Sunday, December 27, 2015

Siri sekunde 4,800 za Magufuli, Shein Ikulu

Harakati za kutafuta suluhu ya mzozo wa kisiasa wa Zanzibar, uliotokana na kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 zimeanza kupamba moto baada ya Rais John Magufuli kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, Ikulu jijini Dar es Salaam jana.

Rais Magufuli na Dk. Shein walifanya mazungumzo Ikulu kuanzia saa 8:30 hadi saa 9:50.

Rais Magufuli ambaye alikutana na Dk. Shein siku tano tangu atembelewe ofisini hapo na Maalim Sief Sharif Hamad, alibaki na siri ya mazungumzo hayo, kwa upande wake, ingawa mgeni wake alieleza shabaha ya kuja Bara.

Tangu kufutwa kwa matokeo hayo na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kumekuwa na mvutano wa kisiasa baina ya Chama cha Wananchi (CUF) ambacho Seif alikuwa mgombea wake na Chama cha Mapinduzi (CCM).

CUF imekuwa ikiilaumu ZEC kwamba iliamua kufuta uchaguzi huo na kuamuru marudio baada ya kuona CCM iliyokuwa imemsimamisha Dk. Shein kuwania kipindi cha pili ikielekea kushindwa na imekuwa ikisisitiza kwamba haipo tayari kurudia uchaguzi huo ambao tayari wananchi walishaamua.

Baada ya mazungumzo na Rais Magufuli, Dk. Shein alizungumzia kilichomleta Ikulu ya Dar es Salaam akisema kuwa nia ilikuwa kumweleza Rais Magufuli hali ya kisiasa Zanzibar na yanayoendelea baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.

Alisema alimweleza Magufuli kwamba mazungumzo ya kutafuta mwafaka Zanzibar yanaendelea chini ya Kamati Maalum ambayo anaiongoza, wakiwemo marais wastaafu Jakaya Kikwete, Abeid Aman Karume, Makamu wa kwanza wa Rais, Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Idd na Rais Mstaafu serikali ya awamu ya tano Zanzibar, Salmin Amour.

Dk. Shein alisema mazungumzo ya kutafuta mwafaka wa kisiasa visiwani humo yalishaanza tangu Novemba 9 na bado yanaendelea na aliahidi kuwa yakifikia mwisho watanzania watajulishwa.

“Nimekuja kumpa taarifa ya maendeleo ya mazungumzo yetu ili aweze kujua kinachoendelea Zanzibar... mazungumzo yanaendelea na yatakapokamilika umma utafahamishwa,” alisema Dk. Shein kwenye taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Dar es Salaam.

Kwenye taarifa hiyo hakukuwa na sehemu yoyote iliyomnukuu Rais Magufuli kuhusu mazungumzo hayo na mgeni wake badala yake taarifa nzima ilimnukuu Dk. Shein pekee.

Desemba 21, Rais Magufuli alikutana na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK), Maalimu Seif, kujadili hali ya kisiasa visiwani humo.

Licha ya kile kilichojadiliwa na viongozi hao kutowekwa bayana, taarifa za vyombo vya habari ziliwakariri zikisema wameridhishwa na hali ya usalama na utulivu inayoendelea.

Taarifa ya jana ilisema Rais Magufuli alimpongeza Rais wa Zanzibar, Dk. Shein, Hamad pamoja na viongozi wote wanaoshiriki mazungumzo ya kuleta hali ya uelewano Zanzibar.

Kadhalika, Rais Magufuli aliwapongeza na kuwashukuru wananchi kwa kudumisha amani na utulivu wakati wa mazungumzo baina ya viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha Mapinduzi (CCM) huko Zanzibar, taarifa ilisema zaidi.

Kwanini uchaguzi ulifutwa Zanzibar?
Mwenyekiti wa ZEC Jecha alisema ameamua kufuta matokeo ya uchaguzi huo baada ya kutawaliwa na vitendo vya udaganyifu ikiwemo idadi ya wapiga kura kuzidi katika baadhi ya vituo kinyume na idadi ya watu waliosajiliwa katika daftari la wapiga kura.

Alitaja sababu nyingine kuwa ni kutofautiana baina ya wajumbe wa ZEC kiasi cha kusababisha wengine kupigana na kwamba makamishna wa tume hiyo badala ya kufanyakazi zao walijigeuza mawakala wa vyama vyao.

Alisema aliamua kufuta uchaguzi huo kufuatia malalamiko ya vyama mbalimbali vya siasa kuhusu aksoro zilizojitokeza wakati na baada ya kupiga kura.

"Kumegundulika kasoro nyingi katika uchaguzi huu miongoni mwa hizo ni kubainika kwa baadhi ya vituo hasa Pemba vimekuwa na kura nyingi kuliko daftari la wapiga kura wa kituo husika," aliwahi kusema Jecha wakati akitangaza kufuta matokeo hayo.

Alisema hilo ni jambo la kushangaza ikizingatiwa kwamba "baadhi ya wapiga kura hawakwenda kuchukua vitambulisho vyao vya kupigia kura".
Aidha, Jecha alisema kura hazikupata ulinzi mzuri hususan kisiwani Pemba, kwani baadhi ya mawakala wa vya vyama vya siasa katika kisiwa hicho walifukuzwa.

Kutoka Zanzibar, makanisa mbalimbali yameingilia kati mzozo wa kisiasa visiwani hapa uliotokana na kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 kwa kuzitaka mamlaka zinazohusika kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hilo.

Wito huo ulitolewa jana na viongozi wa dini katika ibada ya Krismasi zilizofanyika katika Makanisa mbali mbali Mjini Zanzibar huku askari wakiwa wameimarisha ulinzi wa doria katika maeneo hayo.

Akihubiri katika Kanisa la Kiijili la Kirutheri Tanzania (KKKT) Mwanakwerekwe Mjini Zanzibar, Mchungaji Shukuru Steven Maloda, lazima tatizo hilo lifikie mwisho kwa viongozi kuendelea kukutana na kujadili mustakabali wa taifa hilo.

Alipongeza hatua zinazoendelea kuchukuliwa na viongozi wa kitaifa, wakiwemo Marais wastaafu Zanzibar za kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo ambalo bado linaendelea kutawala kwenye vyombno vya habari.

“Hatua ya viongozi kukaa pamoja kusaka suluhu ya tatizo ni jambo zuri na linathibitisha azma yao njema ya kuhakikisha Zanzibar inabakia kuwa nchi moja na yenye amani kwa manufaa ya wanachi wake," alisema.

Askofu wa Kanisa la Roman Jimbo la Zanzibar Dk. Augustino Shao alisema Serikali na wananchi wanapaswa kuenzi na kudumisha misingi ya amani na umoja wa Kitaifa kwa maendeleo ya taifa na wananchi wa Zanzibar.

Hata hivyo, alisema kuwa suala la uwajibikaji linapaswa kupewa umuhimu mkubwa ili kuharakisha maendeleo kutokana na Tanzania kuendelea kubakia nyuma kimaendeleo licha ya kuwa na rasilimali za kutosha ikiwemo ardhi, madini, hifadhi za wanyama, mito na gesi.

Alisema juhudi za kupambana na vitendo vya rushwa, ufisadi na kukosekana uwajibikaji kwa watumishi wa umma kunakofanywa na Rais John Magufuli zinapaswa kuungwa mkono na Wantazania.

“Lakini safari bado ndefu. Lazima serikali iwajibike zaidi ili kurejesha matumaini ya maisha bora kwa watanzania,” alisema Askofu Dk. Shao.

Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la Anglikana Doyosisi ya Zanzibar, Hafidh Michael aliwataka waumini kujenga utamaduni wa kusafisha mazingira bila ya kusukumwa au kusubiri wito wa viongozi wa kitaifa.

Alisema usafi wa mazingira upewe umuhimu na uzito katika jamii kutokana na umuhimu wake katika kulinda afya ya binadamu na ustawii wa maendeleo ya jamii kwa wananchi wake.

Ripoti zaidi na Mwinyi Sadallah, Zanzibar
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: