Tuesday, December 8, 2015

Kocha aanika siri ya Cannavaro kuyumba.

Licha ya Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro' kusisitiza kuwa kiwango chake bado kiko juu, kocha wa zamani wa Yanga, Bandari Mtwara na Transit Camp, Kenny Mwaisabula, amesema kiwango cha beki huyo kimeshuka.

Katika siku za karibuni, wachambuzi wa soka wamekuwa wakidai kutoridhishwa na nahodha huyo wa Yanga na Taifa Stars huku wakiishauri Yanga kusaka mbadala wake.

Hata hivyo, beki huyo ameibuka na kusisitiza kuwa kiwango chake kiko juu na ana uhakika wa kufanya vizuri katika safu ya ulinzi ya Yanga msimu huu.

Cannavaro alisema anaamini mchango wake bado unahitajika kwenye kikosi cha Yanga.
Alisema kukosea katika baadhi ya mechi alizocheza msimu huu akiwa na Yanga na timu ya Taifa (Taifa Stars), haimaanishi kiwango chake kimeshuka na anastahili kuachwa.

"Bado niko vizuri, mchezaji wa mpira kila siku huwezi kuwa sawasawa, bado sijaona mchezaji wa kunitoa katika kikosi cha kwanza kama wengi wanavyofikiria," alisema Cannavaro.

Alisema kuwa yeye ni mchezaji mzoefu na anajua kupambana kulingana na hali ya timu mpinzani, hivyo bado ana nafasi ya kuisaidia timu yake katika harakati zao za kusaka mafanikio zaidi.

"Katika soka kuna mambo mengi yanaweza kukutokea au ukakumbana nayo, ninafahamu jinsi watu wanavyofuatilia nyendo zangu kwa ukaribu,'' alisema zaidi Cannavaro.

MWAISABULA AMCHAMBUA
Wakati Cannavaro akitamba kuwa bado yupo 'fiti, Mwaisabula aliliambia Nipashe jana kuwa kiwango cha beki huyo mwenye asili ya Zanzibar kimeshuka na anahitaji kuongeza mazoezi ili arejee katika kiwango chake halisi.
Kutokana na kuporomoka kwa kiwango chake, Mwaisabula alisema Cannavaro amekuwa akifanya makosa mengi katika kila mechi anayocheza na kuigharimu timu yake.

"Kiwango cha Cannavaro kimeshuka sana, amecheza mechi nyingi na hii inamfanya sasa afanye makosa mengi uwanjani, hata ukiangalia mechi mbili za mwisho kabla ligi haijasimama, hakuanza na nyingine alitokea benchi, hii inatoa picha kwanza kiwango chake hakiko sawasawa," alisema Mwaisabula.

Kocha huyo ambaye sasa ni mchambuzi wa soka, alisema kuwa haamini kama umri wa beki huyo (miaka 33) ni mkubwa na kumtaka afikirie kuachana na soka kama baadhi ya wadau wanavyosema.

"Yeye mwenyewe anatakiwa ajipime, asisikilize maneno ya watu, ninaweza kutoa mfano wa Willy Martin ambaye aliichezea Ushirika Moshi, Yanga halafu akaonekana kiwango chake kimeshuka, akataka kupokea, nilimchukua nikampeleka Majimaji akafanya mazoezi vizuri na alifanikiwa kucheza miaka mitatu na baadaye akajiunga Simba halafu Bandari," alieleza zaidi kocha huyo.

Kabla ya kuanza kwa msimu huu, Yanga ilisajili beki wa kimataifa kutoka Togo, Vincent Bossou, lakini ameshindwa kumnyang'anya namba Cannavaro kwenye kikosi cha kwanza cha mabingwa cha mabingwa mara 25 wa Tanzania Bara.

*Imeandaliwa na Somoe Ng'itu na Devotha Kihwelo
CHANZO: NIPASHE

No comments: