Wednesday, January 13, 2016

Magufuli kiboko.

Wakati, Rais John Magufuli, akifikisha siku ya 70 ofisini leo tangu kuapishwa kwake Novemba tano mwaka jana, gazeti hili limebaini kuwa mpaka sasa amepanda ndege mara moja tu na kutoka nje ya jiji la Dar es Salaam mara mbili tu.

Taarifa hizo ambazo zilithibitishwa na mmoja wa wasaidizi wa Rais Magufuli, zinaeleza kwamba, jana ndiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kupanda ndege tangu aingie madarakani.

Katika safari yake ya jana, Rais Magufuli alitumia ndege kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar kuhudhuria sherehe za maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi ya visiwa hivyo.

Kwa mujibu wa kikokotozi cha mtandaoni (Distance calculator), umbali wa kutoka Dar es Salaam mpaka Zanzibar ni kilomita 73.43.
Muda wa kutoka Dar es Salaam kwa ndege kwenda Zanzibar, kikokotozi hicho kinaonyesha ni dakika 14 mpaka dakika 20 kutegemea na ukubwa wa ndege na mwende kasi inayotumia.

Jana Rais Magufuli alikuwa miongoni mwa viongozi wa kitaifa waliokuwapo kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar kuuungana na Rais Ali Mohamed Shein katika kusherehekea kilele cha maadhimisho ya sherehe za Mapinduzi.

Wengine waliokuwapo ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan; Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa; marais wastaafu wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete na Rais Mstaafu wa Zanzibar, Abeid Amaan Karume.

Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa, safari iliyomtoa Rais Magufuli kutoka Magogoni, Ikulu jijini Dar es Salaam hadi Zanzibar ni ya pili tangu alipoapishwa Novemba 5, 2015 baada ya kushinda kwa asilimia 58.46 ya kura halali zilizopigwa katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.

Mbali na safari hiyo, safari nyingine ni ile aliyotumia usafiri wa barabara kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma kufungua Bunge la 11 na kupendekeza jina la Waziri Mkuu.

Katika safari hiyo ya Dodoma ambako ndipo makao makuu ya nchi na kuliko na Ikulu ya pili kwa ukubwa ya Chamwino ukitoa ile ya Magogoni, Rais Magufuli baada ya kuzindua Bunge Novemba 20, 2015 alikaa kwa siku kadhaa kabla ya kurejea Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa kikokotozi cha umbali, kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma ni kilomita 583.64 ambazo kwa gari linalotembea wastani wa mwendo kasi wa kilomita 112 kwa saa, litatumia saa tano na dakika 12 kumaliza safari hiyo.

Wakati leo akifikisha siku ya 70 ofisini, Rais Magufuli hajawahi kusafiri nje ya nchi na mara kadhaa amekuwa akitimiza ahadi yake ya kuhakikisha kuwa mabalozi wa Tanzania katika nje ya nchi wanaliwakilisha taifa kwenye baadhi ya mikutano ili kuondokana na gharama zinazoepukika.

“Lazima tukubaliane kuwa katika kubana matumizi kuna faida na hasara zake, ndiyo maana hata kutosafiri kwake kutakuwa na faida nyingi lakini kunaweza kuwa na hasara kidogo. Ila lazima tu tukubaliane ukitaka kwenda mbiguni lazima kwanza ufe, vivyo hivyo ukitaka kubana matumizi kutakuwa na hasara zake,” alisema mmoja wa wasaidizi wa kiongozi huyo.

Wakati akizindua Bunge, Rais Magufuli alisema safari za nje zimeligharimu taifa Sh. bilioni 356.3, ambazo kati yake Sh. bilioni 183.1 zilikuwa kwa ajili ya tiketi za ndege, Sh. bilioni 68.6 ziligharamikia mafunzo na Sh. bilioni 104.5 zilikuwa za posho.

Rais Magufuli ambaye amebana safari za nje za watumishi wa umma, aliliambia Bunge kwamba, fedha hizo zingeweza kujenga kilometa 400 za barabara ya lami.

Licha ya safari hizo za kikazi, Rais Magufuli pia alisafiri kutoka Dar es Salaam hadi Msoga, mkoani Pwani kwenye msiba wa dada wa Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete.

Mpaka sasa, licha ya watumishi wengi wa serikali kuomba kusafiri nje ya nchi na kunyimwa kibali, serikali imewasimamisha kazi watumishi wanne wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), kwa kwenda nje ya nchi bila kibali maalumu cha Ikulu.

Itakumbukwa pia kuwa, mpango wa Rais Magufuli wa kubana matumizi, ulifanya utaratibu wa kusherehe siku ya Uhuru ibadilishwe na watu kuadhimisha siku hiyo kwa kufanya usafi badala ya kwenda uwanja wa taifa kuangalia gwaride na halaiki ambayo huwa inagharimu mabilioni.

Kutokana na kuahirishwa kwa shamrashamra hizo, Sh. bilioni nne zilizookolewa na kuelekezwa kwenye utanuzi wa barabara ya Bagamoyo eneo la Mwenge mpaka Morocco ambako kazi hiyo inaendelea kwa sasa.

Mpango huo wa kubana matumizi ya serikali, pia ulifanya sherehe ya kufungua Bunge ifutwe na fedha zake kuelekezwa kununua vitanda vya wagonjwa kwa ajili ya Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Hatua ya Rais Magufuli kutosafiri mara kwa mara huku pia serikali yake ikidhibiti safari za nje kwa viongozi na watumishi wote wa serikali imekuwa ikiwavutia watu wengi nchini na kwingineko nje ya Tanzania, akiwamo mgombea urais wa upinzani nchini Uganda, Dk. Kizza Besigye.

Katika moja ya mikutano yake ya kampeni akiwa kwenye wilaya ya Agago, nchini humo, Besigye alisema akiingia Ikulu atafuata nyayo za Rais Magufuli kwa kupiga marufuku safari holela za nje ya nchi na kuongeza kuwa ataiuza ndege anayoitumia mpinzani wake, Rais Yoweri Museveni, aina ya Gulfstream V Jet.

Licha ya rekodi ya Rais Magufuli ya kutosafiri kwenda Ulaya na nchi nyingine za nje ya Tanzania hata mara moja tangu aingie madarakani kuwavutia wengi, baadhi ya watu waliozungumza na Nipashe wamedai kuwa hali hiyo ni balaa kubwa la kiuchumi kwa wasaidizi wa Rais ambao wengi wangetamani asafiri zaidi kama ilivyo kwa wakuu wengine wengi wa nchi za Kiafrika waingiapo madarakani.

Kutokana na rekodi ya safari za Magufuli, ni wazi kuwa hadi sasa, wasaidizi wa Rais huyo wa awamu ya tano watakuwa wamehusika katika safari za kutoka jijini Dar es Salaam kuelekea kwenye Ikulu ndogo ya Chamwino, Dodoma na Unguja visiwani Zanzibar alikokuwa jana.

“Rais yeyote anaposafiri ni lazima aambatane na timu ya watu kadhaa wa karibu yake. Kama Rais anasafiri mara kwa mara, ni wazi kwamba hawa pia hunufaika kwa safari hizi ambazo huambatana na posho nzuri za safari. Hata hivyo, kwa hawa (wasaidizi) wa Rais Magufuli hali iko tofauti… Rais amesafiri mara chache na hivyo wao pia watakuwa wameguswa na ratiba hiyo kwa kusafiri mara chache,” chanzo kimoja kiliiambia Nipashe jana kuhusiana na safari za Rais.

SAFARI ALIZOJIKOSESHA MAGUFULI
Pengine katika kutekeleza agizo alilolitoa la kudhibiti safari za nje, Rais Magufuli hakusafiri kwenda kwenye mkutano wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Madola (CHOGM) uliofanyika visiwa vya Malta Novemba 27, mwaka jana.

Badala yake, Rais Magufuli alimtuma Balozi wa Tanzania nchini Uingereza kwenda kumwakilisha katika mkutano huo, akiwa pamoja na maofisa wengine watatu na hivyo jumla yao kuwa watu wanne. Inaelezwa kuwa wakati wa utawala wa awamu ya nne, msafara kwenye mkutano kama huo uliofanyika Malta ulikuwa ukimhusisha Rais, baadhi ya mawaziri na maafisa wengine wa juu serikalini ambao kwa ujumla walikuwa takribani 50.

Novemba 29, mwaka jana, Rais Magufuli alitakiwa kuwapo jijini Paris, Ufaransa katika mkutano wa kimataifa wa 21 kujadili mabadiliko ya tabianchi duniani (COP21) ambapo wakuu wa nchi takriban 150 kutoka katika nchi 195 walishiriki, wakiwamo marais Barack Obama wa Marekani na Xi Jinping wa China. Hata hivyo, hakukwea ndege kwenda kuhudhuria mkutano huo na badala yake akabaki nyumbani akiendelea kushughulikia ‘upasuaji majipu’, hasa Mamlaka ya Bandari (TPA) na Mamlaka ya Bandari (TRA).


Desemba 5, 2015, Rais Magufuli hakupanda ndege pia kwenda Johannesburg, Afrika Kusini kulikokuwa na mkutano wa tano wa wakuu wa nchi za Afrika na Rais wa China, Xi Jinping, kupitia Jukwaa la Nchi za Afrika na China (FOCAC). Katika mkutano huo, Rais Magufuli aliwakilishwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu.
CHANZO: NIPASHE

5 comments:

Anonymous said...

Hali ya uchumi iko pale pale. Wananchi acheni ushabiki.

Anonymous said...

WAACHE VIGELEGELE KAMA WANAVYOAMBIWA

Anonymous said...

Kama wanavyosema wakenya magufuli is the real deal. Na ni deal kweli si mchezo kwani uwezekano wa kimabadiliko ya kiutawala na uendashaji wa nchi za east Africa ni mkubwa kutokana na ushawishi wa utendaji kazi mzuri wa magufuli. Future ya Tanzania chini ya uongozi wa Dk Magufuli ni yenye kuleta matumaini makubwa katika nyanja za maendeleo.

Anonymous said...

Tanzania chini ya magufuri inawezekana, hata hizo nchi zilizoendelea zilianza hivi hivi kama huu mfumo unaoendeshwa na mueshimiwa raisi, na maendeleo uenda pole pole kwa kurekebisha nyanja mbali mbali

Anonymous said...

Kweli magufuli ni poa. Lkn haki iwe sawa kwa watanzania wote. Mungu ibariki Tanzania