ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, January 2, 2016

MAADHIMISHO YA SHEREHE ZA MIAKA 52 YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR YAPO PALE PALE, ASISITIZA BALOZI SEIF

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya maadhimisho ya Kitaifa Zanzibar akitoa Taarifa rasmi ya Maadhimisho ya Sherehe za kutimia Mikaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa Wanahabari. Kushoto ya Balozi Seif ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Ahmad Kassim na Mkurugenzi wa Idara ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa Nd. Ameif Ussi.

Wanahabari wa Vyombo mbali mbali wakimsikiliza kwa makini Balozi Seif akitoa Taarifa rasmi ya maadhimisho ya Sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar kutimia Miaka 52.

Wapiga picha wa vyombo mbali mbali vya Habari wakiendelea kuchukuwa matukio kwenye mkutano wa Waandishi na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi Seif ambae pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Maadhimisho ya Kitaifa Zanzibar akisisitiza jambo mbele ya Waandishi wa Habari wakati akijibu baadhi ya maswali aliyoulizwa. Picha na – OMPR – ZNZ.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Maadhimisho ya Sherehe za kutimia Miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 yatafanyika kama kawaida na kupangwa kuanza rasmi kesho jumapili ya Tarehe 3 Januri 2016.
Alisema Serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha kwamba katika muda wote wa maandamisho hayo kunakuwa na hali ya utulivu na usalama mkubwa katika maeneo yote ya Visiwa vya vya Unguja na Pemba.
Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Maadhimisho ya Kitaifa Zanzibar alisema hayo wakati akitoa Taarifa rasmi ya ratiba ya maadhimisho ya sherehe za Miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar mbele ya Wana Habari hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Alisema suala la upande wa Upinzani kuzisusia sherehe za Mapinduzi kwa kisingizio cha Rais aliyepo madarakani si halali ni muendelezo wa kuwapotosha Wananchi walio wengi nchini.
Balozi Seif alifafanua kuwa Rais wa sasa Dr. Ali Mohammed Shein ataendelea kuwa rais hadi yule atakayechaguliwa rasmi na kihalali na Wananchi ale kiapo kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kama ilivyokwishatolewa ufafanuzi na wanasheria walio wengi.
Alisema tukio hili la maadhimisho ya sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar kutimia miaka 52 ni jambo la kujivunia kwa kila Mwananchi wa Visiwa vya Unguja na Pemba mpenda maendeleo na anayeifahamu vyema Historia ya Zanzibar kabla na baada ya Mapinduzi.
Alieleza kwamba ipo miradi mingi na tofauti ya Wananchi ambayo Viongozi na hata baadhi ya wanachama wa upande wa upinzani walishiriki kuibuni sasa inakuaje miradi hiyo waiachie wakati tayari imeshalengwa kuinufaisha jamii iliyowazunguuka.


“ Tuna kila sababu na ni haki yetu kusherehekea siku hii adhimu katika Maisha yetu. Hivyo tuambizane, tushajiishane na tushiriki katika matukio mbali mbali ya maadhimisho ya sherehe hizi kuanzia mwanzo hadi mwisho “. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba Miradi yote ya Maendeleo ipatayo 24 ambapo 16 ikiwa imekamilika na Minane inatarajiwa kuwekwa mawe ya msingi imehusishwa katika maadhimisho hayo itakayoanza Jumatatu ijayo.
Alisema madhimisho hayo yataanza rasmi kesho Jumapili ikiwa ni siku maalum kwa kazi za usafishaji wa masingira katika maeneo mbali mbali Unguja na Pemba ukilenga zaidi katika sehemu za kutolea huduma za kijamii kama Hospitali, Vituo vya Afya pamoja na masoko.
Mwenyekiti huyo wa Halmashauri ya Maadhimisho ya Kitaifa Zanzibar alifahamisha kwamba ingawa zoezi hilo hufanyika kila zinaponza sherehe za Mapinduzi lakini mwaka huu juhudi malum zinapaswa kuchukuliwa ili kuhakikisha maeneo yote yanakuwa katika hali ya usafi muda wote.
Alikumbusha kuwa hivi sasa Taifa linakabiliwa na tatizo la kuwepo kwa maradhi ya Kipindupindu, hivyo jamii ina wajibu wa kutumia fursa hizi za maadhimisho ya sherehe za Mapinduzi kwa kuchukuwa hatua za kujikinga na kupambana na maradhi hayo ambayo kwa kiasi kikubwa husababishwa na mazingira machafu ya sehemu zinazotumika na jamii katika shughuli za kila siku.
Alisema kwa vile suala la usafi wa mazingira ni la lazima Viongozi Wakuu wa Kitaifa watahakikisha wanaungana na Wananchi katika zoezi hilo kwenye maeneo watakayopangiwa.
Alieleza kwamba utaratibu maalum umeshaandaliwa kwa kila mamlaka za Mikoa, Wilaya, Baraza la Manispaa, Mabaraza ya Miji na Halmashauri za Wilaya katika kuratibu mfumo mzima wa kufanikisha zoezi hilo la usafi wa mazingira. 
Akigusia suala la hatma ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar ambalo limekuwa agenda kubwa kwa baadhi ya watu wakiwemo hata wanasiasa nchini wakiendelea kupotosha Wananchi Balozi Seif alisema Taarifa rasmi ya vikao vinavyowakutanisha Viongozi wa juu kulijadili suala hilo itatolewa rasmi mara baada ya kukamilika kwa mazungumzo hayo.
Hata hivyo Balozi Seif alitanabahisha kwamba Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar { ZEC } kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ndio yenye mamlaka ya kuendesha na kusimamia uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.
Alisema kwa vile tume hiyo kupitia Mwenyekiti wake haikuridhika na mazingira yaliyojichomoza wakati wa zoezi la kupiga kura na kulazimika kufuta Uchaguzi pamoja na matokeo yake yote Taasisi hiyo hiyo ndio yenye uwezo wa kuitisha uchaguzi mwengine kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar.
Akijibu baadhi ya maswali ya Waandishi wa Habari Balozi Seif alisema katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984 iko wazi na kutoa mamlaka kwa tume ya uchaguzi ya Zanzibar kupanga uchaguzi mwengine kufuatia kufutwa kwa ule wa mwezi oktoba mwaka 2015.
“ Kinachosubiriwa kwa sasa ni Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kutangaza Tarehe ya uchaguzi mwengine ambapo kujumu la kugharamia uchaguzi huo limo ndani ya mamlaka ya Serikali Kuu yenyewe “. Alisema Balozi Seif.
Kuhusu Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ambao baadhi ya watu wamekuwa wakitoa tafsiri potofu, Balozi Seif aliwajibu wanahabari hao kwamba Baraza la Wawakilishi lilivunjwa lakini Rais wa Zanzibar bado anayo Mamlaka ya kuliitisha iwapo kuna suala muhimu la Kitaifa.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

No comments: