Friday, January 22, 2016

Spika Rebecca Kadaga (Mb) wa Uganda afunga Warsha ya siku mbili ya Sekretarieti ya Chama cha Mabunge ya Jumuiya ya Madola Kanda ya Afrika Jijini Dar es Salaam.

Spika Rebecca Kadaga (Mb) wa Uganda afunga Warsha ya siku mbili ya Sekretarieti ya Chama cha Mabunge ya Jumuiya ya Madola Kanda ya Afrika Jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya Wajumbe wa Sekretarieti ya Chama cha Mabunge ya Jumuiya ya Madola Kanda ya Afrika kutoka nchi mbalimbali za Afrika wakichangia mada katika Warsha kuhusu ushirikishwaji wa wanawake katika ngazi za maamuzi wakati wa siku ya ufungaji warsha hiyo iliyofanyika Jijini Dar es Salaam 21-23 Januari, 2016.
(Picha zote na Benedict Liwenga)

Na Benedict Liwenga.

SPIKA wa Bunge la Uganda, Mhe. Rebecca Kadaga (Mb), ambae pia ni Mwenyekiti wa CWP Kimataifa amezihasa nchi Wanachama wa Sekretarieti ya Chama cha Mabunge ya Jumuiya ya Madola Kanda ya Afrika kuendelea kuwathamini wanawake kwa kuwapa vipaumbele vya ushiriki katika ngazi za maamuzi pamoja na kuwaenzi wanawake waliotoa mchango wa maendeleo ya nchi zao.

Spika Kadaga ameyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam wakati akifunga rasmi Warsha ya siku mbili iliyohusu kujadili ushiriki wa wanawake katika ngazi za maamuzi ili kubuni mbinu na mikakati ya kuongeza idadi ya Wanawake katika ngazi za siasa na kijamii.

Mhe. Kadaga ameeleza kuwa, nchi Wanachama hazinabudi kuthamini mchango mkubwa wa wanawake katika masuala ya kijamii pamoja na kisiasa, hivyo kuna haja ya kuwaenzi kwa kutunza nyaraka zao muhimu ikiwemo kuwaendeleza wanawake kielimu ili kuweza kuleta maendeleo katika nchi husika.

“Ni vema tukaaangalia mchango mkubwa unaotolewa na Wanawake katika nchi zetu hususani katika masuala ya kijamii pamoja na kisiasa, basi  nchi zetu hazinabudi kuwajali kwa kuwashirikisha katika ngazi zote muhimu ili kuwe na usawa kati ya wanawake na wanaume, lakini pia kuna haja ya jamii husika kuwaelimisha wanawake hawa ili waweze kuleta mchango mkubwa katika jamii zetu”, alisema Spika Kadaga.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Utendaji ya CPA Kanda ya Afrika, Mhe. Lindiwe Maseko (Mb) kutoka Afrika Kusini, amezidi kuipongeza Tanzania katika hatua nyingine kwa kujali haki na usawa katika masuala ya kisiasa ambapo pia ameimwagia sifa kwa uchaguzi uliopita wa mwaka 2015 kuwa wa huru na haki na kuzitaka nchi nyingine za Afrika kufanya chaguzi zake kuiga mfano huo.

Kwa upande wao Wajumbe wa Warsha hiyo wameendelea kujadili masuala mbalimbali ambayo yanaweza kuleta mabadiliko katika jamii kwa kuhakikisha kuwa wanawake wanapewa fursa sawa na wanaume katika masuala ya kisiasa na kijamii ambapo msisitizo mkubwa unaotolewa katika warsha hiyo ni ‘ushiriki wa wanawake katika ngazi za maamuzi’.

Sambasamba na hilo, suala la kuwashirikisha wanawake kwa njia ya Vyombo vya habari na mitandao ya kijamii limezungumziwa katika warsha hiyo ambapo msisitizo umetolewa wa kutumia mitandao hiyo kwa njia ya kuelimisha umma juu ya nafasi ya mwanamke katika ngazi za maamuzi ambapo endapo ikitumiwa vema inaweza kuleta usawa katika jamii.

Nchi zilizoweza kushiriki katika Warsha hiyo ni Tanzania, Uganda, Kenya, Ghana, Nigeria, Zambia, Mauritus pamoja na Afrika Kusini.



No comments: