Tuesday, December 8, 2015

KIGOGO WA BANDARI ASEMA WAKUBWA WANAVYOTAFUNA BANDARI LAKINI SISI NDIO TUNAOPATA


Vigogo na watu wakubwa wenye ushawishi serikalini wakishirikiana na baadhi ya wafanyabiashara wametajwa katika orodha aliyokabidhiwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kama wahusika wakuu wa kupitisha kinyemela makontena takribani 2,780 na kukwepa kodi inayokadiriwa kuzidi Sh bilioni 600.
Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake gazetini, ofisa mmoja wa ngazi za juu wa Mamlaka ya Bandari (TPA) ameliambia gazeti hili kuwa ripoti hiyo imeeleza pia jinsi ‘wakubwa’ hao walivyofanikisha kupitisha makontena hayo kwa kutumia kampuni zao za mifukoni na vimemo.
Alisema tayari majina ya vigogo hao yamekabidhiwa kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ambaye tangu ateuliwe kuwa Waziri Mkuu amefanya ziara ya kushitukiza mara mbili Mamlaka ya Bandari (TPA) na kuibua ufisadi huo. Kwa mujibu wa ofisa huyo, vigogo hao wengine walikuwa wakituma ‘vimemo’ kwa wakubwa wa bandari ili wawapitishie makontena hayo, mengine yakiwa ni ya kwao, ndugu zao na wapendwa wao.

Ofisa huyo alisema kutokana na nyadhifa za wakubwa hao, ilikuwa ni mawili, ama ukatae ufukuzwe kazi au upitishe uendelee kubaki kazini na kuneemeka. Alisema kutokana na mtihani huo, wengi wao walilazimika kupitisha makontena hayo kwa lazima ili maisha yaweze kuendelea.


“Tunafanya kazi kwa kasi inayotakiwa, lakini wenzetu, hasa vigogo wakishatoa mizigo sisi ndio tunaopata tabu.
“Lakini wahusika kabisa wenyewe wanajulikana na majina yao yapo na kampuni wanazomiliki zipo na wengine wanatumia makampuni ya mifukoni, Waziri Mkuu tumempa majina yote na kila kitu…lakini tunaohangaishwa ni sisi watu wa chini,


Gazeti hili lilimtafuta kwa njia ya simu Kaimu Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Bandari (TPA), Janeth Luzangi, ambaye alikiri ripoti ya majina ya vigogo hao kuwasilishwa kwa Waziri Mkuu. Kwa mujibu wa Luzangi, ripoti hiyo iliwasilishwa juzi ofisini kwa Waziri Mkuu.

Wakati huo huo, uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika mamlaka mbili zinazofanya kazi kwa pamoja, Mamlaka ya Bandari (TPA) na ile ya Mapato (TRA) umebaini kuwako kwa hali ya sintofahamu, huku wafanyakazi wakisema wanafanya kazi kwa staili ya mguu mmoja ndani mwingine nje.

Kwa upande wa Bandari ya Dar es Salaam, baadhi ya wafanyakazi wameonekana wakihaha kuandaa ripoti zinazohusu mwenendo wa upakuaji na utolewaji wa makontena bandarini hapo. Mmoja wa wafanyakazi wa bandari aliyezungumza na gazeti hili alisema kwa sasa hali ni ya mchakamchaka, huku viongozi pamoja na baadhi ya wafanyakazi wakiwa wametingwa kuandaa ripoti hizo na ufuatiliaji ukiongezeka.

Pamoja na hilo, ofisa mwingine aliliambia gazeti hili kuwa miongoni mwa makontena 2,431 ambayo yamebainika kuwa hayakulipiwa kodi, yapo mengine yaliyouzwa kwa njia ya mnada, huku TRA ikielezwa kuwa ndio wahusika wa hilo.
“Huku sasa ni kazi tu! Watu wanapiga kazi kweli sasa hivi… viongozi wanahaha kuandaa ripoti ya makontena 2,431 ambayo yalitolewa hapa bandarini bila kulipia kodi, hata hivyo miongoni mwa makontena hayo yapo yaliyouzwa kwa njia ya mnada” 
alisema ofisa huyo aliyezungumza na MTANZANIA Jumamosi bila kutaja idadi ya makontena yaliyopigwa mnada, akisema ripoti inaandaliwa.
Akizungumzia hilo, Luzangi alisema TPA haihusiki na kupiga mnada makontena, kwamba wenye dhamana ya kufanya hivyo ni TRA.

MTANZANIA Jumamosi limepata taarifa zinazoonyesha kuwa aina nyingine ya wizi iliyokuwa ikitumiwa na vigogo hao ni kudanganya kwamba baadhi ya makontena yanasafirishwa kwenda nje ya nchi. Hata hivyo, makontena hayo yalikuwa yakibaki na bidhaa zake kuuzwa hapa hapa nchini na hivyo kukwepa kodi.

1 comment:

Unknown said...

Mvunja nchi ni mwananchi mwenyewe yaani inasikitisha sana kuona yakwamba watanzania wengi ambao serikali imetumia rasimali zake nyingi kuwasomesha ili kuliendeleza taifa wanatumia elimu yao kuibia serikali na watanzania wanyone kwa manufaa yao binafsi. Tunaomba sheria ichukuwe mkono wake bila ya kuoneana haya tafadhali.