Hayati Padri Calisti Nauli Nyambo |
Hayati Padre Calisti Nauli Nyambo(pichani) ni mtoto wa tatu wa Familia ya hayati Baba Laurenti Ngasamiaku Nyambo na Mama Augustina Ngambakiha Msaki, alizaliwa tarehe 17/5/1939, katika Kijiji cha Kwamare Kirua Vunjo. Ndugu zake wa kuzaliwa ni Clementina, Martina, Beda, Damas, Adela, Eligi, Flora, Hilda, Domitila na Mary. Calisti alibatizwa na kupokea Sakramenti ya Ekaristi na Kipaimara katika Parokia ya Kirua.
ELIMU YA MSINGI
Mwaka 1948 hadi 1953 alisoma katika Shule ya Msingi Iwa hadi darasa la sita. Kwakuwa wakati ule shule ya msingi Iwa ilikua na darasa la kwanza hadi la sita tu, Calisti aliendelea na masomo ya darasa la saba kule milimaniUsambara mwaka 1954 katika shule ya Msingi Gare. Mwaka 1955 aliendelea na masome ya darasa la nane katika Shule ya Msingi Kichwele (au Uhuru) katika Jimbo Kuu la Dar-es-Salaam.
ELIMU YA SEKONDARI
Mwaka 1956-1957 Calisti aliendelea na masomo kidato cha kwanza na cha pili katika Shule ya Sekondari Umbwe.Alifuzu vizuri masomo yake akachaguliwa kujiunga na kidato cha tatu na cha nne katika Shule ya Sekondari yaPugu Dar es Salaam 1958 hadi 1959.
WITO WA UPADRE
Calisti aliongozwa na Roho Mtakatifu alijisikia kuitwa na kuvutwa na wito wa Upadre. Akaomba kujiunga na masomo ya Seminari kupitia Jimbo Katoliki Moshi. Mwaka 1960 hadi 1962 alijiunga na Seminari Kuu ya Kibosho.
Baada ya kuhitimu masomo ya Falsafa, aliamua kukatiza masomo na malezi ya Seminari. Akaajiriwa kufanya kazi Benki na Serikalini. Kutokana na nguvu ya wito wa Upadre fedha za mshahara hazikutosheleza dhamira na malengo ya maisha yake ya kupenda kumtumikia Mungu. Hivyo aliamua arudi Seminari kuendelea na safari yawito wa Upadre.
Akaomba kujiunga na Jimbo Kuu la Dar-es-Saam. Mwaka 1966 alipelekwa kusoma Teolojia katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Paulo, Kipalapala Tabora. Mwaka 1969 alihitimu masomo na malezi ya seminari akapewa Ushemasi na mwaka huo huo tarehe 14 December 1969 akapewa sacramenti ya daraja la upadre na Mwadhama Cardinal Laurian Rugambwa na akawa padre wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam.
UTUME WA UPADRE
Kwa muda wa miaka tisa alifanya utume katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Alianza kama paroko msaidizi nabaadaye paroko katika parokia kadhaa za Jimbo Kuu la Dar es salaam. Tangu mwaka 1973 hadi 1976 aliteuliwa na Mwadhama Kardinali Rugambwa kuwa Vikari wa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es salaam. Kutoka Dar Es Salaam alifanya utume pia katika Jimbo Kuu la Arusha kwa muda mfupi kisha Mhashamu Askofu Denis wa Jimbo la Arusha akamtuma Marekani kwa masomo ya Chuo Kikuu.
MASOMO YA CHUO KIKUU
Mwaka 1978 alienda Marekani akasoma katika Chuo cha Majesuiti kilichoko Berkeley, California, akatunukiwa Master Degree ya Teolojia mwaka 1982. Alipenda bado kujiendeleza ndipo alipoenda katika Jiji la Washington DC akasoma katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Amerika (Catholic University of America) na akafuzu vizuri akatunukiwa Master of Arts Degree in Religious Education mwaka 1987.
UTUME NCHINI MAREKANI
Padre Nyambo alikuwa padre wa kwanza mwafrika kufanya kazi katika jimbo la St. Petersburg, Florida, Amerika. Alianza kwa kufanya utume wakati wa kiangazi (Summer holidays) katika parokia ya Mt. Joseph 1982 na Parokia ya Utatu Mtakatifu (Blessed Trinity) mwaka 1986-1987.
Askofu wa jimbo la St. Petersburg alifurahiwa na kuridhika na maisha na utendaji wa Padre Nyambo ndipo akampa utume kamili kama wakili paroko katika parokia moja katika jiji la Tampa, Florida mwaka 1988-1991. Wakati huo huo alikuwa Mkurugenzi wa jimbo wa utume wa Wakatoliki Waamerika Weusi katika jimbo la St. Petersburg.
Mwaka 1992-1993 alikuwa Paroko Kiongozi wa parokia ya Mt. Peter Claver Tampa. Kwa kuwa alifanya utume wake vizuri alipewa cheo cha Uparoko tangu mwaka 1993-1997.
Kwa muda wa miaka sita alikuwa Paroko katika Parokia ya Mt. Joseph St Petersburg, yaani, tangu mwaka 1997 hadi 2003. Mwaka huo huo wa 2003 alikuwa Paroko wa Parokia ya Watakatifu Wote (All Saints Parish) hadi mwaka 2013 alipostaafu kisheria.
Pamoja na majukumu ya uparoko na ya Kijimbo, Padre Nyambo alikuwa raisi wa utume wa Waamerika Weusi Wakatoliki katika Mkoa wa Florida.
Alikuwa pia Mjumbe katika Bodi ya Kitaifa ya Wakleri Waamerika Weusi. Padre Nyambo alikuwa pia ni Raisi Mwanzilishi wa Wakatoliki Wakleri Weusi na Umoja wa Mashirika ya Kidini Amerika. Alikuwa pia Mwakilishi wa Kitaifa wa Utume wa Walei Amerika, Mshauri wa Kitaifa wa Shirikisho la Kitume la Watanzania kule Amerika, Mjumbe wa Bodi katika Ofisi za Utume wa Kichungaji kwa Wahamiaji, Wakimbizi na Wasafiri.
Mwaka 2008 alitunukiwa tuzo ya heshima ya askofu mkuu Silvano Tomas kutokana na majitoleo na kazi nzuri kwa wahamiaji. Mwaka 2012 alitunukiwa tuzo ya mtumishi wa Kristu kutoka kwa Congress ya Kitaifa ya Wakatoliki Weusi wa Amerika.
WASIFU WA PADRE KALIST NYAMBO
Padre Kalist alikuwa mtu wa watu. Aliwapenda watu na hasa watu wa taifa lake. Alipenda na kuheshimu nyumbani alikozaliwa, alikokulia, kanisa alikobatizwa, kupata komunyo na kipaimara na shule Msingi ya Iwa alikosoma hadi darasa la sita. Ni miaka michache tu iliyopita alijenga vyumba vipya vya madarasa na vyoo katika shule ya Iwakama shukrani upendo kwa watu wa Kirua.
Alipenda na kutamani sana kuona maendeleo mazuri ya taifa letu. Alipenda kufadhili miradi ya maendeleo hususan elimu na afya. Watu wote waliomfahamu na kumtembelea kule Marekani watashuhudia alivyokuwa akishirikiana vizuri na watu wote na hasa watanzania aliowafahamu kule Marekani. Alikuwa mchapakazi na mwenye furaha kila wakati.
UGONJWA NA KIFO
Mwishoni mwa Mwaka jana, masaa machache kabla ya mwaka mpya Padre Calist Nyambo alishikwa na ugonjwa wa kiharusi akiwa nyumbani kwake akiwa anajiandaa kwenda kufanya Ibada kesho yake ambapo alipelekwa Hospitali kwa matibabu zaidi huko nchini Marekani lakini jitihada za Madaktari Bingwa za kuokoa uhai wake hazikuzaa matunda. Ilipofika tarehe 3 Januari, 2016 Mungu aliyempenda sana Padre Calist Nyambo alimwita kwake akamshikirishe furaha za Ufalme wake.
Ndugu wa marehemu na wanaukoo wote wa Nyambo wanatoa shukrani za kipekee kwa Uongozi wa Diocese ya St. Petersburg, Askofu Amani wa Moshi, Paroko, Watanzania wote wanaoishi USA pamoja na Madaktari kwa namna walivyoshiriki kwa hali na mali katika kufanikisha kuokoa maisha ya mpendwa wetu. Mungu awajalieni wingi wa Baraka na hasa afya ya roho na mwili. Asanteni sana. Taratibu za kuusafirisha Mwili wa Padre Calisti kutoka nchini Marekani kuja nchini Tanzania zinafanyika ambapo mazishi yanatarajiwa kufanyika mwishoni mwa wiki hii katika Kanisa Katoliki Kirua Iwa, Diocese ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro.
Raha ya milele umpe ee Bwana na mwanga wa milele umwangazie. Ampumzike kwa amani. Amina.
3 comments:
We already miss you babu...rest in peace - Love Devota & Izzy
I will miss u alot dad. Am speechless
Poleni ndugu, jamaa, na marafiki wote walioko USA na Tanzania. Poleni sana huu ni msiba mkubwa kwetu wote. Mungu amweke pema peponi. RIP
Post a Comment