Monday, January 18, 2016

Cannavaro: Mkwasa hajanitendea haki

Siku chache baada ya aliyekuwa nahodha wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Nadir Haroub 'Cannavaro' kutangaza kujiuzulu kuichezea timu hiyo, ameitaja sababu mojawapo ni jinsi uteuzi nafasi hiyo kwenda kwa mshambuliaji, Mbwana Samatta ulivyofanyika.

Wiki iliyopita, Kocha wa Taifa Stars, Boniface Mkwasa, alitangaza kumpa Samatta unahodha ikiwa ni siku chache baada ya mshambuliaji huyo wa zamani wa African Lyon na Simba kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika kwa wachezaji wanaocheza ndani ya Afrika.

Cannavaro alisema kuwa hakufurahishwa na kitendo cha kupokonywa unahodha bila ya taarifa rasmi huku akiwa ameitumikia Stars kwa muda mrefu na kwa kiwango cha juu.

"Naona sijapewa heshima yangu, sikupewa taarifa yoyote kama naondolewa kwenye unahodha na badala yake taarifa nimezipata kupitia vyombo vya habari, sidhani kama ni utaratibu mzuri," alisema Cannavaro.

Beki huyo anayeichezea Yanga aliitaja sababu nyingine iliyomuondoa Stars ni lawama za mfululizo alizokuwa akizipata pale timu hiyo inapofungwa au kufanya vibaya kwenye mechi zake za mashindano au kirafiki.

“Katika mechi hiyo tuliyopata kipigo cha kufungwa magoli 7-0 na kama unakumbuka mchezo wa nyumbani tulitoka sare ya magoli 2-2, mechi hiyo muda mwingi tulicheza pungufu baada ya Mudathir (Yahya) kutolewa kwa kadi nyekundu, tulijitahidi kupambana kuhakikisha tunawatoa Algeria lakini ikashindikana, cha ajabu mara baada ya mechi hiyo nilionekana mimi pekee ndiye niliyefungisha, nilijisikia vibaya sababu nilipambana kwa ajili ya taifa langu na mwisho wa siku nikaonekana si lolote,”alisema nyota huyo ambaye pia ni nahodha wa kikosi cha Zanzibar Heroes.

Aliongeza kuwa baada ya kujiondoa Stars, anahamishia nguvu zake kwenye timu yake ya Yanga ili iweze kufanya vizuri kwa kutetea ubingwa wake na mashindano ya kimataifa watakayoshiriki.

“Nimecheza kwa miaka 10, mengi nimefanya na nimepata, muda umefika wa kuwaachia wengine waje kuichezea Stars, kuitoa hapa ilipo na kuipeleka mbele zaidi, nitaelekeza nguvu zangu kwa Yanga.

Naamini ni uamuzi sahihi kwa wakati sahihi kwangu kutangaza kustaafu kuichezea Stars, ninaamini wapo wachezaji wengi wanaochipukia watakaonirithi,” alisema Cannavaro.

Hata hivyo Mkwasa alipotafutwa na gazeti hili kutoa maoni yake juu ya uamuzi wa Cannavaro, hakuwa tayari kuzungumzia jambo hilo.

"Sina comment (maoni) yoyote, kwanza sina taarifa hizo kwa hiyo siwezi kuzungumzia lolote," alisema Mkwasa.

Beki huyo ameichezea Stars tangu mwaka 2007 na alichukua mikoba iliyoachwa na Shadrack Nsajigwa 2012.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: