ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, January 26, 2016

Kafulila matatani tena kwa kumtukana DC

Aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Kigoma kwa madai ya kumtukana Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Hadija Nyembo.

Katika hati ya madai, inadaiwa kuwa Kafulila alitoa ligha ya matusi kuwa “mtu kama Hadija Nyembo unamuokota wapi na kumpa ukuu wa Wilaya. Unamchukua shangingi la mjini huko unasema aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya. Mkuu wa Wilaya akija hapa mana yake polisi wampigie saluti, kuna polisi wenye akili hapa kuliko huyu Mkuu wa Wilaya, wanampigia saluti kwa basi tu mana yake hana akili.”

Kutokana na maneno hayo inaonyesha kuwa Hadija si mtu wa maadili, kitendo ambacho kingeweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Kafulila alipandishwa kizimbani jana mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo, George Buyamba, na kusomewa mashitaka hayo.

Hata hivyo, Kafulila alikana mashtaka hayo na yuko nje kwa dhamana ya mdhamini mmoja mwenye barua ya utambulisho kutoka kwa Ofisa Mtendaji wa Kata na mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh. 500,000.

Upande wa Mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali Raymond Kimbe alidai mahakamani hapo kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa kwa ajili ya kumsomea maelezo ya awali.

Hakimu Buyamba alikubaliana na ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi Febuari 18, mwaka huu.

Kafulila anadaiwa kutoa lugha ya matusi Agosti Mosi, 2013 katika Kata ya Nguruka eneo la Nyumba ya Wageni ya Wilaya ya Uvinza, dhidi ya Hadija.

Mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo jana ya saa tatu asubuhi akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi na umati mkubwa wa watu pamoja na viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa, wapambe wake na madiwani wa vyama mbalimbali vya siasa.

Awali, kesi hiyo yenye namba 6/2015 ilifutwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa wa Kigoma, Slivester Kainda, baada ya upande wa mashtaka kushindwa kupeleka mashahidi mahakamani zaidi ya siku 60.

Baada ya Hakimu Kainda kufuta kesi hiyo, DPP ameirudisha tena mahakamani hapo na kusomwa tena kwa mara ya pili.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Jamaa ni 'political thug'. Arudi shuleni.