Mwanza. Mama wa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mabatini, Janeth James (6), aliyekufa maji baada ya kusombwa na mafuriko yaliyotokea wiki iliyopita, amesema anajuta kumpeleka mwanaye kuanza darasa la kwanza.
Mama huyo, Nyanchuga John mwenye watoto wawili alisema juzi kuwa asingempeleka shule mtoto wake asingesombwa na mafuriko na kufa maji.
“Najuta kwanini mwanangu tulikupeleka shuleni, bora tungekuacha uendelee kukaa nyumbani, kwani haya yote ya kusombwa na mafuriko yasingekupata, shule imenipotezea mtoto.
“Kifo chako kimeicha familia katika simanzi kubwa kwasababu ulikuwa mtoto wetu wa kwanza na umemuacha mdogo wako pekee yake.
“Mwanagu aliipenda shule, alikuwa na ndoto kubwa maishani mwake, lakini bora angeiacha shule machoni mwetu, umeniachia simanzi umeondoka kipenzi changu,” alisema Nyanchuga.
Baba wa marehemu, James Japheth alisema kifo ni mipango ya Mungu na hakuna anayeweza kuibadilisha.
Mwili wa Janeth ulizikwa juzi katika makaburi ya Kisesa baada ya kupatikana kwenye Mwalo wa Kirumba Ziwa Victoria ukielea.
Janeth alisombwa na mafuriko Januari 14, saa sita mchana baada ya kumponyoka baba yake katika daraja la Mabatini wakati akitoka kumfuata shuleni siku ya pili tangu aandikishwe darasa la kwanza.
No comments:
Post a Comment