Dar es Salaam. Baada ya kukamilisha uteuzi wa baraza la mawaziri na makatibu wakuu ulioingiza sura nyingi mpya, pangapangua hiyo sasa inawanyemelea mabalozi na maofisa wao wanaoiwakilisha Tanzania nje ya nchi.
Baada ya kuingia Ikulu, Rais John Magufuli alianza kupunguza gharama za uendeshaji Serikali kwa kupiga marufuku safari za nje kwa watumishi wa umma isipokuwa kwa kibali cha Ikulu, akitaka shughuli hizo zifanywe na kusimamiwa na mabalozi.
Magufuli pia aliamua siku ya Uhuru isherehekewe kwa kufanya usafi na fedha ambazo zingetumika kwenye sherehe hizo zielekezwe sehemu nyingine, na pia kupunguza gharama za sherehe za kupongeza wabunge na kiasi kilichobaki kilitumika kununulia vifaa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Kasi hiyo ya kupunguza gharama za uendeshaji Serikali, sasa inaelekea kuangaza kwenye balozi za Tanzania nje, ambako mbali na kupunguza watumishi na kubadilisha mabalozi, Serikali pia itataka kuwaondoa wale waliomaliza muda wao.
Kuna taarifa kuwa mabalozi wote wanaoiwakilisha Tanzania watapewa amri kurejea nyumbani wakisubiri uteuzi mpya, huku wengi wao wakistaafishwa.
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Augustine Mahiga alisema Rais Magufuli hajatoa maelekezo yoyote kuhusu suala la mabalozi japo wakati ukifika atafanya hivyo kulingana na mahitaji ya nchi. Alisema lengo la Serikali ni kuongeza ufanisi katika utendaji wake wa kazi kitaifa na kimataifa hivyo kuwapo kwa mabadiliko hakutaweza kuzuilika.
“Tunatakiwa kujipanga upya ili kuhakikisha kila mmoja anafanya kazi kwa bidii na kwa weledi kwenye nafasi aliyopewa. Nadhani tusubiri kwa sababu wakati ukifika Rais atatuelekeza nani anaenda wapi, anabaki au anastaafu, kinachoangaliwa zaidi ni kuongeza ufanisi,” alisema Balozi Mahiga.
Wasomi walonga
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI), Jimson Sanga alisema mabalozi walioshindwa kuiwakilisha Tanzania ipasavyo lazima matumbo yao yapate joto wakihofia kustaafishwa kwa lazima.
“Natarajia kuziona sura nyingi mpya kwa kwa sababu kazi ya balozi siyo tu kukaa huko nje, ni kuiwakilisha nchi kwa kufanya kazi zote zinazowahusu, hasa za kidiplomasia. Kwa wale walioshindwa kutumiza wajibu wao lazima waugue kwa sababu wanajua Serikali iliyopo madarakani siyo ya kubebana, uwezo wa kazi ndiyo sifa pekee,” alisema Sanga na kuongeza: “Ukizungumzia balozi maana yake ni mtu anaeweza kuizungumzia nchi yake kule anakoiwakilisha. Kwa kifupi anakuwa pale kama nembo ya Taifa, bila shaka elimu ya kidiplomasia ndiyo inayotakiwa kuwa sifa moja wapo wakati wa uteuzi.”
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), Dk Richard Mbunda alisema ilifika hatua balozi anakosa kazi ya kufanya, kama kuingia makubaliano yoyote kwa niaba ya nchi yake, kutokana na wanaohusika na sekta hiyo kuamua kwenda wenyewe.
“Balozi wa nchi ni kama Rais kule anakoiwakilisha nchi yake. Ndiye msemaji na mtendaji mkuu kwa niaba ya Serikali iliyompeleka hivyo natarajia kuona mabalozi watakaopelekwa na Serikali hii, kuwa ni wale wenye weledi na uwezo mkubwa wa kuiwakilisha nchi yao,” alisema Dk Mbunda.
Mhadhiri mwingine wa UDSM, Patrick Myovela alisema anatarajia kuona sura nyingi mpya kwenye uteuzi wa mabalozi, kutokana na kazi nzito ya uwakilishi wa nchi iliyo mbele yao.
“Kama kuna ambaye hakutimiza wajibu wake, panga haliwezi kumuacha. Kinachotakiwa ni uwezo wa kusimamia maslahi ya Taifa hasa kupitia sera ya uchumi,” alisema. Myovela alisema uwakilishi mzuri wa balozi, unaweza kuongeza wawekezaji ndani ya nchi na hivyo kusaidia katika kukuzwa uchumi.
9 comments:
Balozi za Tanzania nje ya nchi ziangaliwe sana. Wamekuwa wakitumia hela hovyo sana na kukaa kwenye nyumba za kifahari wakilipa mamilioni wakati wanaweza kukaa kwenye apartments za kawaida kabisa kama watu wengine. Matumizi ya mabalozi na staff wa nje ni makubwa mno. Watu wamemaliza vipindi vyao lakini wanakaa nje ya nchi bado hawataki kuwapisha wengine nao waende nje. Tunashukuru Magufuli kwa kweli maana inahitajika discipline kwenye hizi balozi zetu.
Annony hapo juu kweli ana donge zito la chuki ama wivu. Wenzako wameajiriwa na Serikali hivyo kwanza wako kwenye utumishi wa Serikali. Pili kukaa kwenye apartment ama nyumba inategemea mambo mengi. Mbona wako wanaoishi kwenye apartment. Tena kuonyesha kutoelewa kwake hajui kwamba kuna apartment ghali hata kuliko nyumba. Hivyo hilo si swala lenye mashiko. Inaeleza huyu jamaa angetaka hata Rais asiishi ikulu bali mtaani na wananchi wengine. Tatu kazi za kibalozi anaonyesha kutozifahamu na kutozielewa. Hivi kukaa sana nje ndio miaka mingapi? Kazi zao unazipimaje? Unadhani ni sherehe tu? Pole sana!'
tunakuomba njoo na japan
Naunga mkono hoja zote zilizotolewa. Tatizo la kuwabeba mabalozi limekuwa na kasoro kwa muda mrefu. Mabalozi wengi walikuwa wakichaguliwa kwa kubebwa bila sifa maalumu za kidiplomasia. Kwa mfano, kuna balozi zetu hapo awali zimewakilishwa na waandishi wa habari, wanasheria, watangazaji wa redio (RTD), watoto wa vigogo, wabunge walioshindwa, n.k. Ufanisi wa kazi wa wengi wao umekuwa wa kuhuzunisha. Tunayo imani kubwa mheshimiwa Rais JPM atarekebisha mwenendo huu.
Shida nikuwa JK hakuwa serious katika chaguzi zake,alipolitize kila jambo vilex2 alikumbatia nepotism ambayo at the end iliadhiri utendaji katika sehemu zote.
"kuna balozi zetu hapo awali zimewakilishwa na waandishi wa habari, wanasheria, watangazaji wa redio (RTD), watoto wa vigogo, wabunge walioshindwa"
Kuwa mtoto wa kigogo haimaanishi huwezi fanya kazi. Mpime mtu kwa uwezo wake. Carolyn Kennedy ni Balozi wa Marekani Japan. Si mtoto wa kigogo? ameshindwa kazi? Wacheni upuzi? Hao watoto wa vigogo ni nani? Mbona hakuna? Wameshindwa kazi wapi? Asijejua kitu asimpime ajuaye.
Waandishi wa habari, wansheria kuwa mabalozi? Hebu taja sifa za mabalozi popote pale duniani!! Kweli wakati mwingine ukibishana na mpumbavu watu wanaweza wasione tofauti!!!
Jamani JK sio rais tena. Muacheni apumzike kwa heshma tunayowapa viongozi wa Taifa letu. Mengi na ya kujivunia aliyafanya
Anza na Balozi zilivyotolewa kwa kujuana..nepotism. Halafu angalia productivity vs. Matumizi ya Balozi zetu. Kama tunatumia zaidi ya tunavyopata - simple business ethics - funga biashara
Kama tunaweza kuzungumzia mema aliyoyafanya akiwa madarakani vipi iwe dhambi kujadili mapungufu yake.
Post a Comment