Zanzibar. Siku moja baada ya mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC) kuitangaza Machi 20 kuwa siku ya marudio ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar, mgombea urais, Maalim Seif Sharif Hamad na Edward Lowassa leo wanakutana na wabunge wote kutoka vyama vinavyounda Ukawa kutoa “tamko zito” litakalotoa mwelekeo wa hali halisi ya kisiasa visiwani humo.
CUF, ambayo inapinga kurudiwa huko kwa uchaguzi, nayo imepanga kufanya vikao vyake vya juu mapema wiki ijayo kuweka msimamo wake kuhusu tangazo hilo.
Wakati hayo yakiendelea, mabomu ya machozi jana yalilipuliwa kwenye maeneo tofauti ya Zanzibar wakati askari wa Jeshi la Polisi wakitawanya watu waliokuwa wamekaa kwenye vikundi, kwa kuhofia kuwa wanaweza kutumia mwanya huo kufanya vurugu.
Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha alitangaza juzi kuwa marudio ya uchaguzi hayatatanguliwa na kampeni za wagombea wa nafasi za urais, uwakilishi na udiwani na wala hakutakuwa na mabadiliko yoyote ya wagombea.
Bado vyama vya upinzani havijatoa tamko kuhusu uamuzi huo wa ZEC, lakini viongozi wa vyama vinavyounda Ukawa; Chadema, CUF, NLD na NCCR Mageuzi wanatarajiwa kuhudhuria kikao hicho kitakachofanyika kwenye Ukumbi wa African Dream.
Habari zilizolifikia gazeti zinaeleza kuwa awali katika kikao hicho Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ulipanga kujadili mkwamo wa kisiasa na jinsi ya kupata suluhu, lakini baada ya ZEC kutangazaa kurudiwa kwa uchaguzi huo, ajenda imebadilika na sasa umoja huo utatoa msimamo wake wa mwisho kuhusu Zanzibar.
Msemaji wa Lowassa, Aboubakar Liongo na Ismail Jussa walithibitisha viongozi hao kutua Dodoma jana jioni tayari kwa kikao hicho ambacho kitaanza asubuhi.
Habari zaidi zinaeleza kuwa awali, Maalim Seif na Lowassa, ambaye alikuwa Waziri Mkuu na ambaye mwaka jana aligombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chadema, watakutana na viongozi wakuu wa Ukawa na baadaye na wabunge wote na kisha kutoa maazimio.
“Ni maazimio ambayo yanalenga kueleza ukweli kuhusu kinachotaka kufanyika Zanzibar. Yatakuwa maazimio mazito,” alisema mpashaji habari wetu.
Januari 20, wabunge wa Ukawa walifanya kikao cha ndani kwenye ukumbi wa Pius Msekwa uliopo viwanja vya Bunge kuhusu hali ya kisiasa visiwani Zanzibar na kutangaziwa kuwa wataelezwa msimamo wa umoja huo leo.
“Watapewa mrejesho wa kikao cha mwisho kati ya Maalim Seif na (Rais wa Zanzibar) Dk Ali Mohamed Shein. (Mwenyekiti wa Chadema, Freeman) Mbowe na mwanasheria wa Chadema (Tundu Lissu) nao wataeleza masuala mbalimbali kuhusu Zanzibar,” alisema mtoaji habari huyo ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema licha ya kuwapo kwa mazungumzo hayo, msimamo wa Ukawa na CUF wa kupinga uchaguzi huo kurudiwa, upo palepale.
“Kesho (leo) tunazungumza kuhusu Zanzibar. Pamoja na mambo mengine tutatafakari hali ya kisiasa visiwani Zanzibar na nchi kwa ujumla na baada ya hapo tutatoa maazimio yetu,” alisema Mbatia.
Alisema lengo la kikao hicho ni kuelezana kwa kina lilipo tatizo, kupewa taarifa na takwimu sahihi.
“Hatuko tayari kurudiwa kwa uchaguzi Zanzibar, Watanzania lazima wakumbuke kuwa ukitenda haki, amani ndipo hupatikana,” alisema.
Alisema kutokana na kufutwa kwa uchaguzi huo, Tanzania imetengwa pamoja na kunyimwa fedha za maendeleo kutoka mataifa makubwa.
“Ole wao wanaofanya mambo haya. Yakisababisha umwagaji damu yatawagharimu na wapo watakaokamatwa na kufikishwa Mahakama ya Kimataifa kwa kusababisha mauaji,” alisema Mbatia.
“Suala la Zanzibar hatukubaliani nalo kwa sababu ukishawekwa utaratibu, halafu ukauvuruga ni fujo. Na duniani kote dola na taasisi huundwa kwa njia ya maridhiano,” alisema.
“Mwaka 1995 na 2000 mauaji yalitokea Zanzibar lakini mwaka 2010 hayakutokea kwa sababu ya maridhiano ya CCM na CUF.
“Leo hii Zanzibar wanarudi kulekule kwa kuwa CCM wasiposhinda inakuwa nongwa. Wanataka wao ndiyo washinde tu na wanadhani wao ndiyo wenye fikra na haki tu. Kama ni hivyo kwa nini mfumo wa demokrasia uwepo?”
Wakati mkutano huo ukiandaliwa, Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa Umma wa CUF, Jussa, ambaye amelielezea tamko la Jecha kuwa halizingatii Katiba wala sheria.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Jussa amelielezea tamko hilo kuwa “la kihuni lisilozingatia Katiba wala sheria” na kwamba vikao vya juu vya chama hicho vitafanyika mapema wiki ijayo kufanya uamuzi.
“Kamati ya Utendaji ya Taifa itakutana tarehe 27 Januari, 2016 na kufuatiwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa litakalokutana Alhamisi, tarehe 28 Januari, 2016,” inaeleza taarifa hiyo iliyotolewa na Jussa akiongeza kuwa vikao hivyo vitafanyika kwenye ofisi za makao makuu ya CUF zilizopo Buguruni jijini Dar es Salaam.
Taarifa hiyo inawataka wananchi ambao kinasema “waliikataa CCM kwa kishindo Oktoba 25”, kuendelea kutunza amani na kuwa watulivu “katika kipindi hiki kigumu na kusubiri maamuzi ya chama chao wanachokiamini”.
Akitangaza tarehe ya kurudia uchaguzi huo juzi kupitia kituo cha televisheni cha Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) ambako pia Januari 28, 2015 alitangaza kuufuta, Jussa alisema kulikuwa na ukiukwaji wa sheria na kanuni za uchaguzi.
Alisema uchaguzi huo utarudiwa ndani ya siku 90. Juhudi za kutafuta suluhisho la kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi huo zilizomshirikisha Dk Shein na Maalim Seif zimegonga mwamba baada ya kufanya vikao tisa bila kuafikiana.
Tayari Maalim Seif ameshajitoa kwenye mazungumzo hayo yaliyohusisha vikao tisa.
Mitaani Zanzibar
Mapema jana hali ilikuwa shwari mitaani wakati watu wakiendelea na shughuli zao za kila siku, lakini ilibadilika jioni wakati polisi walipotumia mabomu ya machozi kutawanya watu waliokuwa wamekusanyika nje ya nyumba zao wakinywa kahawa kwa maelezo kuwa mikusanyiko hairuhusiwi.
Maeneo hayo ni pamoja na Kundemba, Kwa Haji Tumbo na Kinuni na watu kadhaa wanadaiwa kupigwa kabla ya kutawanywa.
Wakizungumza na gazeti hili, mashuhuda wa tukio hilo walisema hakukuwa na sababu yoyote ya polisi kufanya jambo hilo kwa kuwa ni kawaida vijana na wazee kukusanyika maeneo hayo kwa ajili ya kunywa kahawa na kucheza keramu.
Eneo la Haji Tumbo, kijana mmoja alitolewa ndani ya duka la simu na kupigwa kisha polisi kuondoka naye pamoja na pikipiki yake aina ya Vespa.
“Wamekuja wakaingia kwenye duka la simu kwanza wakapiga mabomu kama mlivyosikia ule mlio, kisha wakamchukua. Lakini kwanza wamempiga,” alisema Mahmoud Ali, mkazi wa eneo hilo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mukadam Khamis Mkadam hakupatikana jana kuzungumzia suala hilo.
Imeandikwa na; Fidelis Butahe, Hassan Ali, Kalunde Jamal na Salma Said
Mwananchi
1 comment:
Acheni kuzungusha! Mpeni ushindi wake Maalimu seif basi.
Post a Comment