Kwa mujibu wa wabunge wa upinzani, watalazimika kutumia mwanya wa kuomba mwongozo wa kiti cha spika na maswali ya papo kwa papo kwa waziri mkuu kuwasilisha hoja zao.
Hata kwa wale ambao watachangia hotuba ya Rais Magufuli, wengi watajikita kujadili kasoro za serikali zilizoonyeshwa na yale ambayo yanaonekana ni magumu kutekelezeka.
Akizungumza jana na waandishi wa habari mjini hapa, kuhusu ratiba ya mkutano huo wa bunge, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Bungeni, Owen Mwandumbya, alisema mkutano utaanza leo na kumalizika Februari 5, mwaka huu ukiwa na shughuli za kujadili hotuba ya rais, kujadili na kuridhia Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano na Bunge kukaa kama Kamati ya Mipango.
Mbali na shughuli hizo, alisema kutakuwa na kiapo cha uaminifu kwa wabunge 11, ambao wamechaguliwa na wengine kuteuliwa na rais mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa kwanza wa bunge.
Mwandumbya alisema katika mkutano huo, jumla ya maswali ya msingi ya kawaida 125, yanategemewa kuulizwa na kujibiwa.
"Chini ya Kanuni ya 38(1) ya Kanuni za Bunge, Toleo la Januari 2016, utaratibu wa kumuuliza waziri mkuu maswali ya papo kwa papo kila Alhamisi utaendelea. Hivyo kwa kufuata uzoefu, inakadiriwa kuwa maswali ya msingi 16 yataulizwa na kujibiwa na waziri mkuu," alisema Mwandumbya.
Aidha, alisema kutakuwa na shughuli za chaguzi mbalimbali za kuwapata viongozi wa bunge na wawakilishi wa bunge katika vyombo na taasisi mbalimbali.
Alifafanua kuwa, leo utafanyika uchaguzi wa wenyeviti watatu wa bunge na kwamba juzi Kamati ya Uongozi ilipendekeza majina ya wabunge watatu ambao ni Najma Giga, Andrew Chenge na Mary Mwanjelwa kuwania uenyekiti huo.
Mbali na uchaguzi huo pia kutakuwa na uchaguzi wa wajumbe saba wa Tume ya Utumishi wa Bunge, wajumbe watano wa Bunge la Afrika (PAP), wajumbe watano wa Jukwaa la Wabunge wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-PF), Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na wajumbe 12 wa Kamati ya Utendaji wa Bunge la Jumuiya ya Madola (CPA) pamoja na wajumbe watano wa Umoja wa Mabunge duniani (IPU).
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mbunge wa Viti Maalum, Rose Kamili (Chadema), alisema kwa sasa wanaangalia suala la Zanzibar na hatma yake.
Naye Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche(Chadema), alisema kabla ya kuanza kujadili mpango wa maendeleo ya taifa, watahakikisha bunge linajadili hali ya kisiasa Zanzibar kwa sababu mpango unajumuisha na Zanzibar na ni kwa Watanzania.
Alisema katika kujadili hotuba ya rais na mpango huo, lazima serikali iseme wamefikia wapi kuhusu suala la Escrow kwa watu waliochukua fedha kwa magunia katika benki ya Stanbic ili wajulikane ni akina nani.
"Katika mpango wa miaka mitano ambao tumeuona, Janeth Mbene ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, amekiri serikali ilifanya makosa kubinafsisha viwanda, hivyo serikali inatakiwa ikiri kuwa ilifanya makosa kuuza nyumba hizo.
"Kwenye mpango huu, wamezungumza kupunguza matumizi ya serikali wakati majaji, makatibu wakuu na wakuu wa idara mbalimbali wanakaa kwenye mahoteli Dar es salaam,"alisema Heche.
Alisema lazima serikali ikiri pia katika hilo, na kwamba mpango huo umejaa takwimu za uongo, huku akitolea mfano upatikanaji wa maji ambao alisema mpango uliweka wazi kuwa unasema maji yamepatikana kwa asilimia 68 wakati hata katika jimbo lake hakuna huduma hiyo.
"Maji hayapo kule, hizi ni takwimu za uongo za kupika, hakuna kitu kilichofanyika, hizo asilimia 68 wamezitoa wapi? Haya kwenye afya juu ya kupunguza vifo vya akina mama na watoto, sera ya afya inasema kila kata kutakuwa na zahanati na kituo cha afya lakini kwenye jimbo langu lenye kata 26, tatu tu ndio zina vituo vya afya, vijiji vingi havina zahanati, nadhani ni mambo ambayo yataibuka katika kujadili huu mpango,"alisema Heche.
Alisema ukizungumzia kipindupindu, ni dalili kuwa bado hakuna maji safi na salama, hivyo mpango kama unasema uongo haiwezekani kujadili kwenda mbele, lazima useme ukweli kwa takwimu halisi.
Naye Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Upendo Pendeza, alisema kwanza watataka serikali iseme ni kwa vipi itashirikisha sekta binafsi katika kuhakikisha uwekezaji wa viwanda unakuwa na tija.
"Kwenye hotuba yake rais, alisema mambo ya viwanda, lakini ukiangalia kwenye maeneo mengi wanazungumzia kuacha suala hilo kwa sekta binafsi, kwa hiyo sisi tunataka aeleze vizuri kwa namna watakavyoshiriki kwenye suala la viwanda na ajira ziongezeke kwa vijana," alisema Pendeza.
Mbunge wa Mtera Livingston Lusinde (CCM), alisema ataibua suala la Bandari Kavu Dodoma.
Pia, alisema takwimu ambazo serikali imewasilisha bungeni juu ya maji vijijini kupitia mpango wa maendeleo ya awamu ya pili hazipo sahihi kwa hiyo ataitaka serikali iwasilishe majina ya vijiji vilivyopata maji.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment