Tuesday, December 29, 2015

Uporaji wa fedha kwa bodaboda watikisa Dar

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura

Matukio ya uporaji na mauaji kwa kutumia pikipiki yanazidi kushika kasi na kusababisha hofu kubwa kwa wananchi na wafanyabiashara jijini Dar es Salaam pindi wanapotoka benki, wanaposafirisha fedha kutoka eneo moja kwenda jingine au kufanya manunuzi.

Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa, uporaji huo unaofanywa na majambazi kwa kutumia pikipiki hasa aina ya Boxer una mtandao mkubwa wa wahusika kutoka hatua ya kwanza ya mtu anapochukua fedha iwe benki au sehemu nyingine yeyoye hadi tukio zima la kuporwa linapotokea.

Jana watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi katika eneo la Mikocheni, jijini Dar es Salaam walimuua Conrad Kamukara, kwa kumpiga risasi akiwa anaelekea ofisi za kampuni ya Nabaki Afrika kununua vifaa vya ujenzi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, alithibitisha kutokea kwa tuki hilo na kusema watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wakiwa kwenye pikipiki walimvamia kijana huyo na kumpiga risasi na kumuua.
Kamanda Wambura alisema kabla ya tukio hilo kutokea, Kamukara alikuwa akiongea na ndugu zake kwa simu kuwa ataelekea Nabaki Afrika kununua vifaa vya ujenzi vikiwamo vigae.

Alisema polisi walipofika eneo la tukio walipekua katika gari la marehemu na kukuta Sh. milioni moja, kompyuta mpakato pamoja na simu ya mkononi.
Baadhi ya watu waliokuwapo katika eneo la tukio walilieleza Nipashe kuwa, majambazi hao walikuwa katika pikipiki (bodaboda) aina ya Boxer na walipotekeleza tukio hilo waliondoka kwa haraka.

Vyanzo vingine vilieleza kuwa majambazi hao baada ya mauaji hayo walichukua Sh. milioni sita kutoka kwa marehemu.

Nipashe limebaini kuwa matukio mengi ya uporaji wa fedha yanayotokea uhusisha baadhi ya wafanyakazi wa benki ambao siyo waaminifu, pamoja na baadhi ya walinzi wa kampuni binafsi ambao siyo waaminifu kwa kushirikiana na majambazi kufanikisha uporaji.

Kwa hali ya kawaida majambazi wanaotekeleza matukio hayo ya uporaji hawawezi kuhisi mtu aliyebeba kiasi cha fedha pasipo kupewa taarifa kamili kutoka kwa mtu wa karibu na anayebeba fedha hizo.

Inadaiwa wafanyakazi hao wa benki wasiowaaminifu kutokana na tamaa ya kupata fedha nyingi kwa haraka, hudiriki kupanga mpango na majambazi kwa kuwapa taarifa pindi mteja anapomaliza kuhudumiwa katika benki husika.

Chanzo kimoja (jina limehifanyiwa) kililieleza Nipashe kuwa, kuna baadhi ya wafanyakazi wa taasisi za fedha ambao siyo waaminifu huwasiliana na majambazi kwa njia ya simu muda mfupi baada ya mteja kuchukua kiasi kikubwa cha fedha.

Chanzo hicho kilieleza kuwa, mbali na wafanyakazi hao wasio waaminifu kuna kundi jingine la walinzi wa kampuni binafsi ya ulinzi ambayo hulinda katika baadhi ya benki ambao huwasiliana na majambazi wanapomwona mteja ametoka katika moja ya benki akiwa na kiasi kikubwa cha fedha.

“Utakuta mlinzi wa kampuni anapewa mshahara wa 150,000 kwa mwezi na analinda benki kubwa, halafu kila siku anaona watu wanatoka na maburungutu ya fedha, lazima atapanga dili na majambazi kufanya uporaji,” kilieleza chanzo hicho.

KAMANDA KOVA ATOA TAHADHARI
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, jana aliwatahadhairisha wafanyabiashara wakubwa hasa wa maduka makubwa ya kubadilisha fedha kuwa makini na usafirishaji wa kiasi kikubwa cha fedha kwa njia ya kawaida.
Alisema njia salama ya kusafirisha fedha ni ya kietroniki na endapo suala hilo litakuwa gumu watafute ulinzi wa polisi ili kuepuka kuvamiwa na watu wenye nia mbaya na kuhatarisha maisha yao.

MATUO YALIYOTOKEA HIVI KARIBUNI
Agosti 29, mwaka huu, eneo la Jangwani, jijini Dar es Salaam, watu wanaosadikiwa kuwa majambazi walilisimamisha daladala na kuingia ndani kupora mkoba uliodaiwa kuwa na fedha, kisha kumuua mtu huyo.
Watu hao waliokuwa na pikipiki aina ya Boxer walikuwa wakilifuatilia basi hilo lililokuwa likifanya safari zake kati ya Kariakoo na Mwenge na walipoingia katika gari hilo saa 7:00 mchana waliwaamuru abiria wote wainame na kuelekea kiti cha nyuma alikokuwa amekaa mtu huyo aliyebeba mkoba.

Aidha, Desemba 2, mwaka huu, watu wanne waliodaiwa kuwa majambazi walivamia gari dogo aina ya Toyota Saloon na kupora fedha zilizokadiriwa kuwa Sh. milioni 70.

Tukio hilo lilitokea katika makutano ya barabara ya Nyerere na Mandela, eneo la Tazara, karibu na ofisi za Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC).
Majambazi hao walikuwa katika pikipiki mbili na kulisimamisha gari hilo ambalo lilikuwa linaelekea benki.

Desemba 8, mwaka huu, watu sita wanaodaiwa kuwa majambazi walivamia benki mbili ya CRDB na DCB kwa wakati mmoja eneo la Chanika, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam na kumuua mlinzi kisha kupora kiasi kikubwa cha fedha ambacho hakikufahamika.

Watu hao walifika katika eneo hilo la tukio wakiwa na usafiri wa pikipiki aina ya Boxer nne wakiwa wamepakizana.

Mbali na matukio hayo, Aprili 21, mwaka huu, eneo la Kinondoni, watu wanne waliodaiwa kuwa ni majambazi walivamia gari la raia wa kigeni na kumpora Sh. milioni 15 kisha kutokomea wakiwa na usafiri wa pikipiki aina ya Boxer, kabla ya Jeshi la Polisi kuwasaka na kuwakamata baadaye.
CHANZO: NIPASHE

4 comments:

Anonymous said...

Nashauri wafanya kazi na walinzi wa mabenki wanyang'anywe simu zao(gsm) wanapokuwa kazini

Bob said...

Ndugu Muheshimiwa Kamanda Kova,wizi wa kutumia pikipiki na bunduki umeongeza kasi kubwa sasa. Nakushauri tuma vijana wako waanze msako haraka iwezekanavyo wakamate pikipiki zinazotumiwa kwa ujambazi zipo mitaani kila siku mnapishana nazo. Tusingoje mpaka Muheshiwa Raisi Magufuli akukosoe kwamba huna kasi ya kutosha. Majambazi wanatembea na pikipiki mchana kweupe na mnapishana nao kila siku. Naomba Kamanda Kova usilikalie kimya hili. Tutaokoa maisha ya watu wengi iwapo kuanzia leo Polisi pamoja na wananchi wenye nia njema tutupie macho kwenye pikipiki zote zipitazo machoni kwetu zenye mashakamashaka zisimamishwe na kukaguliwa. Naamini kwa staili hii itapunguza ujambzi huo. Aksanteni.

Anonymous said...

Ilitakiwa wafanyakazi wote wa benki wasiingie na simu ofisini iwe amri. Walizi wawe wanakaa nje ya mlango. Humo ndani wanatafuta nini wakati wao ni walinzi?!!.. Tena pamoja na kukaa nje simu ni marufuku. Watu wamegeuka wanyama. Na hizo piki piki wameruhusu nyingi mno. Zifanyiwe usajiri upya. Hasiye na leseni ya kuendesha pikipiki apigwe chini. Kupunguza matatizo. Wawawekee utaratibu boda boda wanavuruga amani.

Anonymous said...

WIZI WOWOTE ULE AMBAO CHANZO CHAKE NI WATEJA KUCHUKUA FEDHA BENKI,NI WAFANYAKAZI WA BENKI HUSIKA AMBAO KIMSINGI NI MAJAMBAZI NA NDIYO WANAOTOA TAARIFA KWA MAJAMBAZI WENZAO AMBAO WANAKUA WAMEKWISHA JIPANGA NJE.KITU AMBACHO SIJAKIFAHAMU NI KITU GANI POLISI DAR-ES-SALAAM WANASHINDWA KUKIELEWA, HAWAKIFAHAMU.KILICHOPO NA CHA UKWELI NI KWAMBA USHIRIKIANO WA UJAMBAZI WA MABENKI YETU NI MAJAMBAZI WAFANYAKAZI WA BENKI,MAJAMBAZI WANAOSUBIRIA NJE AMBAO WAPO MATAWI MAWILI,RAIA NA POLISI AU ASKARI WA MAJESHI MENGINE WASIO WAAMINIFU,WALE WAIOFUKUZWA KAZI,WALE WALIOPO BADO MAJESHINI LAKINI HATA UONGOZI WAO WANAWAFAHAMU KWA KUWATUHUMU KUKOSA UAMINIFU.HII HAIWEKWI WAZI KWA NINI?RAIA WANAZIDI KUANGAMIA.TATIZO LINAELEWEKA,TATIZO LINAFICHWA.DAWA NI MOJA TUU KUWABADIRISHA MAKAMANDA MALEGEVU WA MBINU,UELEWA,WABISHI NA WADAU-SHIRIKI WA UJAMBAZI.POLISI MNATUMALIZA,TUKIMBILIE WAPI? JESHINI?