Kahama. Fedha za ushuru wa huduma zilizotolewa na Mgodi wa Buzwagi mwaka jana, zimewaponza vigogo watano wa Halmashauri ya Mji wa Kahama, mkoani Shinyanga baada ya Baraza la Madiwani kuwasimamisha kazi kwa kudaiwa kuzitumia vibaya kwa maslahi binafsi.
Hatua hiyo ilikuja baada ya kujiridhisha na taarifa ya kamati ya uchunguzi iliyoundwa na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Vita Kawawa kuonyesha zaidi ya Sh800 milioni kati ya Sh1.6 bilioni hazijulikani ziliko.
Miongoni mwa watumishi hao yumo aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kabla ya kuhamishiwa Halmashauri ya Longido mkoani Manyara, Felix Kimario na aliyekuwa Mhandisi Mkuu wa Halmashauri ambaye alihamishiwa Halmashauri ya Nanyumbu mkoani Mtwara, Msumba Msoka.
Viongozi wengine waliosimamishwa kazi na baraza hilo ni pamoja na Mweka Hazina wa Halmashauri, Wilfred Kisheri na Mhasibu wake, Alex Mroso kwa kudaiwa kushindwa kutoa takwimu sahihi ya kampuni za nje zinazofanya kazi ndani ya mgodi huo na kusababisha hasara ya Sh400 milioni pamoja na Ofisa Biashara wa Halmashauri hiyo, Elius Mollel.
Katika tuhuma hizo, yumo pia Katibu wa Bodi ya Zabuni, Joseph Maziku ambaye ni Ofisa Ugavi wa Halmashauri hiyo, kwa pamoja, juzi walisimamishwa kazi kupisha uchunguzi ambao kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Abel Shija utafanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Kabla ya kusimamishwa kazi vigogo hao, Kawawa aliwataka madiwani kuhakikisha wanachukua hatua kali za kisheria dhidi yao kwa kuisababishia hasara Halmashauri hiyo.
Kawawa alitoa kauli hiyo alipokuwa akiwasilisha taarifa ya kamati yake ya uchunguzi aliyoiunda kuchunguza matumizi mabaya ya fedha hizo ambazo zingetumika kwenye miradi iliyotekelezwa chini ya viwango.
Kawawa alisema Idara ya Fedha chini ya Mweka Hazina wake, Kisheri, ilitoa takwimu za kampuni 17 badala ya 168 za nje zinazofanya kazi ndani ya mgodi huo.
Akitangaza uamuzi wa kuwasimamisha kazi watumishi hao, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Abel Shija alisema Baraza limeridhia na watumishi wengine watano watakuwa chini ya uangalizi.
Watumishi hao ni wajumbe wa bodi ya zabuni wanaodaiwa kushiriki kutoa zabuni hewa kwa kampuni hizo.
“Tunaendelea kuangalia nyendo zao na kama watabainika walishiriki, watachukuliwa hatua pia,” alisema
No comments:
Post a Comment