ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, December 17, 2015

Muhimbili yapata CT Scan mpya

By Herieth Makwetta, Mwananchi

Dar es Salaam. Serikali imeanza kufunga mashine mpya ya vipimo ya CT Scan kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ikiwa ni mkakati wa kukabiliana na tatizo la upungufu wa vifaa tiba.

Kifaa hicho kimekuja wakati MNH ikihaha kutengeneza mashine nyingine kubwa ya uchunguzi ya MRI kwa agizo la Rais John Magufuli baada ya kukaa muda mrefu bila ya kufanya kazi na kusababisha wagonjwa kulazimika kuchukuliwa vipimo kwenye hospitali binafsi.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema jana kuwa ameamua kumtafuta mbia mwenye mashine hiyo ili kuendana na jitihada za kupunguza tatizo la wagonjwa kusubiri huduma ya uchunguzi kwa muda mrefu wakati mashine hizo zinapoharibika.

Ummy, ambaye jana asubuhi alifanya ziara yake ya kwanza hospitalini hapo, alisema baada ya kutaarifiwa kwamba mashine hizo zimeharibika siku zilizopita, alifanya mpango wa kuhakikisha inapatikana mbinu mbadala ili kupambana na tatizo hilo.

“Tunachojaribu kufanya hivi sasa si kununua mashine mpya. Hivi sasa watu wanatumia teknolojia mpya. Tumejifunza ili uweze kufanya vizuri zaidi hununui kifaa, unanunua teknolojia ndiyo matarajio yetu ya mbele.

“Tunamwambia mtu, tunataka utufungie vifaa kadhaa na anahusika na matenengezo. Tunamwambia kwa mwaka tutampelekea wagonjwa kadhaa,” alisema Mwalimu.

“Tumepata mbia ambaye ana mashine ya CT Scan, kwa hiyo hivi sasa inafungwa na tunategemea hadi kesho mchana (leo) huduma zitakuwa zimerejea. Muhimbili inaendelea kutengeneza mashine ambayo imeharibika na kufikia Jumatatu tutakuwa na mashine mbili za CT Scan,” alisema Mwalimu.

Alipoulizwa kuhusu hatima ya mashine ya zamani na namna mkakati wa kuzidilisha ili kuendana na kasi ya tekonolojia, Ummy alisema wataalamu wa Muhimbili wameeleza kuwa sababu ni kutofanyiwa matengenezo kwa muda mrefu.

Hata hivyo, alisema mashine hizo ni teknolojia ya zamani na zina vipande sita wakati wengine wanatumia CT Scan zenye vipande 64 hadi 380.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Dk Lawrence Museru alisema hospitali hiyo italipia gharama za wagonjwa wote wa dharura na wale wa msamaha ambao watapelekwa hospitali binafsi ili kupatiwa huduma ya vipimo vya MRI na CT Scan.

“Tutatoa huduma ya vipimo kwa wagonjwa wote wa dharura watakaofika hospitalini kwa kipindi hiki ambacho mashine zimeharibika, lakini wananchi watambue kwamba ubovu wa mashine hizi unasababishwa na uchakavu wa vifaa na kutofanyiwa matengenezo ya mara kwa mara,” alisema.    

1 comment:

Anonymous said...

kupata hii ct scan mpya si tatizo tatizo je wataalamu tunao?je ikiharibika kupata speya part mpaka nje na je utengenezaji wake tunao wa hapa nchini au tena ndo tuwakumbatiye wao kwa kila kitu.

Africa Tanzania yangu uhuru wa mamboleo bado utatutoa roho.

namkumbuka sana baba wa taifa alikataa yasichimbe madini yetu ardhini na yakaae huku huko mpaka watanzania tusome tuwe na elimu yetu tuje tuchimbe wenyewe tuwe na taalamu zetu tuiokoe nchi yetu kwa mafisadi wa nje na ndani.

leo hii namkumbuka sana baba wa taifa hakuna kama yeye hata kama ana mapungufu yake lakin japo mmoja jema analo na ni hili alitaka tuelimike tuje kuikomboa nchi yetu si leo kupewa vya bure kila pembe ya dunia.na kukenua mijinno na kufarahi.