ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, January 12, 2016

...Shein ajibu mapigo, asema ‘jiandaeni kwa uchaguzi’

By Hassan Ali, Mwananchi

Zanzibar. Kuna kila dalili kwamba mazungumzo ya kutafuta suluhu ya mkwamo wa kisiasa Zanzibar yamevurugika baada ya wahusika wakuu wa pande mbili, kuzungumza hadharani na kutoa misimamo tofauti.

Wakati Maalim Seif Sharif Hamad wa CUF akiitisha mkutano wa waandishi wa habari Dar es Salaam jana na kusema chama chake hakipo tayari kuona uchaguzi unarudiwa, Dk Ali Mohamed Shein wa CCM amewataka wafuasi wa chama hicho kujiandaa kwa uchaguzi wa marudio.

Akihutubia mkutano maalumu wa CCM wa maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar, uliofanyika Viwanja vya Maisara Suleiman, mjini hapa, Dk Shein amewataka wafuasi wa chama hicho kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa marudio pindi Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) itakapotangaza tarehe.

Rais huyo wa Zanzibar alisema jana kwamba huo ndiyo msimamo wa chama chake na hakijatafuna maneno tangu ZEC ilipotangaza uamuzi wa kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015.

Alirudia kauli yake aliyowahi kuitoa hivi karibuni kwamba yeye ni Rais halali wa Zanzibar kwa mujibu wa Katiba na kama yupo asiyeridhika aende mahakamani ili apate tafsiri sahihi ya kisheria.

Alieleza furaha yake ya kufanyika kwa mkutano huo katika viwanja hivyo ambavyo muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar, marehemu Mzee Abeid Amani Karume alitoa tamko la kufuta ubepari, kupinga dhulma, kutaifisha ardhi na kufuta vyama vyote vya siasa, baada ya kupigiwa mizinga Machi 8, 1964.

Mkutano huo pia ulikuwa ni kilele cha matembezi ya Vijana wa CCM (UVCCM), yaliyoanza Januari 9 katika Jimbo la Kitope, Wilaya ya Kaskazini B, Unguja.

Viongozi mbalimbali wa CCM akiwamo Kaimu Katibu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka ambaye alisema matembezi hayo ni kielelezo cha utayari wa vijana katika kuyalinda na kuyaenzi Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964.

Kuhusu mazungumzo ya kukwamua hali ya mkwamo wa kisiasa wa Zanzibar, Shaka alisema: “leo Januari 11 tunaomba tuanze kuitumia ile kaulimbiu ya Rais wa Muungano ya ‘Hapa Kazi Tu’ kwa kuamua vile vikao vya Ikulu sasa basi au tutahesabu kuwa ni ufujaji wa mali ya umma.”

Wengine waliohudhuria ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi ambaye alisema: “Kuna njama zinafanywa ili vyama vidogo visishiriki uchaguzi lakini sisi tunasema hata ikiwa CCM peke yake tutashiriki uchaguzi.”

Alisema hakuna haja tena ya kuendelea na mazungumzo hayo. “...Tujiandae na uchaguzi wa marudio. Nasikia wenzetu wamejiandaa siku ikitangazwa tarehe ya uchaguzi watatumia nguvu ya umma, sisi tunawakaribisha wafanye hivyo na matokeo yake watakuja kuyaona.”

Kwa upande wake, Samia aliwaomba vijana wadumishe umoja na mshikamano.

Vijana hao wa CCM waliomba uongozi wa chama hicho kumvua uanachama Rais mstaafu, Amani Karume kwa madai kuwa hana masilahi na chama, yeye na familia yake.

“Kwa kauli moja umoja wa vijana wa Chama cha Mapinduzi tunataka avuliwe uanachama na afukuzwe mara moja Amani Abeid Karume,” alisema mmoja viongozi wa umoja huo.

1 comment:

Unknown said...

Ccm na utawala wa mabavu kama kushindwa mlisha shindwa sasa mnatumia nguvu na sio democracia na mnawasiwasi kama hao cuf watawaongoza wazanzibar wataleta mabadiliko nchini na amtapata nafasi ya kutawala tena