TAMKO
LA SHIRIKISHO LA VYAMA VYA TIBA ASILI TANZANIA
(SHIVYATIATA)
KUHUSU
MAELEZO YA WAZIRI WA AFYA ALIYOYATOA TAREHE 15/01/2016, JUU YA TIBA ASILI NA
TIBA MBADALA.
Ndugu waandishi wa Habari na ndugu wananchi,
shirikisho la vyama vya Tiba Asili Tanzania (shivyatiata) ni chombo
kinachosimamia vyama vyote vya Tiba Asili hapa Nchini pamoja na Waganga wote wa
Tiba Asili na pia ndiyo msemaji wao kwa Serikali, Mashirika ya Kitaifa na
Kimataifa na kuhakikisha chombo hiki kinasimamia na kulinda maslahi yote ya
Waganga wa Tiba Asili hapa nchini
Hivyo basi ,kutokana na maelezo
yaliyotolewa na Waziri mwenye dhamana na mambo ya Afya mnamo hiyo tarehe
15/01/2016 shirikisho kwa kutambua dhamana tuliyonayo mbele ya Umma wa Waganga
tunapenda kuwasilisha tamko letu kwenu nyinyi waandishi wa Habari na wanchi kwa
ujumla ili muweze kuelewa yanayoendelea
katika Tiba Asili hapa nchini.
Ndugu waandishi wa Habari, kwanza
mtakumbuka kuwa mnamo tarehe 14/12/2015 Naibu waziri wa Afya maendeleo ya
Jamii, jinsia, wazee na watoto Mhe. Dkt HAMISI KIGWANGALA (MB) alifanya ziara
katika kituo cha Tiba Mbadala cha Tabibu anayejulikana kwa jina la Dr MWAKA.
Baada ya ziara hiyo mengi yalizungumzwa na hata tamko la Wizara lililotolewa
terehe 24/12/2015 lililohusu Tiba Asili na Tiba Mbadala kwa upande mmoja nalo
lilichangia kuwepo kwa malumbano ya hapa na pale kutoka kwa watoa huduma wa
Tiba Asili na Tiba Mbadala, na wengine wakafikia hatua ya kupinga agizo hilo na kuitisha mgomo.
Ndugu waandishi wa Habari tunapenda
mfahamu kuwa Wizara ya Afya katika kufikia
kutoa tamko hilo la tarehe
24/12/2015 hawakushirikisha chombo chenye dhamana ya waganga ambacho ni
shirikisho hili la vyama vya Tiba Asili Tanzania, Lakini kwa kutambua dhamana
tuliyonayo kwa waganga wote wa Tiba Asili na kwa kutambua kuwa popote
panapokuwa na mgogoro basi njia sahihi ni kukaa
mezani kujadiliana ili hatimaye amani ipatikane.
Hivyo sisi Shirikisho tuliomba kikao
na Mh. Waziri wa Afya ambacho kilifanyika tarehe 28/12/2015 na ambacho
kilionesha nuru ya kufikia maelewano, Na kwa kuwa siku hiyo tarehe 28/12/2015 Waziri wa Afya Mhe. UMMY
MWALIMU alitamka mbele ya vyombo vya habari kuwa yupo tayari kukaa kujadiliana
na yeyote Yule ambaye amekwazwa na agizo
la Wizara.
Hivyo sisi shirikisho tuliweza kukaa
na wadau wa Tiba Asili na Tiba Mbadala ambao kimsingi ndiyo haswa walikwazika
na agizo hilo la Wizara na hatimaye tarehe 31/12/2015 tulifanya kikao cha
pamoja kati ya wadau hao, shirikisho, na Wizara ya Afya tukiongozwa na
Uenyekiti wa Mhe. UMMY MWALIMU (MB) ambaye
ndiye waziri mwenye dhamana na mambo ya Afya .
Ndugu waandishi wa Habari napenda
ifahamike kuwa kikao hicho cha tarehe 31/12/2015 tulikubaliana kuwa wale wote
wanaopeleka matangazo yao na vipindi kwenye Baraza kwa ajili ya kuhakikiwa basi
Baraza liwaruhusu kuendelea na program yao hiyo na uhakiki wa Baraza usizidi
siku tatu (3) kwa ujumla makubaliano yote ilikuwa ni utekelezaji wa sheria namba 23 ya
Tiba Asili na Tiba Mbadala ya mwaka 2002 na kanuni zake na pia sheria
nyinginezo za nchi na pia utekelezaji huu uwe wa pande zote, na mwisho Mhe Waziri
alituhaidi kuwa tamko lingine la Serikali litatolewa tukiwa wote.
Lakini katika hali ya kushitua na kushangaza Mhe Waziri wa
Afya ametoa tamko bila ya kutushirikisha sisi wadau wengine kama tulIvyokubaliana
.
Hivyo tunaamini Waziri asingefanya
hivyo kukiuka makubaliano isipokuwa ni kushauriwa vibaya na vyombo vya chini
yake ambavyo vinadhammana ya kumshauri juu ya Tiba na tunaamini hivyo kwa kuwa
viongozi wenye dhamana ya kumshauri walio chini yake wao ni wanataaluma ya
Udaktari wa kisasA, Hivyo wameshindwa kumshauri Waziri vizuri kwa sababu wanapigania maslahi ya Taaluma yaona
hawapo tayari kutoa ushirikiano wa dhati kwa Tiba Asili, lakini tunamuomba Mhe.
Waziri kwa kuwa yeye ni mwanasheria basi aimome sheria namba 23 vizuri ili aweze kujiridhisha.
Tunaamini kuwa viongozi hao walio
chini yake wangetumia nafasi na dhamana waliyo nayo kumshauri Mhe Waziri vizuri
juu ya Tiba Asili bila kuweka mbele
maslahi ya Taaluma yao, basi yote haya yasingetokea .
Ndugu waandishi wa Habari, Tiba Asili
imekuwepo hapa nchini kwa mika mingi kabla ya kuja tiba ya Kisasa ambayo kwa kadri siku
zinavyozidi nayo inazidi kupoteza
umaarufu wake na kuiacha Tiba Asili ikizidi kuchukua nafasi kubwa katika nchi
yetu, Hivyo kitendo cha Tiba Asili na Sasa Tiba Mbadala kuzidi kuchukua nafasi kubwa kwa wananchi ambayo hivi sasa ni asilimia 70%
mijini na asilimia 80% vijijini wanatumia Tiba Asili kitendo hicho kinawakera
hao wanaoitwa madaktari wa kisasa na ndiyo maana maneno yamekuwa mengi kwa
upande huu waTiba Asili na Tiba mbadala na kufikia hata hatua ya kutukejeri eti
kwa nini tunavaa mavazi meupe wakati wa
kutoa tiba?, kwa nini tunaitwa Madaktari
kama wao? Na wengine hufikia kusema eti sisi waganga wa Tiba Asili na Tiba
mbadala unaongoza kusababisha Vifo vya Wagonjwa kitu ambacho siyo kweli hata
kidogo kwani Tiba Asili imeokoa na inazidi kuokoa maisha ya watu wengi mijini
na vijijini, mfano mdogo katika Tiba Asili yapo magonjwa mengi yasiyoambukiza
tunayatibu na pia tunaunga mifupa na waliovunjika hurejea katika hali yao ya
kawaida ndani ya wiki mbili hadi mwezi mmoja kitu ambacho kwa Tiba ya Kisasa
imekuwa ndoto kwao,
Lakini vilevile Tiba hiyo ya Kisasa
ndiyo inaongoza kwa vifo vya watu wengi mijini na vijijini na ushaidi wa hilo
ni uwepo wa mochwari karibu kila
hospitali kwa ajili ya kuhifadhia maiti zitokanazo na watu waliokuwa ni
wagonjwa na wakitibiwa katika Hospitali hizo na hao Madaktari bingwa wa Kisasa.
Ndugu waandishi wa Habari na ndugu
wananchi, shirikisho la vyama vya Tiba Asili Tanzania tunapinga vikali matamshi
yote yanayotolewa yakiwa yanalenga kuidhalilisha Tiba yetu ya Asili ambayo imekuwepo hapa nchini
kwa miaka mingi na kwa sasa tunaiboresha na kuiendeleza ili iwe ya kisasa
zaidi.
Hatupo tayari kuona watoa huduma wa Tiba Asili wananyanyaswa na
kudhalilishwa ndani ya nchi yao, Hii ni nchi yetu sote.
Hivyo hakuna mwenye haki ya kujiona
kuwa yeye na kundi lake ndiyo bora na
wengine siyo bora, yeye ndiyo anahaki ya
kuzungumzia mwili wa mtu na wengine hawana haki hiyo, yeye ndiyo ana haki ya
kuvaa koti jeupe wakati wa kutoa Tiba na wengine haki yao ni kuvaa kaniki.
Kama kuna watu wapo tayari kuona hayo
yanaendelea kutendeka sisi tunasema
hatuko tayari na muda wote hatutokuwa tayari.
Hivyo katika hili tamko lililotolewa tarehe 15/01/2016 na Mhe
Waziri wa Afya tunabainisha mambo gani tunayaunga mkono na mambo gani
hatuyaungi mkono
MAMBO TUNAYOYAUNGA MKONO
1.
Tunaunga
mkono Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala
kuongezwa watumishi wa kutosha lakini wawe na moyo wa kuipenda Tiba
Asili na Tiba mbadala
2.
Tunaunga
mkono kuwepo mpango mkakati kwa muda mrefu kuwezesha kufanikisha
uboreshaji wa Huduma wa Tiba Asili na
Tiba mbadala lakini mpango huo uwe wa vitendo
zaidi.
3.
Tunaunga
mkono watoa huduma wote, vituo vyote vya kutolea huduma, dawa na vifaa tiba
vinasajiliwa .
4.
Tunaunga
mkono mwongozo wa mafunzo kwa watoa
huduma wote nchini kuhusu namna ya kuweka kumbukumbu za wagonjwa , kutoa rufaa kwa
wagonjwa (lakini rufaa hizo ziwe kwa pande zote siyo waganga tu kupeleka
wagonjwa mahospitalini na mahospitali nayo yalete wagonjwa wao kwa waganga wa
Tiba Asili na Tiba Mbadala)
5.
Pia
tunaunga mkono kuwepo kwa mawasiliano kati ya Wizara Afya na Wizara
zinazohusika na mambo ya Habari, OFISI YA RAIS Tamisemi, na Taasisi za utafiti
MAMBO AMBAYO HATUYAUNGI MKONO
1.
Hatuungi
mkono kuondolewa kanuni inayoruhusu
matangazo kwa idhini ya Baraza isipokuwa
tunataka sheria iachwe kama ilivyo juu ya utoaji wa matangazo .
2.
Hatuungi
mkono kuongezwa adhabu kwa sababu hata iliyopo haijawahi kutumika kwa wakosaji
3.
Hatuungi
mkono kuweka ukomo wa usajili mijini na
vijiji kwa sababu tangu usajili uzinduliwe ni miaka mitano sasa na waganga
waliosajiliwa hawazidi elfu kumi na moja (11,000), Hivyo siyo kazi rahisi
kusajili waganga elfu sitini na nne(64,000) kwa muda wa miezi mitatu na sita,
ikiwa wapo watu wamejaza fomu za Baraza
tangu mwaka 2011 na walilipia Ada za
usajili Banki lakini hadi leo hawajapata vyeti, kwa hiyo hata hatua ya
kuwazuia wasitoe huduma hilo haliwezekani.
4.
Hatuungi
mkono kuzuia kuuza dawa au kugawa dawa eti hadi iwe imesajiliwa na Baraza,
kupimwa na maabara ya mkemia mkuu wa serikali na kupewa kibali na TFDA hilo
halikubaliki kwa sababu tunaamini kuwa TFDA ni mmoja ya wanaosababisha migogoro
ya Waganga ikiwemo kutoa vibali vya
waganga kutangaza katika Radio na Televisheni na hali hawaruhusiwi kutoa vibali hivyo
lakini Wizara ya Afya wameshindwa kuikemea TFDA, Tunataka utaratibu wa kupima
dawa, kusajili katika Baraza uende sambamba na uuzaji na ugawaji wa dawa hizo
kwa wagonjwa .
5.
Hatuungi
mkono agizo la kusajili vifaa tiba TFDA
kwani agizo hilo siyo la kisayansi na halitekelezeki kwa mazingira yaliyopo
hapa nchini ambayo hivi sasa wapo watu wengi wananunua na kutumia vifaa tiba
kwa ajili ya kujiangalia Afya zao kwa hiyo siyo kazi rahisi kwa mtu binafsi
kwenda kusajili mashine ya Glukosi TFDA tunataka waachwe wavitumie kwa kuwa wao
ndiyo wanavitumia na kuviamini.
6.
Hatuungi
mkono kuzuia matangazo ya aina yoyote yanayohusu Tiba Asili kwa sababu sheria
inaelezea utaratibu wa kutangaza , na pia tunaomba ifahamike kuwa matangazo
yanayohusu Tiba Asili hayamuthiri mwananchi yeyote ikilinganishwa matangazo ya
sigara na vilevi vingine lakini Wizara ya Afya ipo kimya juu ya matangazo hayo
na kuacha watu wengi wakiangamia kwa kutumia vitu hivyo. Kama hoja ni Tiba
isitangazwe kwa Dunia ya sasa haiwezekani watu ni wengi na vifaa vya kutangazia
vipo, zamani watu walikuwa wachache na
hakukuwa na vifaa vya kutangazia, isitoshe hata Ibada zinatangazwa kwanza ndiyo
utaona watu wanajaa makanisani na misikitini kwa hiyo kusema Tiba isitangazwe
haikubaliki hata kidogojambo la msingi ni kuboresha utaratibu iliopo unaohusu
matangazo na siyo kuuondoa .
Uganga wa Tiba Asili na
Tiba Mbadala siyo jambo la kuhujumu uchumi wala madawa ya Tiba Asili si madawa
ya kulevya . Na pia kuwazuia watoa huduma kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo
vya habari na mikutano ya hadhara kuhusu Tiba Asili na Tiba Mbadala nalo
halikubaliki hata kidogo, Huo ni uvunjifu
wa katiba na ni kinyume cha haki za Binadamu na pia itakuwa ni kuingilia Taaluma ya Mtu,
isipokuwa zuio liwe kwa mtu ambaye si
Mganga.
Hivyo basi kutokana na
hayo tuliyoyaeleza tunaamini kuwa sisi
waganga wa Tiba Asili na Tiba Mbadala tunahujumiwa na tunaamini kabisa wapo
watu hawaitakii mema tiba yetu hii, hivyo tunataka mambo yafuatayo
yatekelezwe:-
1.
Viongozi
wote wenye dhamana ya kumshauri Waziri juu ya Tiba kwa kuwa wameshindwa
kumshauri vema na wameegeme kupendelea Taaluma yaoTunaomba mamlaka ya juu
iingilie swala hili ili haki itendeke
2.
Tiba Asili iundiwe Wizara yake kwa sababu
madaktari wa kisasa sisi tunawapenda
lakini wao hawatupendi wanaona
Wizara ya Afya ni ya kwao peke yao.
3.
Ili
tuwe na Imani na Wizara ya Afya tunataka tuwe na Mganga mkuu wetu wa Tiba Asili
na Tiba Mbadala wa serikali kuliko kuwa na hawa wa kawaida ambao kazi yao kubwa
ni kupendelea Taaluma zao.
4.
Kuanzia
sasa Waganga wote wasajiliwe na shirikisho kwa kuwa ndiyo linaweza kuwatambua
na kuwafuatilia kwa karibu utoaji wao wa huduma na Baraza libaki na kazi ya
kuthibitisha vyeti vyao tu .
5.
Tunataka
heshima ya Tiba Asili ienziwe na siyo kudharauliwa.
6.
Tunataka
waziri mwenye dhamana na Afya awaeleze Watanzania ni watu wangapi wanakufa kwa siku katika hospitali za serikali na za
Binafsi ambazo zina hao wanaoitwa Madaktari bingwa.
7.
Mamlaka
ya juu ya Wizara ya Afya kwa maana ya Ofisi ya Waziri mkuu tunaomba iingilie
kati swala hili, ikae na sisi wadau wa Tiba Asili ili ukweli ujulikane na
muafaka upatikane tunaamini katika
majadiliano, na tunaimani na Serikali yetu inayoongozwa na Mhe.Rais Dkt. JOHN POMBE MAGUFULI.
Ahsanteni sana kwa
kunisikiliza
ABDULRAHMAN
M. LUTENGA
Mwenyekiti
wa Taifa wa Shirikisho la vyama vya Tiba Asili Tanzania
Tarehe
16/01/2016
No comments:
Post a Comment