Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Cyprian Mkeha aliwaachia washitakiwa hao kwa dhamana baada ya kutimiza masharti, yaliyotolewa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Katika kesi ya msingi, washitakiwa wanane ambao ni wafanyakazi wa TRA pamoja na wafanyakazi wa Bandari Kavu (ICD) ya Kampuni ya Azam, wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, kwa kula njama za kudanganya na kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 12.7.
Washitakiwa walioachiwa kwa dhamana ni Masamaki, Mkuu wa Kituo cha Huduma kwa Wateja TRA, Habibu Mponezya na Meneja Udhibiti wa Forodha na Ufuatiliaji, Burton Mponezya, ambao waliwasilisha ombi la dhamana katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Waliachiwa baada ya kutimiza masharti ya kila mmoja kutoa mahakamani hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh bilioni mbili, kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika waliosaini hati ya dhamana ya Sh milioni 20 na mmoja kati ya wadhamini hao ni mfanyakazi wa serikali.
Katika dhamana yake, Masamaki aliwasilisha hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh bilioni 2.129 mali hiyo ipo katika eneo la Mikocheni na inamilikiwa na Sospeter Machunge ambaye aliwasilisha mahakamani hati ya kukubali, hati yake itumike kumdhamini Masamaki.
Habibu aliwasilisha hati mbili za mali zenye thamani ya Sh bilioni 2.129, ambapo hati moja ya mali yenye thamani ya Sh milioni 574 inamilikiwa na Salum Said, na nyingine ya Sh bilioni 1.55 inamilikiwa na Wakifu Abdallah.
Hata hivyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, alipinga hati hizo kupokelewa na kuhoji Abdallah amepata wapi mali zenye thamani hiyo akiwa na miaka 30. Abdallah alidai amerithi kutoka kwa baba yake na pia anajishughulisha na biashara ndogo ndogo.
Burton aliwasilisha hati mbili za mali zenye thamani ya Sh bilioni 2.3, moja ya mali yenye thamani ya Sh milioni 373 inayomilikiwa na Kampuni ya Theokratia Ltd, pamoja na hati ya mali yenye thamani ya Sh bilioni 1.6 inayomilikiwa na Sabah Salum, pia waliwasilisha hati za tathmini ya mali hizo.
Wamiliki wa mali hizo walikuwepo mahakamani na kuridhia hati zao zitumike kuwadhamini washtakiwa hao, pia washtakiwa hao walikuwa na wadhamini wawili ambao kila mdhamini mmoja alisaini hati ya Sh milioni 20 na kuwasilisha hati zao za kusafiria mahakamani.
Katika masharti mengine yaliyotolewa na Jaji Winifrida Korosso wa Mahakama Kuu, washtakiwa hao hawaruhusiwi kusafiri nje ya Dar es Salaam bila kibali cha Mahakama ya Kisutu na pia kila baada ya wiki mbili wanatakiwa kuripoti ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa.
Baada ya washitakiwa hao, wanaowakilishwa na Wakili Alex Mgongolwa na Majura Magafu, kukamilisha masharti ya dhamana, Wakili Msigwa alidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Hakimu Mkeha alisema washtakiwa watakuwa nje kwa dhamana na washitakiwa wengine, wataendelea kuwa rumande hadi Desemba 30, mwaka huu itakapotajwa tena.
Desemba 4, mwaka huu, Masamaki na wenzake walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka ya kula njama ya kudanganya na kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 12.7.
Wanadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Juni mosi na Novemba 17, mwaka huu sehemu isiyofahamika, walikula njama za kuidanganya Serikali kuhusu Sh bilioni 12.7, kwa madai kuwa makontena 329 yaliyokuwa kwenye Bandari Kavu ya Azam (AICD), yametolewa baada ya kodi zote kufanyika, jambo ambalo si kweli.
Katika mashtaka mengine, inadaiwa kati ya siku hizo, kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao vizuri, washtakiwa waliisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 12.7. Washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu mashtaka na kurudishwa rumande kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment