
Moshi. Sakata la kukamatwa kwa raia wa India, Jain Anarungi kwa tuhuma za kutorosha madini ya Tanzanite yenye thamani ya Sh2.5 bilioni katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), limechukua sura mpya baada ya kampuni maarufu mjini hapa kutajwa kuyauza madini hayo kuanza kuchunguzwa.
Hata hivyo, tayari Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani ametangaza Serikali kutaifisha madini hayo yenye uzito wa gramu 2871, kwa mujibu wa Sheria ya Madini 6(4) ya Mwaka 2010 kama ilivyofanyiwa marekebisho 2015.
Habari za uhakika ilizonazo Mwananchi kutoka polisi na wizarani, zinadai kuwa Anarungi ameitaja kampuni hiyo kuwa ndiyo iliyomuuzia madini hayo, haijafahamika bado kama walioyauza waliyalipia kodi au la.
Kamishna wa Madini Kanda ya Kaskazini, Alex Magayane jana alisema uchunguzi bado unaendelea kuwabaini waliouza madini hayo kama walifuata sheria.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Fulgence Ngonyani alisema lengo la uchunguzi huo ni kutaka kuona kama utaratibu ulifuatwa, pia kubaini mtandao unaofanya kazi ya kutorosha madini nchini. Mfanyabiashara huyo ambaye anadaiwa kufika mara kwa mara Arusha kununua madini hayo, anadaiwa awali alichukuwa kibali cha kununua madini katika Kampuni ya Tanzanite Forever Ltd, lakini hata hivyo, hakumkuta mkurugenzi wa kampuni hiyo, Faisal Shabhai ambaye alikuwa safarini India kwa matibabu ya mtoto wake.
Akizungumza jana, Shabhai alithibitisha kumfahamu mfanyabiashara huyo na kueleza kuwa mara kadhaa alifika nchini kununua madini kwenye kampuni yake na alilipa kodi za Serikali. “Binafsi namjua huyu mfanyabiashara na alikuja kununua madini kwangu lakini baada ya kunikosa ndipo alienda sehemu nyingine,” alidai Shabhai.
1 comment:
Giiii hii Bongoland imeoza kweli. I feel very sorry for Magufuli, where will he start? everywhere kumeoza! It will take 50 years kuzoa uozo huo.
Post a Comment