Monday, December 7, 2015

‘Kampuni ya kusafirisha magogo ilidanganya’

By Kelvin Matandiko na Musa Mwangoka

Dar/Rukwa. Wizara ya Maliasili na Utalii imesema kampuni iliyohusika na usafirishaji wa makontena 31 yaliyokamatwa na magogo ya mninga katika Bandari ya Dar es Salaam, ilidanganya hivyo itawajibika kuthibitisha ilikoyatoa.

Novemba 27, mwaka huu, wizara hiyo ilikamata makontena ya magogo yenye thamani ya Sh310 milioni yakisafirishwa kwenda China huku wasafirishaji wakidai yametoka Zambia.

Siku mbili baada ya kunaswa makontena hayo, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Adelhelm Meru alimwagiza Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Mohamed Kilongo kwenda ofisi za TRA zilizopo Tunduma kufuatilia nyaraka za kampuni iliyohusika na usafirishaji huo.

Hata hivyo, Dk Meru alisema jana kuwa ripoti ya ukaguzi huo imekamilika akisema awali wahusika walisema yametoka Zambia, lakini wizara yake imethibitisha siyo kweli.

“Wahusika watueleze wameyatoa wapi hayo magogo, kumbe ni ujanja ujanja tu, sasa watueleze source (chanzo), wakishindwa tutawafikisha mahakamani,” alisema Dk Meru.

Katika hatua nyingine, Polisi mkoani Rukwa wanamshikilia ofisa forodha wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kulisaidia jeshi hilo kwa uchunguzi wa magogo 665 na mbao za mkurungu zilizokuwa zikisafirishwa kinyume cha sheria. Mbao na magogo hayo yalikamatwa katika Kijiji cha Kasesya wilayani Kalambo, Mkoa wa Rukwa.
Mwananchi

No comments: