Advertisements

Tuesday, December 1, 2015

Miss Tanzania atajwa ufisadi wa Sh1.3 trilioni




Shose Sinare 
Kia ufupi Sinare hakupatikana kufafanua suala hilo ilhali Awale alifukuzwa nchini hivi karibuni.

Dar es Salaam. Aliyekuwa ofisa mwandamizi wa benki ya Stanbic tawi la Tanzania, Shose Sinare amehusishwa na mipango ya kifisadi ambayo imeisababishia Serikali ya Tanzania hasara ya Sh1.3 trilioni kati ya mwaka 2012 na 2013. Taarifa ambazo gazeti hili limepata kutoka Uingereza na hapa nchini, mwanadada huyo ambaye alikuwa mrembo wa Tanzania mwaka 1996, alishirikiana na aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Bashir Awale. Sinare hakupatikana kufafanua suala hilo ilhali Awale alifukuzwa nchini hivi karibuni. Alipoulizwa jana kuhusu tuhuma hizo, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hosea alisema anatambua suala hilo, linafuatiliwa na taasisi yake na hakutaka kutoa maelezo zaidi. Taarifa kwamba Serikali imetumbukia katika kashfa nyingine kubwa ya ufisadi zimebainika baada Taasisi ya Uchunguzi wa Makosa Makubwa ya Ufisadi ya Uingereza (SFO) kuwasilisha mahakamani ushahidi wake kwamba kiasi cha Sh1.3 trilioni kilipotea wakati wa uuzwaji wa hati fungani za Serikali kwa benki ya Stanbic inayomilikiwa na Standard Group ya Afrika Kusini. Mwanasheria wa SFO, Edward Garnier aliiambia Mahakama ya Southwark Crown ya jijini London, Uingereza inayosikiliza shauri hilo la kibiashara kwamba wakati wa mchakato wa benki kununua hati fungani Awale na Sinare walihusika. Garnier alisema Awale alifukuzwa kazi Agosti 2013 baada ya kushindwa kutoa ushirikiano kwa timu ya uchunguzi ya ndani na Sinare alijiuzuru Juni 2013 na hivyo naye alifanikiwa kukwepa uchunguzi.

Katika uchunguzi huo, Garnier alisema maofisa hao waliwataka maofisa wa Serikali ya Tanzania wawapatie kwanza kiasi cha Dola za Kimarekani 6 milioni (Sh13 bilioni) ili waweze kufanikisha mkopo wa Dola 600 milioni (Sh1.3 trilioni) na ziingizwe kwenye akaunti za maofisa binafsi wa Serikali. Dola 6 milioni ni asilimia moja ya mkopo huo wa Dola 600 milioni. Garnier alisema mpaka sasa hakuna anayefahamu fedha hizo zipo mikononi mwa nani. Hii ni mara ya pili SFO inafanikiwa kuibua ufisadi wa mabilioni ya dola kwa maofisa wa Serikali ya Tanzania baada ya ule wa mwaka 2002 ambapo maofisa waliongeza Sh73 bilioni katika bei halisi ya rada kutoka kampuni ya vifaa vya kijeshi ya Uingereza ya BAE Systems. Watanzania walipopata habari hizo walipiga kelele maofisa waliohusika wachukuliwe hatua lakini Serikali ilikataa. Baadaye yalifanyika makubaliano maofisa wasishtakiwe na BAE pia isishtakiwe, lakini fedha zilirejeshwa nchini.
Katika shauri hili yanataka kufanyika makubaliano kama hayo ya awali kwamba Stanbic inayonilikiwa na kampuni ya Standard Group ya Afrika Kusini ambayo ni kampuni tanzu ya Industrial and Commercial Bank of China (ICBC) inatakiwa kulipa Dola 32.2milioni sawa na Sh69 bilioni, ikiwa ni pamoja na kuwalipa SFO Dola 16.0 milioni sawa na Sh36.3 bilioni. Pia inatakiwa kulipa faini ya Dola 6 milioni (Sh12.9) na riba Dola 1 milioni (Sh2.1bilioni) kwa Serikali ya Tanzania.

Zitto Kabwe
Akizungumzia sakata hilo, Kiongozi Mkuu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe aliitaka Serikali kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria wote waliohusika na ufisadi huo. Zitto, kupitia taarifa kwa vyombo vya habari aliyoitoa jana alisema kati ya mwaka 2012/2013, Serikali kupitia Wizara ya Fedha iliuza hati fungani zenye thamani ya kiasi hicho cha fedha, ambapo dhamana za Serikali zilinunuliwa na benki ya Stanbic inayomilikiwa na benki ya Standard Group ya Afrika Kusini. “Hata hivyo, sehemu ya fedha hizo hazikuingia kwenye akaunti za Serikali ya Tanzania na pia gharama za bond (hati fungani) hiyo zilipaishwa kupitia wakala wa kati kati (middle men) na hivyo kupelekea rushwa ya takribani $60 milioni (Sh129 bilioni) kutolewa kwa maafisa waliothibitisha biashara hiyo,” alisema.

Stanbic
Hii itakuwa mara ya pili benki ya Stanbic kuingia katika mgogoro baada ya mwaka jana kutuhumiwa kupitisha kiasi kikubwa cha fedha kilichotokana na mgawa wa Sh306 bilioni kutoka Akaunti ya Tegeta. Baadhi ya maofisa, mawaziri na watu maarufu waliopewa fedha zinazoaminika zilitoka Tegeta Escrow kupitia benki ya Mkombozi walijulikana na wakafikishwa katika Baraza la Maadili, lakini waliopokea fedha kutoka Stanbic hawajulikani ingawa uchunguzi uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) aligundua kwamba watu hao walichukua kwa mifuko ya sandarusi na plastiki.

-Mwananchi












No comments: