TAARIFA
KWA UMMA.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. George
Simbachawene (Mb) amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala kumsimamisha kazi
mara moja Kaimu Afisa Biashara wa Manispaa ya Ilala Bw. Dennis. N. Mrema kuanzia leo tarehe 07 Januari, 2016 kwa kosa
la kusababisha upotevu wa Mapato ya Serikali kutokana na urasimu wa kukusudia,
mazingira ya rushwa na uzembe katika utoaji wa leseni za Biashara.
Kutokana na hali hiyo Mhe. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
TAMISEMI ameelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kumuondoa
kwenye nafasi yake Kaimu Afisa Biashara wa Manispaa ya Ilala na nafasi yake
kukaimiwa na mtu mwingine ili kupisha uchunguzi zaidi juu ya tuhuma zilizotolewa
dhidi yake.
Mhe. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais –TAMISEMI amefikia
uamuzi huu baada ya kupokea malalamiko mengi kutoka kwa Wafanyabiashara ambao wamemlalamikia
Mtendaji huyu kwa ukiukwaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu za utoaji wa Leseni
za Biashara, Urasimu na Mazingira ya rushwa.
Katika uchunguzi wa awali uliofanyika kwenye
Halmashauri ya Manispaa ya Ilala mambo yafuatayo yamegundulika:
(i)
Ukiukwaji wa Makusudi wa Sheria, Kanuni na
Taratibu za utoaji wa Leseni za Biashara.
(ii)
Kutoa
Leseni za Biashara zaidi ya 843 bila kuwa na Vyeti vya uthibitisho wa Walipa
kodi ‘Tax Clearance Certificates” hivyo
kuikosesha Serikali Kodi ya Mapato.
(iii)
Kukaa na fomu za Wafanyabiashara 336 kwa muda
mrefu bila sababu za msingi.
(iv)
Kukiuka Mwongozo wa Mkataba wa Huduma kwa
wateja ambao unamtaka Afisa Biashara kutoa Leseni za Biashara ndani ya siku 2
hadi 3 baada ya muombaji kuwasilisha maombi yake ya kupatiwa Leseni ya Biashara.
Aidha,
Mheshimiwa Waziri wa Nchi , Ofisi ya Rais-TAMISEMI amewaagiza Maafisa Biashara
wote nchini watoe huduma za Leseni kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu , kuacha
urasimu na kujiepusha na vitendo vya rushwa.
Imetolewa
na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Ofisi ya Rais-TAMISEMI,
07 Januari, 2016.
No comments:
Post a Comment