhili na si za wazazi.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Lilian Lotasorwaki alisema wamepishana na mwenyekiti huyo baada ya kugoma kuingiza fedha za usafiri wa pikipiki yake binafsi Sh 500,000 kwenye taarifa ya wazazi hali iliyosababisha kuwa na mvutano mkubwa baina ya mwalimu na mwenyekiti huyo.
Hata hivyo, Diwani wa kata hiyo, Shadrack Mgwami alisema ufisadi uliofanywa na mwenyekiti huyo ni mkubwa na amekuwa akiwaongoza kwa ubabe huku akitumia ngao yake ya mwenyekiti kujinufaisha, hivyo alimtaka Kaimu Mtendaji wa Kata, mtu huyo akamatwe na kufunguliwa mashtaka.
Mabumba alisema Soka amekamatwa kwa tuhuma ya kula fedha za wazazi Sh milioni 3.6 zilizopangwa kufanya ukarabati wa madawati hivyo yupo chini ya ulinzi kwa Jeshi la Polisi kwa mahojiano ya ubadhirifu huo na ikibainika kuwa na kosa atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment