Wednesday, December 9, 2015

Aomba gharama za kumtunza Dk Mahanga gerezani



By Fidelis Butahe, Mwananchi

Dar es Salaam. Aliyekuwa Waziri wa Kazi na Ajira, Dk Makongoro Mahanga huenda akafungwa mwaka mmoja jela iwapo atashindwa kulipia Sh47milioni za gharama ya kesi aliyoifungua Mahakama Kuu kupinga taarifa na habari zilizoandikwa dhidi yake kwamba elimu yake ni feki.

Dk Mahanga ambaye kwa sasa ni kada Chadema alifungua kesi hiyo mwaka 2009 baada ya gazeti la Nipashe kuandika habari kuwa elimu yake ni feki, ikinukuu kitabu cha ‘mafisadi wa elimu’ kilichoandikwa na Kainerugaba Msemakweli na kutaja orodha ya wabunge akiwamo Dk Mahanga ambaye wakati huo alikuwa naibu waziri.

Kutokana na kushindwa kulipa gharama za kesi hiyo, Desemba 2 mwaka huu, Ofisi ya Msajili wa Mahakama Kuu imemuandikia barua Mkuu wa Gereza Kuu la Ukonga kutaka kujua maombi ya makisio ya gharama za kumtunza mfungwa wa kesi ya madai namba 145 ya 2009 ambaye ni Dk Mahanga.

Sehemu ya barua hiyo yenye kichwa cha habari ‘Maombi ya makisio ya gharama za kumtunza mfungwa kwa kesi ya madai namba 145/2009’ inasema, “...Mshinda tuzo ndugu Kainerugaba Msemakweli ameleta maombi ya kutaka mdaiwa Dk Makongoro Mahanga atumikie kifungo kama mfungwa wa kesi za madai. Tafadhali nijulishe makadirio ya gharama za kumtunza mfungwa wa kesi za madai kwa siku.”

Katika kesi hiyo, Dk Mahanga anatakiwa kumlipa Msemakweli Sh14milioni na mwandishi wa habari aliyeandika habari hiyo, Muhibu Said Sh33milioni.

Dk Mahanga alipoulizwa juu ya suala hilo alisema hana taarifa zozote na anaweza kulipa fedha hizo na kukwepa kwenda jela.

Msemakweli ambaye pia ni mwanasheria alisema jana kuwa baada ya Dk Mahanga kutoonekana, Mahakama Kuu iliamuru mlalamikiji alipe gharama za kesi.

Muhibu alisema, “Ninachotaka kuona kikifanyika ni kufuatwa kwa sheria tu na mhusika (Dk Mahanga) atekeleze kila anachopaswa kukifanya kwa mujibu wa sheria.”
MWANANCHI

No comments: