Thursday, January 14, 2016

Nape aitaka Chadema imtimue Lowassa




Mwananchi
Dar es Salaam. CCM imemjibu mwanasheria Mkuu wa Chadema ikisema ili chama hicho kikuu cha upinzani kionekane kinapambana na ufisadi kwa vitendo, kinatakiwa kumuunga mkono Rais John Magufuli na kumvua uanachama Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, katibu wa itikadi na uenezi wa chama hicho tawala, Nape Nnauye alisema Chadema iliachana na ajenda ya kupambana na ufisadi baada ya kumpokea Lowassa Julai mwaka jana baada ya jina lake kukatwa katika mchakato wa CCM kusaka mgombea wake wa urais.

“Sisi hatukumpitisha (Lowassa) awe mgombea wetu wa urais kwa sababu hiyo (ya ufisadi) na ndiyo maana yeye mwenyewe aliamua kuondoka na kwenda Chadema,” alisema Nape.

“Hata katika kampeni za uchaguzi mkuu, Chadema hawakuzungumzia ajenda ya ufisadi, ni kama Lowassa aliifunika tu.”

Alikuwa akimjibu Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu ambaye katika mahojiano maalum na Mwananchi juzi, alisema ufisadi ni ajenda ya kudumu ya chama hicho kwa kuwa Rais Magufuli hataweza kuufumua wote katika kipindi cha miaka mitano.

Huku akichelea kueleza kiundani sababu za CCM kutomfukuza Lowassa kwa tuhuma za ufisadi mpaka alipoamua kujiondoa na kujiunga na Chadema, alisema kauli ya Lissu inalenga kuwahadaa Watanzania.

“Kauli ya Lissu ni ya kushangaza sana. Sisi tunajua jinsi ambavyo Chadema na washirika wake walivyojitenga na ajenda ya ufisadi. Kama kweli wanaupinga, basi wamuunge mkono Rais Magufuli ambaye kwa sasa anapambana na ufisadi kwa kasi,” alisema mbunge huyo wa Mchinga.

“Wakati mwingine kila jambo hufanyika kwa wakati wake. Suala la kupinga ufisadi CCM lilianza siku nyingi tangu enzi za kujivua gamba. Tumeendelea nalo mpaka watu wakajiondoa wenyewe,” alisema Nape.

Alisema hoja ya kupinga ufisadi ndani ya CCM ilikibeba chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana na kikapata ushindi mnono, huku Chadema iliyokuwa ikilia na ufisadi ikishindwa.

“CCM tulieleza sababu za kutompitisha Lowassa kugombea urais na hilo lilikuwa wazi,” alisema.

Katika ufafanuzi wake wa juzi, Lissu alisema ili apambane na ufisadi, Rais Magufuli anapaswa kuacha tabia za CCM na kumtaka mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) amtangaze mshindi halali wa Uchaguzi Mkuu ambao Chadema wanaamini Maalim Seif Sharif Hamad alishinda.

Pia Lissu alimtaka Rais ataje majina ya waliokwepa kodi ili kama watajitokeza kuwania uongozi, wadhibitiwe kwa kuwa Katiba imezungumza kwa maneno makali dhidi ya vitendo hivyo viovu.

Aidha, aliponda uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo anayetajwa kuhusiska katika sakata la uchotwaji wa Sh3060 bilioni kutoka akaunti ya Tetega Escrow.

Miaka 39 ya CCM

Akizungumzia maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 39 ya kuzaliwa kwa CCM, Nnauye alisema uzinduzi utafanyika Januari 31, visiwani Zanzibar na mgeni rasmi atakuwa makamu mwenyekiti wa chama hicho na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein.

Alisema kilele cha maadhimisho hayo kitakuwa Februari 6, mjini Singida na yataongozwa na mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete ambaye aliiongoza Serikali ya Awamu ya Nne.

“Viongozi wa kitaifa na baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu watakaohudhuria maadhimisho haya watapangiwa shughuli za ujenzi wa chama na taifa katika wilaya zote za mkoa wa Singida, siku tatu kabla ya kilele cha maadhimisho,” alisema.

Alisema mikoa yote nchini inapaswa kuandaa shughuli hiyo wiki moja kabla ya maadhimisho, na kwamba lengo ni kufanya shughuli za ujenzi wa chama hicho katika maeneo yao.

“Tutakachokifanya wiki hiyo ni kupokea wanachama wapya, kufanya mikutano ya kuwashukuru wananchi kwa kuiamini CCM na kuichagua iendelee kuongoza, kuhamasisha wananchi kufanya kazi ili kujiletea maendeleo,” alisema.

7 comments:

Anonymous said...

Nape acha kuingilia maswala ya vyama vingine. Wewe sio msemaji na wala mwamuzi wa chama hicho. Unaharibu sana maswala chama!!

Anonymous said...

Uchaguzi umepita tumeona mafanikio na magumu yaliyopita kipimo. Mafisadi ni wengi na ufisadi wa EL hauonekani ila unasemwa midomoni tu. Waliokwepa kodi na washirika wa fedha mabilioni wametajwa na hakuna aliyechukuliwa hatua stahiki. Edward amejikalia kimya bado anakuwa gumzo kwa kitu kipi sasa. Kuwepo Chadema bado kunawaumiza CCM vivta. Huu sio muda wake mh. Nape. Fanyeni kazi za waTanzania ambazo ndizo alizozitaka EL bado tuna safari ndefu ya mabadiliko na sio ndani ya CCM bado!? Mh. JPM anaungwa mkono na itikadi na waTanzania wote kwa ujumla lakini bado anahitaji nguvu na yote hiyo ataipata Upinzani hasa CDM huko bungeni. Twende kazi tuache lalamiko ya kumfuata EL.

Anonymous said...

Mafisadi wamejaa ccm lkn hawaongelewi. Tunaomba msh. Magufuli uwaibue humo ndani kwa ndani. Piga kazi.

Anonymous said...

Kama waziri nape hakutakiwa kuja na story za kisiasa, hata Kama ni katibu uenezi CCM busara kwanza nadhani JPM pindi akipata uMWKT CCM nape atapigwa chini. Sidhani Kama elimu inamsaidia kitu huyu jamaa ni mtupu sana, ili ni tatizo la kusoma ukubwani bila kuingia darasani lakini anafaulu mitihani sababu ya hela zake.

Anonymous said...

Koma wewe nape hujafunga tu domo
Lako taarabu Na uwaziri vitu tofauti
Anza ccm kuliko kuingilia ya wengine ina kuhusu nini wewe Na ccm yako
Ya Zanzibar hamjamaliza mbona husemi
Mtoto ndogo hovyo

Anonymous said...

Have a sit and shut up Nape,

Anonymous said...

Nape badala ukae kimya. Acha kushededea. Ulikuwa out. Shukuru hilo bao la mkono. Yana mwisho.