ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, January 14, 2016

Karume pasua kichwa CCM.

Sakata la kutaka Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk. Amani Abeid Karume, avuliwe uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa madai amekuwa akishirikiana na wapinzani, sasa linaelekea kukipasua kichwa chama hicho kikongwe nchini.

Hoja ya kumvua uanachama wa CCM Dk. Karume ilitolewa na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM), Sadif Khamis Juma, alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara wa kuadhimisha miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar katika uwanja wa Maisara mwishoni mwa wiki.

Akizungumza na Nipashe jana visiwani humu, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alisema hoja ya kutaka kumjadili na kumfukuza uanachama Dk. Karume, bado haijawiva.

Vuai alisema kuwa CCM ina taratibu zake katika kuwajadili wanachama wake wanaokwenda kinyume na miiko na maadili ya chama hicho kabla ya kufikia hatua ya kutoa maamuzi.

Alisema Chama hakiwezi kujadili mwanachama wake kabla ya kupokea malalamiko kutoka katika tawi la mwanachama ama jumuiya na mhusika kupewa nafasi ya kujitetea.

Aliongeza kuwa CCM inafanya kazi kwa kufuata Katiba na taratibu za Chama na haiwezi kumjadili mtu kwa pupa au jazba.

“Kama wahusika wataleta malalamiko yao, lazima wathibitishe tuhuma zao na mhusika apewe nafasi ya kujitetea kupitia vikao vya Chama,” alisisitiza Vuai.

Aidha, alisema kuwa malalamiko ya mwanachama kuvunja miiko na maadili, yanatakiwa kujadiliwa katika vikao vya Chama na si mkutano wa hadhara.

“Suala hilo bado halijaiva na huwezi kumjadili mwanachama kabla ya kupokea malalamiko rasmi na mhusika kupewa nafasi ya kujitetea,” aliongeza Vuai.

Hata hivyo, akihojiwa na Nipashe mjini hapa jana kuhusu shutuma zilizotolewa na UVCCM dhidi yake, Rais mstaafu Dk. Karume alikataa kuzungumza chochote.

“Sadallah (jina la mwandishi wetu), unataka nini kuhusu jambo hilo? Waulizeni wenyewe waliosema,” alijibu kwa kifupi Dk. Karume.

Wakati hayo yakitokea, Chama cha Wananchi (CUF) Zanzibar, kimekanusha kuwa hakina ushirikiano na Dk. Karume wa kuihujumu CCM Zanzibar.

Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Omar Ali Shehe, alisema chama chake kimekuwa kikimpa heshima kubwa Dk. Karume kama kiongozi mstaafu na mtu aliyefanya kazi kubwa ya kuwaunganisha Wazanzibari kupitia maridhiano yaliyozaa Serikali ya Umoja wa Kitaifa mwaka 2009.

“Tunamheshimu Karume kama kiongozi aliyeongoza nchi na mtu aliyefanya kazi kubwa ya kuwaunganisha Wazanzibari yeye na Maalim Seif Sharif Hamad,” alisema Shehe.

Alisema CUF haihitaji msaada wa kisiasa kutoka chama chochote kutokana na nguvu zake za kisiasa kujitosheleza kufikia malengo ya kuleta mabadiliko ya utawala visiwani Zanzibar.

Alisema bahati mbaya baadhi ya watu hawapendi kuona Wazanzibari wakiwa kitu kimoja baada ya maridhiano kufanikiwa kuimarisha hali ya amani na mshikamano kwa wananchi wake.

Alisema kimsingi CCM imeshindwa kusimamia misingi na malengo ya Mapinduzi na kupoteza nguvu za kisiasa na kuanza kufikiria kufukuza wanachama wake kama ilivyotokea kwa Waziri wa zamani, Mansoor Yussuf Himid na mwanasiasa mkongwe visiwani humu, Hassan Nassor Moyo.

Hata hivyo, alitahadharisha kuwa kama CCM watamfukuza Dk. Karume, basi huo ndiyo utakuwa mwisho wao wa kisiasa duniani kwa sababu kitendo hicho ni sawa na binadamu kumkata miguu.

Wakati akihutubia katika mkutano wa hadhara wa kuadhimisha miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar katika uwanja wa Maisara, Mwenyekiti wa UVCCM, Sadif Khamis Juma, alisema wakati umefika kwa Dk. Karume kufukuzwa katika Chama kwa madai kwamba anashirikiana na wapinzani kuizorotesha CCM.

Alidai kuwa kwa muda mrefu Dk. Karume amekuwa na ajenda za kuwasadia wapinzani kisiasa badala ya chama chake, kitendo alichokieleza kuwa ni kwenda kinyume na miiko na maadili ya chama hicho.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

CCM ZANZIBAR KILICHABAKIA NI KUNYANYUA MIKONO, KILICHOBAKIA NI KUTAPATAP....
MNAANZA KUBAGUANA WENYEWE KWA WENYEWE NA KUFUKUZANA, NANI ATAKAE BAKIA SALAMA KATIKA CCM ZANZIBAR?